Novemba 5 mwaka huu Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk John Magufuli itatimiza miaka mitatu.
Kwa hakika sisi tuliopata fursa ya kuwawakikilisha Watanzania wengine katika utumishi wa zama hizi za mageuzi, tuna mengi ya kusimulia.
Ni kwa sababu hiyo basi katika kuelekea siku hiyo mimi na timu yangu tutakuwa nanyi katika ukurasa huu maalum kila wiki siku ya Jumamosi kueleza mageuzi kwenye sekta mbalimbali yaliyotokea katika miaka hii mitatu.
Kwa utangulizi, yatosha tu kusisitiza kuwa miaka hii mitatu ilikuwa miaka ya kazi ya kurejesha misingi muhimu katika ujenzi wa Tanzania mpya, misingi ambayo ukiacha mambo mengine, naamini, ni nguzo kuu za mafanikio katika miaka mitatu ya Rais Magufuli na ambayo inaweza kuongoza zaidi katika utekelezaji siku zijazo.
Nia na dhamira ya maendeleo
Tunapoelekea kufanya tathmini ya mageuzi yaliyotokea katika miaka hii mitatu, ni muhimu kutambua kuwa nia na dhamira ya Rais na wasaidizi wake wote, imekuwa bayana na isiyo na hiyana.
Tunaweza kujadili nadharia mbalimbali za namna ya kufikia malengo ya kimaendeleo yatokanayo na dhamira hizo na kuona kipi kiwe kipaumbele, lakini katika miaka hii mitatu ni mtazamo wangu kuwa nguzo hii ya “dhamira ya maendeleo” imekuwa chachu ya magaeuzi tunayoyaona.
Mtazamo wa kuhakikisha kazi zinafanyika, fedha zinatumika, ubunifu na kujituma kunatumika kuleta maendeleo, ni jambo la sisi kujisifu kwa sababu baadhi ya maendeleo kama tutakavyoyaona katika makala zijazo bila dhamira hii na nguzo nyingine ama yasingepatikana au yangechukua muda mrefu.
Ndio maana hata alipoamua kulifufua Shirika la Ndege (ATCL) wapo walioona hiyo ni ndoto. Alipoahidi kujenga reli ya kisasa na ya umeme, alipoahidi atazalisha umeme mwingi zaidi, wengi walidhani zingebaki kuwa ahadi za kisiasa. Miaka mitatu sasa nguvu ya dhamira imeshinda udhaifu wa woga wa kudhindwa.
Ndege ziko angani, reli watu wako kazini na kwa upande wa umeme megawati nyingi zimeshazalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mageuzi na si mazoea
Katika nadharia ya maendeleo inayoungwa mkono na wasomi na wanamageuzi mbalimbali hasa viongozi wa kimageuzi kama Lee Kuan Yew wa Indonesia au wataalamu wa kusimamia mageuzi kama Profesa Idris Jala wa Malaysia, watakuthibitishia kwamba dhamira na nia tu havitoshi.
Kiongozi mzuri wa kimageuzi ni yule anayekwenda zaidi ya hapo. Anabuni mifumo na kuisimamia katika kuitekeleza kwa mtindo mpya unaoachana na mazoea ya kufanya mambo kwa staili ileile iliyokuwa haileti tija yoyote.
Mimi ni shahidi kuwa katika miaka hii mitatu moja ya miongozo na misimamo muhimu ambayo Rais Magufuli na wasaidizi wake tumetembea nayo ni kubuni na kutekeleza mikakati ya kuleta mageuzi katika kila sekta.
Ililazimu wakati fulani kufanya mambo hata yaliyokinzana na nadharia zilizozoeleka vitabuni na kuwaacha wasomi waliomeza vitabu hivyo kutabiri huenda tungeshindwa. Hatukushindwa na hatimaye tukatengeneza nadharia mpya kutokana na uzoefu wetu mpya.
Kuna watu waliozoea mambo fulani fulani yangebaki kama yalivyo ili maisha yao binafsi yazidi kuwa mazuri (huku wengi wakibaki katika umaskini na ukosefu wa huduma). Mwanzo hawakuelewa, na tuliwaelewa, ilibidi wapige kelele kidogo, leo wanaona manufaa yalivyo kwao na kwa wengi wengine.
Hapa kuna kisa muhimu tutakiona huko mbele cha mageuzi yaliyofanyika katika mashirika yetu ya umma kama Bandari, MSD, TIC, ATCL, NIC, TPDC na TTCL miongoni mwa mengi mengine. Miaka mitatu hii nguvu na nguzo ya ari ya kuleta mageuzi na kuondoa mazoea vimeshamiri.
Kujitegemea au kujitenga?
