Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Matokeo mabaya ni ya shule au mwanafunzi?

15566 Joseph+Chikaka TanzaniaWeb

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lengo la kila mwanafunzi ni kufanya vizuri katika taaluma yake kwa ngazi yoyote atakayokuwa.

Hilo huenda sambamba na kupata maarifa na ujuzi ambao utamsaidia katika kuboresha maisha yake, ya wengine na taifa kwa jumla.

Kwa muda mrefu kumekuwapo mijadala hasa pale matokeo ya mtihani wa taifa yanapotoka. Watu huzigawa shule kutokana na kiwango cha ufaulu, hivyo kuziona shuleni fulani kuwa ni shule bora kwa kupitia kigezo cha ubora wa matokeo.

Kwa hoja hii maswali ya kujiuliza ni je, matokeo hayo ni ya shule au ni ya mwanafunzi? Na, ni nani anastahili pongezi kati ya shule, mwanafunzi na wadau wa elimu kama vile wazazi, walezi, viongozi wa elimu katika ngazi mbalimbali?

Matokeo mabaya ni ya mwanafunzi

Lipo kundi ambalo huamini kuwa matokeo yoyote ya kitaaluma yawe mazuri au mabaya mwenye kubeba jukumu hilo la pongezi au lawama ni mwanafunzi.

Kundi hili huweka masuala mengine yote yanayomzunguka huyo mwanafunzi kuwa siyo kigezo cha kumfanya ashindwe kufikia malengo yake ya kitaaluma. Huchukulia kuwa ni changamoto za muda tu ambazo mwanafunzi yeyote hapaswi kuzishindwa.

Kundi lenye mtazamo huo humchukulia mwanafunzi kuwa kitovu cha hamasa ya ujifunzaji na ufundishaji. Na kwamba mwanafunzi ana nafasi kubwa ya kuwa chachu ya mafanikio yake binafsi ya kitaaluma.

Kwa mfano, tumtazame mwanafunzi wa shule A ambaye alipata daraja la nne katika mtihani wake wa taifa wa kidato cha nne. Pia, tumtazame na mwanafunzi mwingine kutoka shule B ambaye aliyepata daraja la kwanza katika mtihani huo.

Kwa mfano huo hapo juu, tutagundua kuwa shule A haikuweza kumfanya mwanafunzi wake yule mmoja apate daraja la kwanza, la pili au la tatu. Vilevile, tutabaini kwamba shule B, nayo haikuweza kuwa kikwazo kwa mwanafunzi wake yule aliyepata daraja la kwanza.

Kwa hali hiyo, wanafunzi na wazazi wanapaswa kufahamu kuwa kumpeleka mwanafunzi katika shule ya A au shule B hakumhakikishii huyu mwanafunzi matokeo mazuri au mabaya.

Matokeo ya aina zote hizo yana uhusiano na shule lakini zaidi yana uhusiano na mwanafunzi husika.

Aidha, ni wajibu wa mwanafunzi kutafuta mbinu halali zinazoweza kumfanya azingatie masomo yake vizuri.

Hii ikiwa ni pamoja na kujifunza kupitia mazingira na vitabu mbalimbali, kusikiliza mawaidha ya watu wazima na waliomtangulia kuona mambo. Ni dhahiri mwanafunzi huyo atabaini siri za mafanikio ya kitaaluma zilizojificha.

Hivyo, kuwa katika shule fulani siyo kigezo kikubwa cha matokeo mazuri. Wanachopaswa kufanya wanafunzi ni kutumia fursa za kimazingira, kiutendaji na yote yanayoweza kumfanya afanye vizuri katika masomo yake ikiwamo nidhamu.

Pia, nafasi ya shule katika matokeo ya kitaaluma kiwilaya, kimkoa au kitaifa siyo kinga kwa mwanafunzi mmoja mmoja katika darasa na katika shule hiyo husika. Hii ni kwa sababu, hakuna kigezo cha mteremko; kwamba, shule C imekuwa nafasi ya juu kitaifa labda ya 10, hivyo haiwezi kumsaidia mwanafunzi wa shule hiyohiyo aliyepata daraja la nne au sifuri.

Hilo ni sawa pia na kigezo kwamba shule C ilipitwa na shule D katika matokeo. Lakini hilo pia, siyo kigezo kwa wanafunzi watano wa shule C ambao walifaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza.

Haijalishi shule aliyosoma mwanafunzi husika itashika nafasi ya ngapi katika matokeo ya mitihani ya taifa kiwilaya, kimkoa ama kitaifa.

Hayo yatakuwa ni matokeo ya shule kwa ujumla yanayochangiwa na wahitimu wote wa darasa la mtihani husika. Kinachojalisha hapo ni kwa kiwango kipi mwanafunzi binafsi amefaulu.

Kama tujuavyo kuwa nafasi ya shule kitaifa au kimkoa huwa haimpeleki mwanafunzi kidato cha tano au ngazi ya chuo kikuu.

Matokeo binafsi ya kitaaluma ndiyo humpatia fursa hiyo ya kuendelea na masomo ya ngazi ya juu. Katika hilo huwa hakuna mbadala wa kutofanya kazi ama kusoma kwa bidii.

Hivyo basi matokeo mabaya kwa mwanafunzi yawe chachu ya kumfanya ajitume zaidi. Wapo walio katika shule zenye kila kitu, lakini bado walishindwa na wale walio katika mazingira magumu.

Matokeo ni ya shule

Hakuna shule yenye kupenda matokeo ya kitaaluma ya wanafunzi wake yawe mabaya. Hakuna. Shule zote zingependa wanafunzi wake wote hata wale wenye matatizo ya ujifunzaji wapate matokeo na mafanikio mazuri.

Matokeo mabaya ya mitihani huijengea taswira mbaya shule kwa jamii. Hali hiyo inapoendelea hasa katika shule binafsi, watu husitisha kupeleka watoto na vijana wao huko.

Hivyo, shule hizo zinaweza kupoteza wanafunzi na kushindwa kujiendesha na hatimaye hutoweka katika ulimwengu wa shule.

Hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba shule zinahitaji matokeo mazuri. Kwa mtazamo huo, aina yoyote ya matokeo yawe mazuri au mabaya, shule haiwezi kukwepa kuwa sehemu ya mafanikio au kushindwa.

Ni wajibu sasa wa jamii kuchukua hatua za makusudi za kufahamu mazingira sahihi kwa watoto na vijana. Pia, kuwa na uhakika wa taaluma bora na nidhamu badala ya kutafuta shule yenye ufaulu mkubwa. Hii ni kwa sababu kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, kunaweza kusimsaidie mwanafunzi asiye na maadili bora.

Taaluma lazima iendane na nidhamu nzuri. Kila mmoja anayo fursa ya kujihoji, ili kuona kama matokeo yake mazuri au mabaya ni ya shule au ni ya kwake binafsi.

Columnist: mwananchi.co.tz