Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbunge adaiwa kuhonga majembe, matokeo yake yapingwa mahakamani

101701 Uchaguzi+pic Mbunge adaiwa kuhonga majembe, matokeo yake yapingwa mahakamani

Wed, 8 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kesi za kwanza kabisa zilizohusu uchaguzi ziliibuka baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1980 kutangazwa.

Baadhi ya walioshindwa walikwenda mahakamani kupinga waliotangazwa kuwa washindi.

Miongoni mwa wabunge ambao ushindi wao ulipingwa mahakamani ni Simon Chiwanga aliyeshinda Wilaya ya Uchaguzi ya Dodoma Mjini na Chediel Mgonja aliyeshinda Wilaya ya Uchaguzi ya Pare.

Miamba miwili hiyo, Chiwanga na Mgonja, ilipelekwa mahakamani na hatimaye kushindwa kesi dhidi yao.

Akiwa Waziri wa Elimu ya Taifa, Chiwanga alishindwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 26, 1975. Chiwanga alikuwa mmoja wa wabunge walioshinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1970.

Hata hivyo, zaidi ya asilimia 75 ya wabunge wa Bunge lililotokana na uchaguzi huo wa 1970 walishindwa katika uchaguzi wa Oktoba 1975, Chiwanga akiwa miongoni mwa walioshindwa.

Pia Soma

Advertisement
Miongoni mwa wabunge walioanguka kwenye uchaguzi huo pamoja na Chiwanga ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini, Musobi Mageni Musobi na Waziri Mdogo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Saleh Tambwe.

Chiwanga ambaye aligombea kiti cha Dodoma Mjini mwaka 1975, alishindwa na Severino Supa aliyepata kura 24,865. Chiwanga alipata kura 20,507. Kura zilizoharibika zilikuwa 749.

Lakini katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1980, Chiwanga aliibuka mshindi dhidi ya Supa. Ulikuwa ni uchaguzi wa wabunge wenye mvutano mkubwa kuliko yote Tanzania ikilinganishwa na chaguzi nyingine zilizotangulia.

Kumbukumbu zinatuonyesha kuwa katika uchaguzi huo wa mwaka 1980, Chiwanga alipata kura 34,107 dhidi ya kura 25,339 alizopata mpinzani wake, Supa. Kura 914 ziliharibika, ingawa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 75,010, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 60,360.

Baada ya kushindwa uchaguzi wa 1980, Supa ambaye alishinda uchaguzi wa 1975, alipinga ushindi wa Chiwanga mahakamani kwa kigezo kwamba ushindi huo ulitokana na kuhonga majembe kwa wapiga kura wa kijiji cha Nkong’onta ambako sasa ni Chuo Kikuu cha Dodoma.

Supa alishinda kesi hiyo na Chiwanga akanyang’anywa ubunge, na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza mbunge kushinda kesi ya kupinga matokeo mahakamani, kilichofuata ni uchaguzi ndogo ambapo walioomba kupendekezwa ni pamoja na Supa mwenyewe.

Hata hivyo, Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilikata jina lake na kuweka wagombea wawili wapya ambao ni Marehemu Sala Mwenge na Donald Kusenhta, mshindi akawa ni Sala Mwenge.

Kesi nyingine iliyovutia zaidi kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1980 ni ile ya mpiga kura William Bakari na dhidi ya Chediel Yohane Mgonja. Wapiga kura hao walikuwa wakipinga ushindi wa Mgonja wakidai kuwa ushindi huo si halali. Ingawa Mgonja hakushinda kiti chake cha Pare katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1970, alishinda katika uchaguzi wa 1975 na wa 1980.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1980 Mgonja alipata kura 17,156 dhidi ya kura 14,464 alizopata mpinzani wake, Francis Manongi. Kura zilizoharibika ni 895. Waliojiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo walikuwa 35,628 na waliojitokeza kupiga kura ni 32,545

Kulingana na kumbukumbu, kati ya mwaka 1965 na 1967 Mgonja alikuwa Waziri wa Maendeleo na Utamaduni na ambaye kwa wakati huo aliweka rekodi ya kuwa waziri kijana kuliko wote Tanzania.

Mgonja ambaye mwaka 1967 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi (Mambo ya Nje) na mwaka 1968 akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu, alikuwa ndiye Waziri aliyetoa tamko la serikali ya Tanzania kuitambua Jamhuri ya watu wa Biafra iliyojitenga na Nigeria mwishoni mwa miaka ya 60. Hadi wakati wa uchaguzi wa mwaka 1970 Mgonja alikuwa Waziri wa Elimu.

Ingawa hakurudi bungeni katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1970. Mwalimu Julius Nyerere alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Tanu Mtwara. Huo ni uteuzi pekee ambao Mwalimu alimjulisha kabla hajautangaza. Ilikuwa ni kipindi cha madaraka mikoani na vita ya ukombozi ya Msumbiji. Mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya pili, ukifuatia Dar es Salaam katika kuchangia vita vya ukombozi.

Katika shauri hilo namba 84 la mwaka 1980 lililofunguliwa na William Bakari na mwenzake dhidi ya Mgonja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama Kuu iliamua kuwa, mpiga kura ana haki kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Walalamikaji walishinda.

Katika uchaguzi huo huo wa mwaka 1980 Mgonja alidaiwa kuwa aliiba kura na kwa sababu hiyo ushindi wake haukuwa halali. Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilimhukumu Mgonja kutoshiriki uchaguzi kwa kipindi cha miaka 10.

Mgonja ana historia ndefu, tangu Chuo Kikuu cha Makerere Uganda miaka ya 1950 mwishoni hadi kuwa mbunge na waziri mwenye umri mdogo zaidi mwaka 1965 kwa kumwondosha kwenye nafasi ya ubunge Elias Kisenge, aliyekuwa katibu mkuu wa Tanu katika Uchaguzi wa Jimbo la Same Mkoa wa Tanga wakati Same ikiwa ni sehemu ya Mkoa wa Tanga.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1980 kulikuwa na ushindani mkubwa katika nafasi ya Ubunge kuliwakilisha Jimbo la Same, pamoja na ushindani huo Mgonja alishinda uchaguzi ule.

Ushindi ule haukuwaridhisha washindani wake, hivyo wakaupinga kupitia wapiga kura na mahakama ya arufani ikawapa haki.

Kesi hiyo iliendeshwa kwa karibu miaka miwili, kuanzia mwaka 1981 hadi 1982, hadi hukumu ilipotolewa.

Ingawa awali Mgonja alishinda kesi kwa kigezo cha kwamba wapigakura hawana haki ya kupinga ushindi wa mgombea, kwenye rufaa katika Mahakama ya Rufaa wadai hao walifanikiwa kupata haki hiyo baada ya mahakama ykusema mpigakura ana haki ya kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo alikuwa ni Jaji Joseph Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu.

Licha ya hukumu hiyo, mwaka 1983 Mwalimu Nyerere alimteua Mgonja kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga licha ya kuwa adhabu yake ya kutojihusisha na nafasi za kisiasa kwa muda wa miaka 10, ambayo alikuwa haijatumikiwa hata kwa mwaka mmoja.

Columnist: mwananchi.co.tz