Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mawaziri wadogo wabwagwa Uchaguzi Mkuu 1965

98983 Pic+mawaziri Mawaziri wadogo wabwagwa Uchaguzi Mkuu 1965

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Septemba 30, 1965 ulifanyika uchaguzi mkuu wa kwanza wa Rais na wabunge chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Ilikuwa ni miezi michache baada ya kufanyika mabadiliko ya Katiba yaliyofuta mfumo wa vyama vingi kabla ya Tanganyika kuungana na Zanzibar.

Kwa hiyo, vyama vingine viliondolewa na kubakia Tanganyika Africa Union (Tanu) kwa upande wa Tanzania Bara na Afro Shiraz (ASP) kwa upande wa Zanzibar.

Katika uchaguzi huo, mawaziri wengi wadogo walishindwa katika majimbo yao. Bunge jipya la Tanzania likawa na wajumbe ambao hivi sasa tunawaita wabunge.

Wapigakura waliojitokeza katika uchaguzi huo waliwachagua wajumbe 107 kati ya viti 199 vya bunge hilo.

Historia inatueleza, katika kipindi hicho, wapigakura waliruhusiwa wale waliokuwa na umri wa kuanzia miaka 21 au zaidi ili waweze kumchagua Rais.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Lakini aliyekuwa na umri wa kuanzia miaka 18, aliruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mwingine wowote lakini si Rais.

Hata hivyo, idadi ya waliojiandikisha na kujitokeza kupiga kura inatofautiana ikitegemea na chanzo cha habari.

Mtandao wa Uchaguzi wa Afrika, umeandika kuwa mwaka 1965, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa watu milioni 3.373 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa watu milioni 2.6.

Lakini kitabu cha “Area Handbook for Tanzania, Volume 550”, toleo la 62 lililotolewa na American University (Washington, D.C.) Januari 31, 1965, kinasema waliojiandikisha katika uchaguzi huo walikuwa milioni 3.36 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa watu milioni 2.266.

Na miongoni mwa watu 803 waliopitishwa katika mashina ya Tanu, ni wanachama 208 tu waliopitishwa kugombea katika majimbo . Majimbo yalikuwa 107. Wagombea katika majimbo sita kati ya hayo, walipita bila kupingwa. Katika kila jimbo kulikuwa na wagombea wawili waliosimamishwa na Tanu.

Manaibu waziri waanguka

Katika uchaguzi huo, Rashid Kawawa, aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais, na mawaziri wanne-- Oscar Kambona, Job Lusinde, Michael Kamaliza na Austin Shaba, pamoja na Francis Vincent Mponji, aliyekuwa waziri mdogo wa kazi, walipita bila kupingwa.

Kwa hiyo yalibaki majimbo 101 ambayo wagombea walitakiwa kupigiwa kura.

Lakini kuna mawaziri wadogo, ambao sasa wanaitwa manaibu, walishindwa katika uchaguzi huo.

Mmoja wao ni Bibi Titi Mohamed, ambaye alikuwa waziri mdogo katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni wa Taifa, alishindwa kukitetea kiti chake cha Rufiji.

Alipata kura 7,343 wakati mpinzani wake, Athumani Mohamed alipata kura 18,145 ikiwa ni ushindi wa kura 10,802.

Mwingine ni Elias Kisenge, ambaye alikuwa ameweka rekodi ya kuwa waziri kijana kuliko wote Tanzania, alipata kura 11,607. Alishindwa kwa tofauti ya zaidi ya kura 8,000 na mpinzani wake, Chediel Mgonja ambaye alipata kura 19,598.

Kisenge alikuwa waziri mdogo katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na pia aliwahi kuhudumu kama waziri mdogo wa tawala za mikoa.

Pia Martin Hauli wa Kondoa Kusini alipoteza kiti chake. Alishindwa kwa tofauti ya zaidi ya kura 21,000 na Konde Jangaa ambaye alipata kura 24,651.

Nicus Buhatwa alikuwa waziri mwingine mdogo aliyepoteza jimbo lake la Ukerewe. Aliambulia kura 5,512 wakati mpinzani wake, George Imerezi alikusanya kura 15,497.

