Dar es Salaam. Wiki iliyopita ilitawaliwa na habari ya mshangao kuhusu kuibiwa kwa kompyuta katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Jambo hilo siyo tu kwamba ni tukio lisilo la kawaida bali linatafsiriwa kama njama fulani imefanyika.
Ofisi ya DPP ni ofisi nyeti ambayo bila shaka ina ulinzi wa kutosha na wengi wasingetarajia kusikia taarifa za kuibiwa kwa kompyuta katika ofisi hiyo inayoshughulikia kesi mbalimbali nchini kwa niaba ya serikali.
Watu mbalimbali waliotoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hilo wameonyesha wasiwasi juu ya kutokea kwa wizi huo wakati ambao ofisi hiyo ikiendelea na jukumu la majadiliano na watuhumiwa wenye kesi za uhujumu uchumi (plea bargaining).
Hata hivyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga alifafanua jambo hilo na kusema ni kweli kuna vipande vya kompyuta vimeibiwa, lakini siyo kwenye ofisi ya DPP bali kwenye ofisi ya mashitaka ya mkoa wa Dar es Salaam.
Taarifa ya Dk Mahiga haiondoi ukweli kwamba ofisi ya mashitaka ya mkoa wa Dar es Salaam nayo inahifadhi nyaraka za kesi mbalimbali ambazo zinasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako pia kuna kesi za uhujumu uchumi.
Bado kuna maswali mengi kuhusiana na wizi huo, haiwezekani mwizi wa kawaida akaenda sehemu kuiba vipande cha kompyuta na kuacha vitu vingine. Waliohusika kwenye wizi huo wanajua wanachokifanya na wasipokamatwa wanaweza kufanikisha azma yao.
Pia Soma
- KAKAKUONA: Tunasubiri Rais afoke ndiyo mambo yaende?
- MAKALA YA MALOTO: Kuhamia Dodoma kumbukumbu halisi kumuenzi Mwalimu Nyerere
- Maendeleo na uwajibikaji, ushirikishaji na uwezeshaji
Kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa picha za mtu mmoja ambaye inadaiwa kwamba alikuwa akiibia serikali Sh7 milioni kwa kila dakika. Picha hizo zimemuonyesha mtuhumiwa huyo akikabidhi mabunda ya fedha taslimu kwa watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa serikali.
Jambo hilo pia linaibua maswali mengi katikati ya mjadala wa kuibiwa kwa kompyuta katika ofisi ya DPP. Moja ya maswali hayo ni kwa nini fedha hizo zilirudishwa na mtuhumiwa zikiwa taslimu wakati serikali ina mifumo yake ya malipo ya kibenki au kielektroniki.
Ingekuwa ni jambo la busara na lisiloibua maswali tata endapo mtuhumiwa ambaye ameridhia kurudisha fedha za serikali kupewa akaunti ya serikali na kwenda kulipa benki, kisha arudishe uthibitisho kwamba amelipa fedha hizo.
Kesi mbalimbali bado zinaendelea na kama ofisi ya mashitaka ya Dar es Salaam itakuwa imepoteza nyaraka muhimu za kesi hizo kutokana na wizi huo basi kuna hatari baadhi ya kesi zikacheleweshwa.
Tukio hilo ni kashfa kubwa kwa ofisi ya DPP na serikali kwa ujumla. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanyika mara moja na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watu waliohusika. Hiyo itajenga nidhamu ya uwajibikaji katika masuala muhimu.
Hata kama hakuna nyaraka zilizoibwa bado tukio lenyewe linaitia doa serikali kwa sababu inafahamika wazi kwamba serikali ina vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo, siyo rahisi ofisi zake zinaingiliwa na wezi kutoka nje.
Uchunguzi huo uanzie kwa wafanyakazi katika ofisi hiyo ya mashitaka ambao wanaweza kuwa wamehusika kwa namna moja au nyingine. Pia, uchunguzi ufanyike kwa watu wa nje ambao wanaweza kuwa wametumia udhaifu wa kukosekana kwa ulinzi katika ofisi hiyo na kuiba vifaa muhimu vya kompyuta.
Jambo hili siyo dogo kama linavyochukuliwa kwa sababu linahusisha ofisi ya umma ambayo inashughulika na kesi za watu. Ni muhimu taarifa za mara kwa mara zikatolewa kwa umma ili kujua uchunguzi huo umefikia wapi.
Uwazi ndiyo nyenzo ambayo inaweza kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya wananchi na ofisi ya mashitaka. Hivyo, ni muhimu kuendesha uchunguzi huo kwa uwazi ili kuwajengea imani wananchi.
Pia, ofisi ya DPP inapaswa kuimarisha ulinzi wake ili kuweka mazingira ya usalama. Ni matarajio ya walio wengi kwamba mfumo wa ulinzi katika ofisi hiyo nyeti utaimarishwa kwa ajili ya uhakika wa nyaraka za umma.