Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mbinu za kuepuka migogoro na bosi wako kazini

35850 Pic+boss Mbinu za kuepuka migogoro na bosi wako kazini

Fri, 11 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nawafahamu watu wengi wenye uwezo mkubwa kazini, ujuzi na maarifa, lakini walijikuta pabaya kwa sababu tu hawakujua kanuni rahisi za kufanya kazi na wakubwa wao kwenye maeneo ya kazi.

Kuishi vizuri na bosi wako siyo kujipendekeza, bali kuelewa kuwa uhusiano kazini una nafasi kubwa ya kuamua hatma yako.

Kwa mfano, huwezi ukafanikiwa ikiwa hujui namna ya kufanya kazi na mtu mwenye mamlaka juu yako, mtu ambaye kwa nafasi yake ndiye mwenye kauli ya mwisho katika taasisi, idara au ofisi unayofanya kazi.

Nafahamu wapo mabosi ambao kwa hulka zao ni tatizo. Hata ungefanya nini, viongozi hawa watazalisha misuguano na hali ya kutokuelewana miongoni mwa wafanyakazi.

Hata hivyo, hiyo haimaanishi tuache kufanya juhudi za kujifunza namna ya kukaa na viongozi wetu kazini.

Hapa napendekeza mbinu tatu za kufanya kazi na bosi wako.

Heshima

Hakuna binadamu asiyependa heshima. Tena inapotokea binadamu huyo amepewa madaraka juu ya wengine, hitaji la kuheshimiwa linakuwa kubwa zaidi.

Siku zote usisahau kuwa bosi na wewe hamfanani. Bosi anaweza kuwa rika lako; inawezekana mmesoma darasa moja; alikuwa rafiki yako wa karibu; una elimu na uzoefu kuliko yeye na mambo mengine kama hayo; lakini anapokuwa na mamlaka ya kukuongoza, hiyo peke yake ni sababu inayotosha kumpa heshima anayostahili.

Heshima inaanza kwa kuheshimu mipaka ya mahusiano kati yako na bosi.

Fahamu, kwa mfano, wakubwa wengi katika kazi hawapendi kufikika

kirahisi. Wengi wao hulinda ushawishi wao kwa kujenga ukuta unaowatenganisha na wafanyakazi wao.

Hawapendi kuzoeleka. Unapokuwa karibu nao, ni rahisi kutafsiri kama kuwakosea heshima.

Usipende kumzoea zoea bosi wako hata kama anaonekana ni mtu wa kawaida. Pia, heshima kwa bosi ina maana ya utii wa taratibu za kazi zilizozopo. Huwezi kufanya mambo kiholela na bado ukadai unamheshimu bosi wako. Kwa mfano, unapokuwa na dharura, omba ruhusa badala ya kujiondokea tu.

Kuheshimu urasimu wa ofisi kwa kupeleka taarifa zinazohitajika mahali panapohusika hiyo ndiyo heshima kwa bosi wako.

Usishindane na bosi

Wafanyakazi wengi, wakati mwingine bila kujua, hushindana na viongozi wao kazini.

Kutaka kuwa bora au kupata sifa zaidi ya bosi wako hayo yanaitwa mashindano.

Tamaa ya kumzidi mkubwa wako wakati mwingine inaweza kukusukuma kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

Lakini ukichunguza kwa makini bidii

hizo, unagundua ni ulevi wa sifa binafsi.

Katika makosa unayoweza kuyafanya ni kuonekana unashindania heshima na mkubwa wako wa kazi.

Siyo wakubwa wengi wanaweza kuvumilia mashindano ya namna hii. Kushindania heshima na mamlaka kunachochea chuki na uadui usio na sababu. Mwathirika wa mashindano hayo ya ‘nani anaweza kuliko mwenzake’ mara nyingi ni mfanyakazi.

Siku zote mfanye mkubwa wako wa kazi aonekane juu yako. Kubali achukue sifa kwa kazi nzuri uliyofanya.

Kama una mawazo

mazuri, mpelekee hata kama atayaleta hadharani kama vile ni ya kwake.

Unapomuuzia sifa zako, kimsingi unajiongezea ushawishi wako kwake.

Eneo jingine hatari linaloweza kukugombanisha na bosi wako ni makundi.

Makundi kwenye eneo la kazi mara nyingi ni mashindano ya madaraka.

Bahati mbaya, saa nyingine waasisi wa makundi haya ni mabosi wenyewe wanaolinda masilahi yao. Usikubali kuchukua upande kwenye makundi hata kama kufanya hivyo kutakuweka ni karibu na mkubwa. Faida ya muda mfupi leo, inaweza kuwa na gharama za muda mrefu.

Usikosoe, shauri

Wengi wetu tunapenda kukosoa badala ya kushauri. Kukosa kwa maana ya kuonyesha mapungufu ni kazi rahisi kuliko kushauri kwa maana ya kuonyesha nini kifanyike kutatua tatizo.

Jifunze kutulia unapoona

upungufu. Usikurupuke kuelezea tatizo kama huna mawazo ya namna ya kupata ufumbuzi. Hata unapokuwa na majibu ya upungufu unaouona, jiridhishe ikiwa kweli wewe ni mtu sahihi wa kuzungumzia

upungufu huo. Kumbuka siyo kila mtu anaweza kushauri na akasikilizwa.

Lazima uaminike kwanza ndipo unachokisema kichukuliwe kwa uzito.

Pia, kumbuka wenye madaraka hawapendi kukosolewa hadharani.

Kumshambulia bosi wako mbele ya kadamnasi hata kama unachokisema ni sahihi inaweza kuwa mwanzo wa matatizo. Tatizo la kufanya hivi ni kwamba bosi akishakukatalia hadharani hatabadili msimamo baadaye.

Ikiwa umejiridhisha kuwa una mawazo chanya epuka ‘kumsurprise’ kwenye

vikao. Tafuta faragha naye kisha sema mawazo yako. Unapofanya hivi

unamfanya ajisikie kuheshimiwa.

Unapotoa ushauri, tumia lugha chanya yenye kuheshimu haki za wengine.

Jenga ushauri wako kwenye kile unachojua kinakubalika. Tumia lugha yenye utulivu, isiyomshambulia wala kumshinikiza bosi kufanya uamuzi unaofikiri ni sahihi. Tumia hoja na takwimu badala ya mihemko, tetesi na hisia.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Mawasiliano: 0754 870 815, [email protected]



Columnist: mwananchi.co.tz