Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mchape adui ucheke na wanawe

42111 Gaston+Nunduma Mchape adui ucheke na wanawe

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Habali za reo mtazamaji wa TV yako bola. Kalibu kwenye abali mbarimbari zilizojili urimwenguni ndani ya juma rililopita. Plizenta wako ni Lahma Lamazan a.k.a Lihana na kwenye kamela yupo Abdur Kalim”.

Ukisikia ufunguo wa namna hii badili haraka masafa kwenye simu au kompyuta yako maana utapotoshwa. Haiwezekani mtu aliyechukua jukumu la kukupa habari akakosea kila neno la utangulizi. Bila shaka ataikosea hata habari yenyewe. Jamaa mmoja alitaka kuizungumzia POLIARIO. Akaanza na kirefu chake: “Popurar Flont for ze Ribelation of Saguia er Hamala and Lio de Olo” badala ya Popular Front for the Liberation of Saguia el Hamra and Rio de Oro. Msikilizaji unajiuliza; mtangazaji ameathirika na Upungufu wa Silabi Ulimini?

Au ni swaga za ujana? Maana anazibadili “ri” kuwa “li”, na “li” kusikika “ri”. Wana matatizo yao; Niliwahi kumwona dada anayelala na nguo ya kutokea halafu anatoka na nguo ya kulalia! Pia kuna kaka anayeshusha nguo ya nje na kuilazimisha ya ndani kuziba pengo.

Ni ukweli kuwa yapo makabila yanayokosa baadhi ya herufi kwenye lugha zao. Kwa mfano Wakurya huwa hawana “L”. Akitaka kusema “lakini” atasema “rakini”. Ukisikia anasema “rakini sitaki lawama” ujue si mmoja wao kwani hawana usajili wa “L” katika herufi zao. Hiyo ndiyo inayonifanya niamini kuwa watangazaji wa kizazi kipya wana makusudi yao. Bora mtu anayesema “thubu” badala ya supu utajua kuwa ni Mpare, au “ntoto” utajua Chinga alikusudia kusema “mtoto” kuliko mtu anayesema “Laisi Magufuri”. Mpaka sasa sijaelewa wanasumbuliwa na nini.

Unapohamia kwenye nyumba mpya si ajabu ukahama na angalau kunguni wako wawili. Hivyo tulipoingia kwenye Kiswahili ni wazi tulikwenda na vijitabia kutoka kwenye makabila yetu ya asili (Mother tang). Vijitabia ambavyo havibadiliki kirahisi kwa sababu si vya kufundishwa darasani, bali hujijenga kwa mtoto kabla hajaanza kuongea.

Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha nyingi sana. Kuna Kijerumani (shule, meza), Kiingereza (sketi, baiskeli), Kiarabu (nidhamu, karatasi) na kadhalika. Hivi vitu havikuwa asili yetu, kwa hiyo tuliviita kwa majina vilivyokuja navyo. Hata wao wanapata shida kutamka “ugali”.

Haya yanaletwa na Alfabeti. Hili ni neno muunganiko wa Alfa na Beta (ya kwanza na ya mwisho) kutoka kwa Wagiriki.

Mtangazaji anayesumbuliwa na changamoto hizi haniumizi kichwa. Mfano wengi wanaotoka bara wamezoea “mutu” badala ya ‘mtu’ na ‘mutoto’ badala ya “mtoto”. Wazambia wakitaka kusema “mbwa” hutamka “umbwa”. Haya sijafikia kuyaita makosa.

Ila yapo makosa ya kila siku katika matamshi. Unaweza kudhani yanatokea kwa bahati mbaya sana, lakini yakishakuganda huwa yanakung’ang’ania. Kwa mfano “Hosiptali” badala ya “Hospitali”. “Briskefu” badala ya “brifkesi” na “kusheherekea” badala ya “kusherehekea”. Asili ya neno hili ni “sherehe” na siyo “shehere”.

Utasikia “toka nje” badala ya “toka ndani” (ili uende nje). Au “kaondoka Mbagala” badala ya “kaenda Mbagala”. Pia kuna usemi wa “nimemkuta hayupo” badala ya “sijamkuta”. Utamkutaje mtu asiyekuwepo?

Lakini yapo makosa ya kisarufi ambayo wakosaji huamini kuwa wakosoaji ndio waliokosea. Maneno kama “Hii nyimbo imeimbwa na fulani”. Tambua tofauti ya umoja na wingi. Tofautisha kati ya “wimbo” na “nyimbo” kama ilivyo kwa “ungo” na “nyungo”.

Au unaposikia MC akisema “Kwa niaba yangu mwenyewe” fahamu kuwa “niaba” ni neno la uwakilishi kwa asiyekuwepo. Huwezi kusimama na kujiwakilisha mwenyewe. Hii haitofautiani sana na sentensi ya “Nitapita barabara ya Kilwa Road”. Barabara na road ni kitu kimoja. Mwenzenu mmoja alijitetea Mahakamani kwa kusema: “Mimi nakataa katakata kwamba sijaiba.” Matokeo yake alifungwa kwa kuukataa katakata utetezi wake wa maandishi kwamba hajaiba. Kwa hiyo alikubali kwamba aliiba.

Miaka ya nyuma Redio Tanzania ilikuwa na wasikilizaji wengi. Pengine kutokana na kuwa chombo pekee cha habari kwa Tanzania Bara. Lakini tulishuhudia ikiendelea kuwa hivyo hata baada ya kuanzishwa redio zingine za binafsi. Mimi naamini kuwa weledi ndiyo iliyokuwa silaha yao kuu. Habari zilikuwa za uhakika, lugha ilikuwa sanifu, ulinzi wa maadili ulikuwa wa hali ya juu na uzalendo halisi ulizingatiwa.

Idhaa ya Taifa iliwekeza katika habari, matukio na burudani za nyumbani, Idhaa ya Biashara ilifanya burudani na matangazo, External Service ilijikita kwenye habari, burudani na matangazo ya nje kwa Kiingereza. Hakuna aliyeshindwa kusikiliza redio hii.

Kwa sasa wafuatiliaji wa habari na matukio kwa njia ya mtandao wamekuwa wengi. Vijana wameichukulia fursa hii kuwa sehemu ya ajira na wanajituma kwelikweli kutafuta na kutoa habari zinazotambaa duniani kote. Ni jambo zuri sana. Lakini kama wangetaka kufanikiwa wangezingatia yale yaliyozingatiwa na babu zao wa RTD, kisha ndio wangejumlisha na haya wanayoyatoa sasa. Nina maana ya weledi.

Si lazima kila mmiliki wa TV ya mtandaoni awe mtangazaji, bali anaweza kutoa nafasi kwa watu wenye vipawa vya kutangaza ili chombo chake kipasue anga.

Nina maana hii: si lazima mmliki wa saluni aweke picha yake kuvutia wateja. Atafanya hivyo iwapo tu ana mvuto kwa wateja wake. Na ndiyo maana saluni nyingi zinabebwa na picha za akina Beyonce, Drake na wanamitindo maarufu ulimwenguni.

Siku moja nilisoma katuni ya Kingo iliyomwonesha mtoto akilia kwa kuiogopa picha iliyochorwa kwenye saluni ya kike. Mama wa mtoto alimbembeleza mwanawe kwa kumwambia “usiogope mwanangu, hakuumi”.

Kwa hiyo wamiliki wa TV Online wasilazimishe. Kama wana matatizo na usomaji na mvuto wawaajiri wenye fani zao, na watashangaa mafanikio yatakavyojibu.



Columnist: mwananchi.co.tz