Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Milima na mabonde ya wanawake katika siasa

10181 WANAWAKE+PIC TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Haikuwa kazi rahisi. Kila mtu anajua Mkoa wa Mara ulivyo na mfumo dume, nilitukanwa sana mpaka kuitwa kahaba lakini hilo halikusababisha nisahau lengo langu.”

Ni maneno ya Ester Bulaya, mbunge wa Bunda kwa tiketi ya Chadema aliyeamua kuingia katika kinyang’anyiro cha kugombea ubunge wa jimbo, tofauti na wanawake wengine wanaochuana na kuridhika katika ubunge wa viti maalumu.

Hii ni baada ya kuwa mbunge wa viti maalumu CCM kupitia Umoja wa Vijana wa chama hicho kwa kipindi cha mwaka 2000/2015.

Bulaya ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alimng’oa mkongwe wa siasa aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri, Stephen Wasira, anasema aliamua kugombea jimbo ili awe mfano kwa wanawake wengine wanaokata tamaa kuwa hawawezi.

“Bunda inaongoza kwa umaskini. Mimi kwa taaluma ni mwandishi wa habari. Niliandika haya lakini sasa nikaona muda umefika kuwa mwakilishi ili niweze kuwasemea wananchi wangu kwa kuwa najua shida zao,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Bulaya ambaye ni mama wa mtoto mmoja, jambo pekee lililompa nguvu ni uthubutu licha ya kutengenezewa mazingira ya hofu dhidi ya mpinzani wake lakini hakuogopa.

“Wakati mwingine wanawake hawafanikiwi kwa sababu wanakubali mazingira wanayotengenezewa na watu wanaowazunguka kuwa hawezi. Hiyo yote ni mfumo dume lakini mimi nilitia pamba masikioni na sikukubali kutoka katika lengo nililojiwekea,” anaongeza.

“Nilijiuliza ikiwa asilimia 50 ya wapigakura ni wanawake, kwa nini niogope kugombea? Nikaamua ku ‘focus’ katika lengo langu kwa kuwa nilifahamu nini nataka.”

Hata hivyo, Bulaya anasema changamoto ya fedha kwake haikuwa kikwazo, kwani haikuwa kipaumbele chake na kwamba alihakikisha watu wanakuwa na imani naye kama watampigia kura hatowaangusha.

“Onyesha kama unaweza kutumia nafasi hiyo endapo utapewa na hakikisha wanakuelewa, nimegombea na mtu mwenye uzoefu na siasa wakati mimi sitoki katika familia ya siasa, baba yangu hakuwahi kuwa hata mjumbe wa shina lakini hilo halikunifanya niogope.

“Nilichangiwa hadi na watu wa kipato cha chini, kuna walionifuata na kusema uwezo wao ni mchele kilo tatu kila siku, wengine mchicha lakini wapo waliokuwa na maduka ya kuuza nyama walijitolea kitoweo ili kila siku ili timu yangu ya kampeni isilale njaa,” anaeleza.

Kuhusu suala la muda, Bulaya anasema kwake nalo halikumsumbua kwani aliweza kupanga ratiba yake ingawa ni kweli kuna wakati kama mama alilazimika kukaa mbali na familia kwa muda mrefu lakini alihakikisha kipindi ambacho yupo anatimiza wajibu wake.

Bulaya anasema mpaka sasa anajivunia hajawaangusha wanawake wenzake na kwamba anaamini kufanya kwake vizuri kunafungua milango kwa wanawake kuaminika.

Hata hivyo, siku zote palipo mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Bulaya anasema changamoto kubwa ni kudhalilishwa, kutukanwa na kufedheheshwa wakati wa kampeni zilimkosesha raha.

“Nilikuwa natukanwa sana, niliumia lakini pamoja na maumivu hayo sikutoka nje ya lengo langu, sikujibu kwa kuwa niligundua wapinzani wangu walikuwa wana lengo la kunitoa katika mstari ili nianze kutapatapa lakini pia nilijua wanaogopa nguvu zangu ndiyo maana walitumia mbinu hiyo.”

Wanawake wasibweteke

Bulaya anawashauri wanawake ambao wamepata nafasi kuzitendea haki ili kuaminika na waliowapa mamlaka.

“Hakuna changamoto duniani ambayo itasababisha ushindwe kutimiza wajibu wako kama bado unapumua, tupeane moyo lakini pia tujifunze kusaidia wengine tunapopata madaraka; siku zote palipo na mafanikio utanyooshewa kidole. Hilo lisiwasumbue badala yake ziba masikio na songa mbele,” anasisitiza Bulaya.

Wengine wanasemaje?

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest anasema vyama vya siasa vyote vina shida ya mfumo dume.

“Wanawake wengi wako nje ya mfumo wa siasa na walio ndani ya ambao wana majukumu ya uteuzi katika kura za maoni ni wanaume, hivyo mwanamke anaanza kunyanyapaliwa kuanzia ngazi ya chama chake,” anasema.

Kwa mujibu wa Anatropia, kwa kuwa wenye mamlaka ya uteuzi ni wanaume ambao wengi wana mfumo dume, hata majina yanayopitishwa asilimia kubwa ni ya wanaume na si wanawake.

Anatropia ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 aligombea jimbo la Segerea kupitia Chadema licha ya kushinda katika kura za maoni, chama chake kilikubaliana kumpitisha mgombea wa CUF, Julius Mtatiro chini ya ushirikiano wa Ukawa.

