Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mgumba alivyozichanga karata kwa JPM

10666 Pic+mgumba TanzaniaWeb

Thu, 5 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siasa ni kama mchezo wa karata, ukizichanga vizuri unaweza kulamba dume na ukizichanga vibaya unaweza kuambulia galasa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba ambaye hivi karibuni alizichanga ipasavyo.

Mgumba ambaye ni mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM) alizitumia vizuri dakika 15 kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/19 jijini Dodoma, Juni 22 hadi Rais John Magufuli kumpongeza baada ya kumwapisha.

Akichangia bungeni, Mgumba alizungumzia suala la ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi (export levy), ambako mjadala kuhusu zao hilo ulikuwa umepamba moto kwa wabunge wa mikoa ya Kusini kuungana na wengine kuibana Serikali.

Juzi, Rais Magufuli baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi mbalimbali akiwamo Mgumba, alimpongeza huku akimnyooshea kidole Mwenyekiti wa Bunge aliyekuwa kiongozi wa shughuli za Bunge siku Mgumba anachangia bila kumtaja jina. Hata hivyo, siku hiyo alikuwa Andrew Chenge.

“Nakupongeza (Mgumba) kwa mchango wako ulioutoa bungeni, mimi nafuatilia bungeni wanaochangia na huwa nawaangalia kweli wabunge wa CCM ambao wengine wanajisahau wanashindwa kuelewa kwamba tuna jukumu la kujibu ilani ya CCM nao wanageuka kule,” alisema Rais.

“Utakuta mtu anazungumza tukienda hivi tutashindwa, kwa nini unaendelea kuwa humo, si ondoka.”

Katika michango yao wakati wakichangia, baadhi ya wabunge wa CCM akiwamo Nape Nnauye (Mtama) na Abdallah Bulembo (kuteuliwa) walisema suala la korosho linaweza kuifuta CCM katika mikoa ya Kusini.

Nape alisema, “Mapendekezo haya yanakwenda kuiua CCM Kusini, yanakwenda kutuweka mahali pagumu sana.”

Bulembo alisema kazi waliyoifanya mwaka 2015 katika mikoa ya Kusini ilikuwa ngumu. “Pelekeni haraka fedha za korosho jamani. Mnapotaka kuua zao la korosho, pamba na kahawa kwa wakulima mnawaza nini? Hivi hiyo hela ni yetu kweli? Hivi hamjui kilichotokea Mtwara kweli au mmeweka pamba masikioni?” alisema.

Rais Magufuli akiendelea kumpongeza Mgumba alisema, “Wewe nakupongeza sana, ulisimama, nilikuwa nafuatilia vizuri, mwenyekiti akawa anajaribu kukuzibaziba wa kikao cha siku hiyo. Na kwa sababu mwenyekiti huyohuyo alihusika kuzitengeneza hizo sheria mbaya za wakati ule.”

Rais Magufuli alisema, “Alishiriki kuharibu hizo sheria, akawa anakuzibaziba hukukata tamaa, ukavumilia, akaruhusiwa mtu wa kukupiga, ukavumilia, akaruhusiwa mwingine. Nakupongeza, nikasema wewe unastahili hiki ulichokipata. Nenda kashirikiane na wenzako katika Wizara ya Kilimo, mkafanye mabadiliko makubwa. Wizara ya Kilimo inaajiri watu zaidi ya asilimia 70, tukawatendee mema wakulima wetu.”

Juni 22, Mgumba akichangia bungeni alitumia muda mwingi kuelezea historia ya ‘export levy’ huku wabunge Kabwe Zitto (Kigoma Mjini-ACT-Wazalendo), Hamidu Bobali (Mchinga-CUF) na wengine wakisimama kumpa taarifa.

Alivyozichanga karata

Katika mchango wake alisema, “Suala la export levy kutokana na hali ninayoiona na jambo hili tukiliacha likaendelea hivi, linaweza kugawa Bunge letu, linaweza kugawa Serikali yetu na linaweza kugawa Taifa. Upotoshaji ukikaa muda mrefu ambao siyo sahihi. Suala la export levy lina historia ndefu tofauti na hapa tunapojadili na sababu hizi ni za kisheria kama unavyojua mwenyekiti kazi ya Bunge ni kutunga sheria, Serikali ni kusimamia sheria na Mahakama ni kutafasiri sheria.

