Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbinu za kukabiliana na udhalilishaji kazini

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika makala yaliyopita, tuliona kuwa wakati mwingine tunafanya kazi na watu wanaotudhalilisha. Hawa ni watu wenye tabia ya kukosoa kupita kiasi, kupuuza wengine, kukejeli, kuwafanya wengine wajione hawana thamani kama binadamu wanaostahili heshima.

Aina nyingine ya udhalilishaji ni kufanya kazi na mtu anayependa kutoa maelekezo mengi kupita kiasi, anayefuatilia watu kupindukia, lakini pia mtu anayependa kulazimisha vitu vifanyike hata kama kwa kufanya hivyo anaingilia faragha na imani za watu wengine.

Ingawa wakati mwingine udhalilishaji unaweza kugeuka kuwa sehemu ya maisha ya kazi, lakini madhara yake ni makubwa. Mbali na watu hupoteza ari ya kazi kwa migogoro isiyo na sababu. Hapa ninakuletea baadhi ya mbinu za kukabiliana na tabia hizi mbaya.

Fahamu namna ya kujilinda

Watu wengi wanaopenda kudhalilisha mwingine, kisaikolojia, huwa wana matatizo ya nafsi.

Hawa ni wagonjwa wa nafsi wanaofurahia kuona wenzao wanaumia. Machozi ya wengine ndiyo furaha yao. Jifunze kuishi na watu wa namna hii.

Pia Soma

Kwanza wahurumie. Chukulia tabia hizo za kufoka na kuwabana wengine kama namna yao ya kushughulikia historia ya malezi mabaya utotoni. Mtu wa namna hii, usimpe nafasi ya kuwa karibu na wewe. Lazima atakuumiza.

Kama ni bosi, pokea maagizo yake fanyia kazi endelea na utaratibu mwingine. Unaporudisha mrejesho fahamu kuwa lazima atakosoa ili ajione yuko juu yako. Isikuumize wala usibishane naye. Haikugharimu.

Jenga ukaribu na wenzako

Katika mazingira ambayo kiongozi anapenda kudhalilisha na kuonea wengine, ni rahisi kukata tamaa na kazi.

Usipokuwa makini unaweza kujikuta unakuwa mzembe, mvivu na mtu usiyejali kitakachotokea. Unaanza kuamini huna cha kupoteza.

Katika kukabiliana na hali hii, inashauriwa uwe na watu wakomavu watakaokusaidia kukabiliana na mazingira haya. Kuwa na mtu unayejua anakuelewa. Unaponyanyaswa inakuwa rahisi kumfuata na kumweleza na akakusaidia kurejea kwenye hali yako ya utulivu.

akati mwingine unaweza kudhalilishwa kiasi cha kupoteza hali yako ya kujiamini. Unapokuwa na mtu anayekuelewa, mtu anayekuhakikishia kuwa huna tatizo, hiyo itakurejesha imani yako kwako.

Jikuze kiujuzi

Saa nyingine watu watakudhalilisha kwa sababu wanajua huna uwezo wa kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Usiumie. Ichukulie hiyo kama kichocheo cha kujifunza mambo mapya.

Kama una tatizo la kuandika ripoti vizuri, kajifunze. Tafuta mwenzako anayefahamu mfumo wa uandishi wa ripoti. Jifunze. Kama tatizo ni kuchelewesha kazi za ofisi, jifunze namna nzuri ya kutunza muda ili usiendelee kuchelewa.

Maana yangu hapa ni kwamba usimpe mtu mnyanyasaji upenyo wa kukunyanyasa. Ziba mianya yote ya udhaifu unaoweza kutumika kukuonea. Wahi kazini, fanya kazi kwa bidii, epuka migogoro na watu bila sababu. Unapozingatia sheria na taratibu za kazi unaondoa uwezekano wa mtu mwingine kutumia udhaifu wako wa kutokufuata taratibu ili kukunyanyasa.

Linda faragha yako

Udhalilishaji unaweza kuwa sehemu ya utamaduni wa eneo la kazi. Bosi, kwa tabia zake, anaweza kuwafanya wasaidizi na watu wengine waliochini yake watake kuwa kama yeye.

Ndiyo maana unaweza kushangaa, kama mkurugenzi wa kampuni ana tabia ya kufoka, hata wakuu wa idara nao wanaweza kuwafanyia walio chini yao yayo hayo. Mkuu wa idara akiwa na tabia ya kuchelewesha haki za watu bila sababu, hata wafanyakazi wanaweza kuwafanyia wateja hayo hayo. Maana yake tabia za bosi zimekuwa utamaduni.

Katika mazingira kama haya yenye utamaduni wa uonevu, suluhisho ni kujiwekea mipaka. Fahamu una haki ya kuheshimiwa utu wako kama binadamu mwingine yoyote.

Mtu yeyote, bila kujali nafasi yake kwenye kampuni, hawezi kukutukana, kukufokea na kunyanyasa kwa sababu yoyote ile.

Kukubali kunyanyasika kwa siri au kwa wazi kwa sababu ya kulinda ajira yako kunaweza kukugharimu mbele ya safari. Chora mstari ambao mtu yeyote hawezi kuuvuka.

Tafuta msaada wa kisheria

Nchi yetu inaongezwa kwa misingi ya kisheria. Kila mwajiri analazimika kuheshimu sheria za kazi. Inapotokea kuwa udhalilishaji na uonevu unavuka mipaka ya kuvumilika, usiishie kulalamika. Tafuta msaada wa kisheria.

Kwa upande mwingine, iko haja ya waajiri kuwa makini wanapoteua au kuajiri watendaji wakuu katika taasisi au kampuni zao.

Mbali na kutazama sifa za kitaaluma na uwezo wa kuleta matokeo wanayoyataka, ni muhimu kuchunguza sifa za ziada kama vile uwezo wa kumudu hisia na uwezo wa kuishi na watu.

Sambamba na hilo, ni muhimu kampuni kuwa na sera zinazoeleza bayana hatua za kufuata wafanyakazi wanapokabiliana na mazingira ya udhalilishaji na uonevu.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. Twitter: @bwaya, 0754 870 815

Columnist: mwananchi.co.tz