Mbunge huyo anataja kikwazo kingine kwa wanawake kuwa ni kukosa fedha za kumwezesha kupambana na wanaume.

“Siasa ni fedha, wanawake wengi hawana kipato kikubwa ukilinganisha na wanaume, hivyo hata wanapogombea wanaishia katika hatua za awali kwa sababu tu wanashindwa kwenda sambamba na wanaume,” anasema.

Sababu nyingine ni muda. Anasema, “Siasa inahitaji muda mwingi lakini kama tunavyofahamu mwanamke ana majukumu mengi ya familia ukilinganisha na wanaume, hii ni changamoto kubwa kwani mama hawezi kuacha watoto kwa muda mrefu akaenda kushiriki siasa,” anasisitiza Anatropia.

Diwani wa Viti Maalum (CCM), Kinondoni Hubba Issa anasema licha ya kikwazo cha fedha, hofu na woga pia huchangia kuwavunja moyo wanawake wasijitokeze katika majimbo.

“Wakati mwingine mwanamke anaogopa kujitosa tu kwa sababu ya aliyepo au kukosa ujasiri wa kuthubutu akidhani wapo kina fulani wenye nafasi hizo,” anasema na kuongeza kuwa wakati mwingine wanawake wengi wanakosa taarifa sahihi kuhusu nafasi za uongozi.

Akiounga mkono hoja hizo, Diwani wa Kata ya Ubungo, Rehema Hussein anasema ana uhakika wa kundi kubwa la wanawake kuingia majimboni na kwenye kata kwa sababu vikwazo vingi vinashughulikiwa.

“Sasa hivi tunapata elimu ya kutosha, wanawake wengi hawakuwa na elimu kuhusu masuala ya siasa kwa hivyo tumefunguka ni rahisi kwenda kuchuana na wanaume,” anasema.

Diwani mwingine wa Kinondoni (CCM), Tatu Malyaga anasema “Mwanamke unapochukua fomu ya kugombea wanaume wanaanza kukubeza na kibaya zaidi iwe kwenye hilo jimbo umemkuta mwanaume ambaye amejiwekea himaya kama vile jimbo mali yake, hapo hata usalama wako unakuwa mdogo,” anasema.

Hata hivyo, Tatu anasema katika uchaguzi ujao anatarajia kuona wanawake wengi majimboni kwa sababu sasa fedha si kipaumbele.

Upande wa pili wa shilingi

Tofauti na wanawake wenyewe, wananchi wengine wana mawazo tofauti, Mkazi wa Hananasif Kinondoni, Juma Likote anasema kuwa wanawake hawajiamini ndiyo maana wanashindwa kushindana sawa na wanaume.

“Hata waliopewa nafasi wameshindwa kutushawishi kwamba wanaweza kuongoza, muda mrefu unakuta wanafanya maendeleo na kuanzisha vikundi vya wanawake wenzao na kutuacha wanaume kana kwamba waliowachagua ni wao pekee,” anasisitiza Likote.

Hata hivyo, mawazo hayo yanapingana na ya Hamza Mwinyimkuu mkazi wa Mbagala Rangi tatu ambaye anasema kuwa wanawake wakipata nafasi wanaitumia vyema tofauti na wanaume.

“Kwanza wanawake wana nidhamu na kufanya mambo kwa umakini sana , angalia hata wakiwa barabarani wanaosababisha ajali mara nyingi ni wanaume, hata gari ukinunua kwa mwanamke linakuwa limetunzwa vizuri kwa maana nyingine wakipewa uongozi hawawezi kuwatelekeza wapigakura wao. Ni lazima waende sambamba ili kutatua kero zilizopo,” anasisitiza Mwinyimkuu na kushangaa kwa nini wanawake wanashindwa kuwachagua wenzao wakati ndiyo wapigakura wakuu.

Anasema inashangaza kuona mara nyingi hata majimbo yanayowasimamisha wanawake bado hachaguliwi wakati asilimia kubwa ya wapiga kura ni wanawake, jambo linalohashiria kwamba hawaaminiani.

Vyama vyazungumza

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alikiri kuwepo kwa changamoto ya ushiriki hafifu wa wanawake katika siasa hasa kwenye kugombea majimbo.

Anasema hatua hiyo inatokana na ugumu uliopo hasa katika siasa za upinzani ambazo zimechorwa kipambano hivyo ni nadra kwa wanawake kuingia moja kwa moja.

“Pia, shughuli nyingi za siasa zinazofanyika ikiwamo mikutano ya hadhara ni nadra wanawake kushirikia kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutopewa ruhusu wa watu wao wa karibu,” anasisitiza Shaibu.

Mbali na hilo, Shaibu anakubaliana na mfumo dume kuzidi kutawala kwenye vyama vya siasa, ambavyo vina amini wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ni wanaume peke yake.

“Mfano mzuri angalia katika uchaguzi wa marudio wa Buyungu na kata 77 wanawake wamesimamishwa wangapi kwa vyama vyote?” anahoji Shaibu.

Katika uchaguzi huo, kati ya wagombea 179 sawa na asilimia 96.2 ni wanaume na wagombea 7 sawa na asilimia 3.8 ni wanawake.

Columnist: mwananchi.co.tz