“Nazungumza hapa nikiwa na Finance Bill (Muswada wa Fedha) ya mwaka 2010 ambayo inafanyiwa rejea na watu wengi kwamba hizi fedha kama zinaonekana Serikali imeenda kuwapora watu wa Kusini ambao ni pesa zao, walikubali wakatwe kwenye korosho kwa ajili ya maendeleo ya kwao, lakini Serikali hii bila huruma imeenda kuzichukua bila kuwashirikisha wao. Niseme sio kweli.”

Mbunge huyo alisema kwa mujibu wa Muswada wa Fedha wa mwaka 2010, sheria namba 203 iliyoanza mwaka 1984 na marekebisho yake ya mwaka 2002, 2006 mpaka mwaka 2010 kifungu cha 17A hizo ni fedha za Serikali.

Alisema kifungu cha 17A kinaeleza kuwa mgawanyo utakuwa asilimia 65 zitapelekwa katika wilaya zinazozalisha korosho lakini bado ni fedha za Serikali na si kwamba zimeporwa kwa wananchi.

Zitto akampa taarifa

Kauli hiyo ilimsimamisha Zitto aliyemuomba mwenyekiti amruhusu kumpa taarifa Mgumba. Alimruhusu na alianza kwa kusema, “Namheshimu sana mheshimiwa Mgumba na ni mara chache sana mimi kusimama kutoa taarifa wakati mbunge anazungumza.”

Kisha akaendelea, “Lakini mheshimiwa mwenyekiti, mheshimiwa Mgumba ama anazungumza jambo ambalo halifahamu au ameamua kupotosha makusudi.

“Mimi nilikuwa mjumbe wa kamati ya fedha ambayo ilifanya marekebisho ya Sheria ya Korosho ya mwaka 2010 na katika majadiliano yale na wabunge kadhaa wa kutoka mikoa ya korosho akiwamo Mzee (George) Mkuchika walikuwamo.”

Zitto alisema pendekezo la kupeleka asilimia 65 ya fedha za ‘export levy’ halikuwa la Serikali, bali wakfu wa korosho ambako muswada wa fedha uliopelekwa na Serikali haukuwa na hilo pendekezo. “Tunaposema asilimia 65 ni fedha za korosho, ni kwa sababu kulikuwa na mkutano wa wadau wa korosho wakapendekeza hivyo. Maelezo anayotoa Mgumba ya reference (rejea) ya finance bill sio maelezo sahihi,” alisema Zitto ambaye ni pia Kiongozi wa ACT-Wazalendo.

Baada ya Zitto kumaliza, Mwenyekiti Chenge alimuuliza Mgumba, “Unasemaje kuhusu taarifa hiyo?”

Hata hivyo, Mgumba alisema, “Kama ndugu yangu Zitto anavyoniheshimu na mimi namheshimu sana na yeye anafahamu hivyo, tunaheshimiana sana na nakubali sana maneno yake, lakini sizungumzi maneno ya mitaani, nimesema ninayo Finance Bill ya mwaka 2010 na nitaiwasilisha mezani.

“Hiyo taarifa siipokei kwani mimi naongea mambo ya kisheria na kwa bahati nzuri nieleze kama anavyosema siijui, ni vizuri akajua siongei kitu kama sijui, nimekaa katika korosho kwa miaka 19.”

Aliendelea kusisitiza, “Suala hili sheria ilianza mwaka 1984 baada ya zao hili kudorora nchini, tulifikia uzalishaji zaidi ya tani 174,000 lakini zilishuka hadi tani 16,000 kwa mwaka na ndiyo Serikali ya Awamu ya Kwanza ikaamua kuja na mkakati maalumu wa kufufua zao hili mwaka 1984.”

Mgumba alisema mwaka 1985 ilianzishwa sheria ya kuanzisha Bodi ya Korosho (CBT) kwa ajili ya uendelezaji na kufufua zao hilo, mwaka 1990 ulianza ubinafsishaji wa mashirika na kuwakaribisha wafanyabishara binafsi kutoka duniani kote kuja nchini kushirikiana kufufua zao hilo.

“Mwaka 1994 kampuni niliyokuwa nafanyia kazi ya Olam International ikaja hapa nchini na kuanza kununua. Wakati huo export levy haikuwepo, tulikuwa tuna- export asilimia sifuri,” alisema.

Aliongeza kuwa lengo la kulifufua zao hilo lilikuwa ni kuviwezesha viwanda 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Mwalimu Nyerere mwaka 1978/1979.

