Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mifuko ya plastiki kubakia historia

60231 Pic+plastiki

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mikoani. Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kuanza utekelezaji wa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini, uongozi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Dodoma, Kilimanjaro, Mwanza na Tabora, umedhamiria kuhakikisha vibebeo hivyo vinabakia historia katika matumizi nchini.

Viongozi na watendaji walionukuliwa na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, wameahidi kudhibiti mifuko hiyo sambamba na kutoa elimu na maelekezo kwa wananchi.

Katazo hilo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa bungeni hivi karibuni kwamba kuanzia Juni Mosi ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko hiyo kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

Jiji la Mwanza limeagiza mifuko ya plastiki itikayosalia mikononi mwa wafanyabiashara na watumiaji ifikapo Jumamosi ambayo ni siku ya mwisho kwa bidhaa hiyo kutumika nchini isalimishwe ofisi kuu za jiji eneo la Isamilo, ofisi za watendaji wa kata, mitaa na vijiji.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, ofisa mazingira jiji la Mwanza, Lydia Nyeme alisema wazalishaji na wafanyabiashara wakubwa wenye shehena inayofikia tani moja na kuendelea, watasalimisha bidhaa hiyo Isamilo.

Alisema tayari watendaji wa kata, mitaa na vijiji wamepewa maelekezo ya namna ya kupokea na kushughulikia mifuko itakayosalimishwa kwenye ofisi zao.

Pia Soma

Uwanja wa Ndege wa Mwanza nao umeanza kuchukua hatua kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo kwa kubandika matangazo kuwatahadharisha abiria wanaotoka na kuingia kuhusu matumizi ya bidhaa hiyo kuanzia Jumamosi.

Meneja wa uwanja huo, Pascal Kalumbete alisema kwa kushirikiana na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), wameanzisha kitengo maalumu cha elimu kuhusu katazo la mifuko.

Mwenyeikiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Elibariki Mmari alisema licha ya kuwa na madhara kiuchumi kwa waliowekeza kwenye biashara ya kuzalisha na kuuza mifuko ya plastiki, marufuku hiyo ina faida endelevu kwa Taifa kwa sababu inalenga kulinda mazingira.

Kutoka Iringa, Meneja wa NEMC, Arnold Mapinduzi alizitaka mamlaka za mitaa na miji kutangaza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wananchi kuwasalimisha mifuko.

Wakati NEMC Iringa wakisema hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mbeya, James Kasusura alisema wananchi wameanza kukusanya mifuko hiyo katika maeneo ya kukusanyia taka tayari kwa kupelekwa inakotakiwa.

Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mussa Sima alitoa angalizo kwa mawakala watakaosambaza mifuko mbadala kuwa atakayebainika kupandisha bei atachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema ametembelea moja kati ya viwanda 46 vinavyotengeneza bidhaa hizo na kuelezwa kuwa vifungashio hivyo vitakuwa vinauzwa Sh200 lakini mtaani vinauzwa Sh1,000.

Mkuu wa Wilaya Rombo, Agness Hokororo alisema tayari wananchi na wafanyabishara, wameanza kuelimika juu ya matumizi ya mifuko mbadala, akisema elimu hiyo inaendelea kabla ya kuanza utekelezji wa katazo hilo.

Mkoani Arusha, tayari utaratibu umeshatangazwa wa kuteketeza mifuko hiyo.

Ofisa afya na usafi wa mazingira wa jiji la Arusha, James Lobikoki alisema wafanyabiashara wenye mifuko kuanzia kilo 500 na kuendelea, wanapaswa kuipeleka dampo lililopo eneo la Murieti na walio na kilo chini ya hizo, waipeleke ofisi za Serikali za mitaa.

Imeandikwa na Florah Temba, Yonathan Kossam, Robert Kakwesi, Berdina Majinge, Ngollo John, Peter Saramba na Mussa Juma.

Columnist: mwananchi.co.tz