Inawezekana ikawa ni mazoea kwa baadhi yetu kwamba tunaamini kila maendeleo tunayoyafikia lazima tukope au tuombe misaada kutoka nje. Alipoingia madarakani, Rais Magufuli alianza bayana kukinzana na dhana hii. Awali hakueleweka.
Aliposema Tanzania ina rasilimali nyingi lazima tuhakikishe zinatumika kwa manufaa ya wananchi wetu, aliposema kuna fedha nyingi za umma zinafujwa tupambane kukusanya mapato ili tuelekee kujitegemea na si kila kitu tutegemee misaada, wapo waliofasiri tofauti. Wakajenga hoja isiyoendana kabisa na hoja yetu wakidai Tanzania haiwezi kujitenga na mataifa mengine wala haiwezi kufikia kujitegemea ikiwa peke yake kwa kuwa uchumi wetu ni mdogo.
Hapa, tofauti na waliotunga maswali hayo kwa hoja zao mpya na kujibu mtihani wao, Rais Magufuli hakuwa ameuliza maswali hayo bali swali na hoja yake ilikuwa wazi kuwa tuhakikishe rasilimali tulizonazo za ndani zinakuwa msingi wa kwanza kuelekea kujitegemea na kujiletea maendeleo.Hakusema hatachukua mikopo na misaada. Hakusema atajitenga na dunia.
Miaka mitatu leo tutaona katika makala zijazo jinsi nguzo hii ya azma ya kujitegemea ilivyoleta maendeleo ambayo kama tungetaka kukaa kusubiri maandiko ya miradi yakaridhiwe nje, tungebaki tunasubiri majibu na miradi mingi ikabaki haijatekelezwa.Kujitegemea ndio kipaumbele. Siku alipobadili namna ya kuadhimisha sherehe za Uhuru Desemba, 2015 na kuagiza fedha hizo zikapanue barabara ya Moroko-Mwenge, Dar es Salaam na ambayo leo ipo tayari na inatumika, ndipo wengi wakaanza kuelewa azma hii ya kujitegemea ilimaanisha nini.
Nimepita Mwanza juzi nikitoka mkoani Geita na kujionea mandhari nzuri ya daraja la juu la wapita kwa miguu la Furahisha, Mwanza. Siku Rais alipoahirisha maadhimisho ya Muungano na kuagiza fedha zikajenge daraja hilo na sasa limekamilika na wananchi wanalitumia ndipo akaeleweka zaidi.
Hayo ni madogo lakini muhimu.Kuna kisa tena cha kuifufua ATCL kwa fedha za ndani mpaka sasa shirika hilo liko hai tena likiwa na ndege nne angani ikiwemo ya kisasa kabisa ya Boeing Dreamliner huku nyingine 3 (Dreamliner 1 na Airbus A220-300) zikitarajiwa kufika nchini kati ya Novemba mwaka huu na Oktoba mwakani.
Rais Magufuli hajakomea hapo, ameanza tena, kwa kutumia fedha za ndani, kujenga reli ya kisasa ya umeme kwa kipande cha Dar-Morogoro-Dodoma. Ameanza kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme wa Rufiji utakaozalisha megawati 2,100 zitakazomaliza rasmi tatizo la uhaba wa umeme. Azma ya kujitegemea pia haiwezi kuwa ya dhahiri iwapo mapato hayakusanywi na yakikusanywa yanatumika visivyo. Ni kama nilivyoeleza awali kuna mambo ilibidi tusiende kwa mtindo wa kimazoea bali kimageuzi.
Mengi yamefanyika hadi leo tumetoka wastani wa kukusanya mapato ya bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia wastani wa trilioni 1.3 kwa mwezi. Hivi karibuni Taifa lilipata mstuko tena kusikia mabilioni ya mapato yasiyo ya kodi yaliyokuwa hayakusanywi kutoka taasisi mbalimbali za umma.
Kupitia gawio (kwa kampuni zinazozalisha faida na zile zinazolipa asilimia kati ya 10 hadi 15 ya mapato yao ghafi ya mwaka) kiasi kingine kinachofikia karibu trilioni moja kilikusanywa na fedha hizi zitatumika kutekeleza mradi mwingine mkubwa na wa kihistoria kwa Watanzania utakaotangazwa hivi karibuni.
Kwa hiyo niseme tu kwamba dhamira ya kujitegemea imetupa shauku na ubunifu wa kukusanya zaidi na kuondoa mianya zaidi ya uvujifu wa ukusanyaji wa mapato. Mianya hii ilikuwa inalipotezea Taifa fedha nyingi kwa kiwango cha kuwakosesha wananchi huduma muhimu za kijamii.
Dk Hassan Abbasi ni msemaji mkuu wa wa Serikali
[email protected].