“Kwa ajili ya kubangua, tulikopa mkopo wa Benki ya Dunia (WB) hivyo viwanda 12 vyote vinajulikana, havikubangua hata korosho, korosho yote ikawa inakwenda nje.

“Ndiyo likaja wazo la kuvilinda viwanda vyetu, ndiyo wazo la kuweka export levy, ndiyo ikaja finance bill na kubadilisha sheria mwaka 1996 na ndiyo tukaweka ushuru wa kwanza wa export levy wa asilimia tatu,” alisema.

Taarifa ya Bobali

Baada ya kueleza hayo, Bobali alisimama kumpa taarifa Mgumba huku kukiwa na kelele za hapa na pale bungeni na Chenge alisema, “Waheshimiwa wabunge, mimi ndiyo naongoza kikao na historia ya suala hili naifahamu.”

Kisha alimruhusu Bobali kutoa taarifa ambaye alisema, “Kwa kweli anayoongea (Mgumba) yanaudhi sana.

“Nampa taarifa kwamba kama analolisema ni sahihi fedha hii inapaswa kuwa ya Serikali kwa asilimia 100, iweje leo Serikali ilete finance bill kwa ajili ya kufanya marekebisho ya fedha ya tasnia ya korosho yote ichukuliwe na Serikali, kama Serikali haijui kwamba fedha hiyo inapaswa kwenda katika zao la korosho kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho.

Alipomaliza kutoa taarifa, Chenge alimuuliza Mgumba, “Unasemaje kuhusu taarifa hiyo.”

Mgumba alisema, “Yaani amenipeleka nyumbani, hili suala la kukusanya fedha zote kwenda Mfuko Mkuu wa Hazina halijaanza katika korosho, tulianza (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) Ewura zote zinakwenda Hazina, (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania) TCRA zote zinakwenda Hazina.”

Alisema suala la korosho ndani ya ‘finance bill’ iliyowasilishwa bungeni lililenga kuondoa kipengele namba mbili kwenye matumizi ya fedha kwa mujibu wa sheria iliyotaka asilimia 65 iende kwenye wilaya zinazolima korosho katika mikoa ya Kusini.

Alichosema Chenge

Aliposema hivyo, Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe alisimama kutaka kumpa taarifa Mgumba huku Zitto akisikika akisema, “Kwa nini mwenyekiti (Chenge) usifafanue hili jambo.”

Change alisema, “Hapana. Niwasihi wabunge muachane kumpa taarifa hizo (Mgumba), kwa sababu mbali na Serikali kupitisha haya ya bajeti kuu, wiki ijayo mtapata uamuzi, tutakuja sasa kwenye muswada wenyewe ambao mapendekezo haya yapo.

“Yeye ana haki ya kulielezea kama anavyoona hata kama amejielekeza kusiko na ninyi mtakuja kulinyoosha kwa maelezo ambayo mtaona ni sahihi, mimi kama ‘moderator’ nalifahamu sana suala hili nitakuja na mimi kutoa mchango wangu mbele ya safari.”

Kisha Chenge alimruhusu Mgumba kuendelea ambaye alisema mwaka 1996, iliwekwa asilimia tatu kwa ajili ya ‘export levy’ lakini bado korosho ikawa inakwenda zaidi ya asilimia 90 nje ya nchi na lengo halikufikiwa.

Alisema ilipofika mwaka 2002 Serikali iliongeza kutoka asilimia tatu kwenda tano.

Mbunge huyo alisema licha ya kuongeza asilimia tano, korosho iliendelea kupelekwa nje na hapo ndipo ukaanza mgawo.

“Wakasema kwa sababu lengo la kuzuia korosho isiende nje ni korosho kuwa chache, ni vizuri tutunge sheria tuzigawanye sehemu ya asilimia 65 iende katika wilaya zilizochangia zao hili kufikia mapato yao.

“Asilimia 35 ziende CBT wakati huo mfuko haukuwepo kwa ajili ya kuendeleza zao hili ili kunyanyua uzalishaji na baada ya uzalishaji kuwa mkubwa korosho zitakwenda nje na viwanda vyetu vitapata,” alisema.

Alisema lakini baada ya juhudi zote hizo bado korosho ilikuwa inakwenda nje zaidi ya asilimia 90.

Columnist: mwananchi.co.tz