Mwingine aliyepoteza jimbo ni aliyekuwa Waziri Mdogo wa Kilimo, Misitu na Wanyama Pori, Edward Barongo aliyepata kura 11,005 dhidi ya 11,679 za Jeremiah Bakampenja katika Jimbo la Ihangiro, Bukoba.

Waziri Mdogo wa Elimu, Frank Mfundo, aliyekuwa mbunge wa Handeni, alishindwa na Njama Mbega Issa Mnondwa kwa zaidi ya kura 12,000. Mnondwa alipata kura 16,418. Kuanguka kwa Mfundo kulitimiza idadi ya mawaziri wadogo sita walioanguka katika uchaguzi huo.

Hao wakijumlishwa na idadi ya mawaziri wadogo walioshindwa kuvuka mchujo wa ngazi za awali za wilaya katika kuwania kugombea, wanatimiza idadi ya mawaziri wadogo tisa ambao hawakurudi bungeni kutokana na kushindwa katika uchaguzi huo.

Mbali na hao, Timothy Samjela, aliyekuwa katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Tanu Jimbo la Bagamoyo, naye alishindwa katika uchaguzi huo.

Lakini wapo mawaziri walioibuka na ushindi katika uchaguzi huo katika majimbo yao ambao ni pamoja na Erasto Mang’enya.

Alishinda kiti cha Muheza kwa kumshinda George Cheuta kwa zaidi ya kura 13,743.

Waziri mwingine aliyetetea kiti chake ni Habib Amir Jamal katika Jimbo la Morogoro Kaskazini baada ya kupata kura 5,807 dhidi ya Mgala Ali Juma, aliyepata kura 4,466.

Miongoni mwa watu wenye asili ya Asia walioshinda katika uchaguzi huo ni Mahmud Rattansey aliyekuwa Jimbo la Tabora Kati. Awali Rattansey alikuwa rais wa iliyokuwa Jumuiya ya Waasia Tanganyika.

Tangu uchaguzi wa kwanza wa Baraza la Kutunga Sheria uliofanyika Agosti 1958, wagombea wa Kiasia walioungwa mkono na Tanu ambao ni Sophia Mustafa, Mahamoud Rattansey na rafiki mkubwa wa Mwalimu Nyerere, Amir Jamal, walikuwa wakishinda kwa kishindo.

Miongoni mwa mawaziri wadogo waliotangazwa kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo ni Waziri Mdogo wa Biashara na Ushirika, Ali Saidi Mtaki.

Lakini inaelezwa kuwa katika mchakato huo, Rais Nyerere alitumia mamlaka yake ya kikatiba kumteua Paul Bomani ambaye awali alikuwa Waziri wa Fedha.

Alishindwa katika uchaguzi huo lakini alipoingia bungeni kwa kuteuliwa na Rais Nyerere, akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo.

Rais Nyerere pia alimteua Lady Chesham, ambaye awali alikuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Pia, aliteuliwa katika uchaguzi wa mwaka 1960.

Wengine walioteuliwa ni Chifu Abdallah Fundikira, Joseph Namata aliyekuwa katibu mkuu wa Ofisi ya Rais, Mark Bomani na Ali Migeyo, Wakili Mkuu wa Serikali na mmoja wa waasisi wa Tanu.

Pia aliwateua Wazanzibari wanne ambao ni Bibi Jokha Suleimani, Sheikh Umbaya Vuai, Ahmed Selemani Ali Riami na Himid Mbaye.

Katika uchaguzi huo 1965, Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa mgombea pekee wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa kitabu ha “Tanzania: Party Transformation and Economic Development”, Henry Bienen anaandika Halmashauri Kuu za TANU na ASP zilikubaliana kuwa mgombea wa kiti cha urais awe mmoja na apigiwe kura ya “Ndiyo” au “Hapana”na kwamba, iwapo mgombea huyo angekosa kura nyingi za kumwezesha kuwa Rais, kazi ya Tanu na ASP ilikuwa ni kukaa chini na kupendekeza jina jingine.

Columnist: mwananchi.co.tz