Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Matokeo uchaguzi mdogo yana athari kubwa kwa wapinzani 2020

12524 Uchaguzi+pic TanzaniaWeb

Sat, 18 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa aliwaambia wapigakura: “Mjitokeze mkapige kura kwa wingi, kuhusu Tume itamtangaza nani mshindi, hilo niachieni mimi.”

Lowassa alisema tena: “Hakikisheni mnapiga kura nyingi ili hata CCM wakiiba, zibaki nyingi za kunifanya nitangazwe kuwa Rais.” Hii nukuu ya pili ni nzuri lakini ile ya kwanza ni kiboko. Ilikiwa kauli yenye tafsiri kubwa ya kujiamini na kujenga uhakika. Ni kauli ya kibabe mno.

Je, nini kilitokea? Watanzania wengi mno walijitokeza kupiga kura. Katika watu milioni 23 walioandikishwa kupiga kura, zaidi ya milioni 15.6, sawa na asilimia 67, walipiga kura. Rais John Magufuli alipata kura milioni 8.9, asilimia 58, Lowasa milioni 6.1, asilimia 40.

Ukirejea nyuma, Uchaguzi Mkuu 2010, idadi ya waliojiandikisha ilikuwa milioni 20. Waliopiga kura ni milioni 8.6, sawa na asilimia 42.8. Jakaya Kikwete wa CCM kura milioni 5.3, asilimia 62.8 na Dk Willibrod Slaa Chadema, kura milioni 2.3, asilimia 27. Hiyo ni kwa kutojumuisha matokeo ya wagombea wengine.

Nimeweka matokeo ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2010 na 2015 ili kujisogeza kwenye hoja mahsusi. Ni miaka ambayo uchaguzi wake ulionekana ubabe na nguvu kubwa ya upinzani kuliko uchaguzi wa mwaka 2005 na 2000. Mazingira ya 2015, unaweza kuyafananisha na yale ya mwaka 1995.

Tubaki kwanza kwenye uchaguzi wa 2010 na 2015. Kwa nini pamoja na uchaguzi wa miaka hiyo yote kubeba nguvu kubwa ya upinzani na mchuano mkubwa, lakini 2010 idadi ya wapigakura ilikuwa ndogo kulinganisha na mwaka 2015? Jawabu lipo kwa Lowassa: “Pigeni kura, Tume itamtangaza nani, hilo niachieni mimi.”

Lowassa hakuwa imara kwenye kampeni. Hakumudu kuhutubia kwa muda mrefu. Hakutoa hamasa yenye nguvu alipokuwa jukwaani. Hata hivyo, aliwajengea watu imani kwamba alikuwa na uwezo wa kutangazwa mshindi kama angepata kura za kutosha. Hii ndiyo hamasa iliyokosekana kwa Dk Slaa mwaka 2010.

Dk Slaa alikuwa na hamasa kubwa jukwaani. Aliweza kuhutubia muda mrefu. Hotuba zake zilijenga hisia na mitaani wafuasi wake walitembea wakijiamini. Slaa hakuwaangusha watu waliojitokeza kwenye mikutano yake. Pamoja na hivyo, idadi ya waliopiga kura ilikuwa ndogo.

Sababu ya wakati wa Dk Slaa kura kutokuwa nyingi ni kukosekana kwa imani. Slaa hakuwa na matamshi ya uhakika kuwa alikuwa na uwezo wa kutangazwa mshindi na kukabidhiwa dola, licha ya kwamba kampeni zake zilikuwa na hamasa kubwa. Lowassa alivunja moyo wengi kwenye kampeni, ila alijenga kuaminika.

Uchaguzi Mkuu mwaka 1995, idadi ya waliopiga kura ilikuwa asilimia 77 ya waliojiandikisha. Sababu ni kwamba mgombea wa NCCR-Mageuzi wakati huo, Augustino Mrema alikuwa mtu mzito na alijenga imani kwamba angeweza kushinda na kukabidhiwa dola. Hotuba za Mrema zilikuwa za mtu mwenye kujiamini, ungefikiria vipi kuwa angeweza kuibiwa kura?

Sura inayopatikana

Tunaweza kuipata sura halisi kwa kufanya mapitio ya kauli za viongozi wa vyama vya upinzani katika matokeo ya uchaguzi mdogo unaofanyika mfululizo. Viongozi hawawajengei moyo wapigakura kwamba wakipiga kura zitalindwa na wakipata ushindi watatangazwa. Wanahubiri unyonge na kuibiwa.

Uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika jimbo la Buyungu, Kigoma, Jumapili iliyopita (Agosti 12), mapema kabisa Chadema ilianza kutangaza matokeo kuwa mgombea wake, Elias Michael alikuwa akiongoza kwa kura nyingi kiasi kwamba hakukuwa na uwezekano wowote kwa mgombea wa CCM, Christopher Chiza kutangazwa mshindi.

Saa 1:58 usiku (Agosti 12), Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji aliandika kupitia akaunti yake ya Twitter: “CCM wakitangazwa washindi kwenye uchaguzi wa Buyungu basi utakuwa muujiza ambao hata Mwenyezi Mungu hawezi kuufanya.”

Mashinji akaongeza: “Hongera sana Mh. Elias Michael kwa ushawishi wako mkubwa kwa wananchi wa Buyungu na Tanzania nzima! Tulianza na Mungu, tunamaliza na Mungu!”

Chama cha ACT-Wazalendo kilitangaza kuungana na Chadema katika uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12. Saa 12:7 jioni (Agosti 12), Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Nataka nione CCM itaibaje Buyungu. Maana kipigo wanachopata wakimtangaza mgombea wa CCM hata mawe yatatoa machozi.” Zitto aliendelea kuandika Twitter na Facebook kuhusu matumaini ya Chadema kushinda uchaguzi Buyungu. Saa 3 usiku (Agosti 12), Zitto aliandika: “Chadema amkeni: CCM wanakwenda kupindua matokeo ya Elia Kata ya Kasanda. Wanatumia Polisi na Watu wa Usalama muda huu. CCM wameshindwa kata zote nne Kakonko na jimbo zima. CCM wanatangaza matokeo ya uongo. Chadema wekeni wazi matokeo, msikae nayo. Mmeshinda jimbo hili.”

Mwisho wa yote, Chiza wa CCM alitangazwa mshindi. Kulikuwa pia na matokeo yaliyowekwa wazi mapema, kata ya Turwa, Tarime, yaliyoonesha kwamba Chadema walishinda. Matokeo ya mwisho yakawa mgombea wa CCM kutangazwa mshindi. Haya si mema hata kidogo kwa wapinzani.

Jinsi matokeo yalivyokuwa yakitolewa awali, Chadema waliwaaminisha wanachama, wafuasi wao na Watanzania kwa jumla kwamba tayari walikuwa wameshapata ushindi mkubwa na hakukuwa na uwezekano wowote wa CCM kubadili matokeo. Nini kilitokea? Anayecheka mwisho ndiye mchekaji kamili.

Sasa basi, baada ya wagombea wa CCM kutangazwa washindi katika matokeo ya mwisho, maana yake ujumbe unaoweza kupokelewa na watu wengi walioamini taarifa za awali zilizokuwa zikitolewa na Chadema ni kuwa matokeo yalipinduliwa. Kwa mantiki hiyo, Chadema walishindwa kulinda ushindi waliojinasibu kuupata.

Ongezea kuwa wabunge na madiwani wengi wa upinzani wanajiuzulu na kila uchaguzi mdogo unapofanyika, CCM wanashinda. Kwa kasi kubwa uchaguzi mdogo unawafanya wapinzani waonekane wasio na chao. Wapinzani wanatakiwa kuliona hili mapema na walifanyie kazi yenye uzani wa kukabiliana na tetemeko la sasa.

Kinachoonekana kwa sasa ni kama wapinzani hawashtuki na hali hiyo. Mfano ni sasa hivi, wataendelea kulalamika kuwa walidhulumiwa ushindi wao wa ubunge Buyungu na udiwani Turwa. Watazungumza kwa kutaka huruma ya wananchi na jumuiya ya kimataifa, kwamba uchaguzi Tanzania si huru na haki. Hata hivyo, wanajitengenezea hasara kubwa zaidi.

Hasara kuelekea 2020

Kuijua hasara ya upinzani itokanayo na matokeo ya uchaguzi mdogo kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, vema tukumbuke tena hamasa ya Lowassa, kwamba watu wapige kura kwa wingi, kuhusu nani atatangazwa na NEC kuwa mshindi, hilo alitaka aachiwe yeye.

Ushawishi ni sanaa. Ujenzi wa imani ni kielelezo muhimu cha ushawishi, maana watu huvutiwa na wale wenye kujiamini. Mpigakura hawezi kushawishika kumpigia kura mgombea ambaye hana uhakika kama anaweza kushinda au kama hata akishinda hatatangazwa.

Matokeo ya uchaguzi mdogo unaofanyika mfululizo, jinsi wapinzani wanavyoambulia patupu, na namna ambavyo wanajinadi kuwa wanaibiwa kura, wanawapa hofu wapigakura kwamba kumbe kupanga foleni kuelekea vyumba vya kupigia kura si kitu kinachoweza kuleta mabadiliko.

Hali iliyopo sasa hivi ya wapinzani kutangaza wanashinda kisha baadaye wanaotangazwa kushinda matokeo rasmi wanakuwa CCM, inafanya vyama vya upinzani nchini kuonekana vimejaa unyonge na visivyoweza kuutetea ushindi wao. Athari ya juu kabisa ni kuwakatisha tamaa wapigakura.

Hivyo basi, kadiri matokeo ya uchaguzi mdogo yanavyoendelea kutoa sura yenye kuvinyima ahueni vyama vya upinzani, jumlisha malalamiko ya wapinzani kuhusu kuibiwa kura na kudhulumiwa ushindi, ndivyo inavyowafanya wapigakura wakose mwamko wa kuuendea Uchaguzi Mkuu 2020.

Ni wazi sasa kwamba vyama vya upinzani vinatakiwa kufanya mabadiliko ya namna ya kuuendea uchaguzi mdogo. Wauoneshe umma namna ambavyo wanaweza kuchaguliwa na kushinda. Wawaaminishe Watanzania kuwa wakishinda watatangazwa. Vinginevyo mwaka 2020 hawatapata mwitikio mzuri.

Wafahamu kuwa endapo wapigakura hawatakuwa wengi mwaka 2020, waathirika wakuu ni wao, na CCM watanufaika kwa matokeo hayo. Waache kulalamika na kunung’unika, badala yake wawajengee imani Watanzania kama Lowassa mwaka 2015. Waache kujenga hofu na unyonge. Wathibitishe wanazo stahili za kuchaguliwa na wanatosha kushinda.

 

Columnist: mwananchi.co.tz