Mazingira ya utendaji wa kazi katika siku za leo yamebadilika. Kuacha kazi kumekuwa sehemu muhimu ya ukuaji kazini.
Si ajabu, kwa mfano, kuona mtu mwenye ajira nzuri, anayelipwa vizuri, mwenye nafasi nzuri ofisini kwake akiendelea kuomba kazi sehemu nyinginezo.
Pia kuna ugumu wa mazingira ya kazi. Kutokutabirika kwa usalama wa kazi kunakotokana na migogoro, kutokuelewana, takwa la mkataba wa ajira na wakati mwingine aina ya ajira inaweza kuwa sababu inayowalazimisha watu kuacha kazi sehemu moja na kujaribu kwingine.
Je, uchukue hatua gani unapofikiria kuacha kazi kwa sababu yoyote? Hapa matano ya kujiuliza.
Kuacha kazi kunakukuza?
Fikiria namna gani kuacha kazi kutakusaidia kukua kiujuzi na kiuzoefu. Je, huko unakokwenda utapata mazingira yanayokuwezesha kujifunza mambo mapya zaidi? Je, huko unakokwenda utakuwa salama zaidi ya hapo ulipo?
Pia Soma
- Jifunze kugundua tabia za wafanyakazi
- Vijue vigezo vya kutafuta ajira ya ndoto zako
- Mbinu za kurudisha ari ya kazi iliyopotea
Wakati mwingine inawezekana umeonewa, umebaguliwa, umedhalilishwa, au kufanya kazi kwenye mazingira magumu. Usipokuwa makini unaweza kufanya uamuzi wa kulipiza kisasi lakini ukayajutia baadaye.
Saa nyingine huenda umevutiwa na mwajiri mwingine anayeahidi kukuongezea mshahara zaidi. Lakini hujafikiria kuwa mwajiri wa sasa anayekulipa kidogo, anakupa uhuru wa kufanya mambo mengine yanayoweza kukuongezea kipato. Huko unakokwenda unaweza usipate muda wa kufanya mambo hayo.
Umesikiliza ushauri unaoaminika?
Kabla hujatekeleza azma yako ya kuacha kazi, jiulize umefanya mawasiliano na watu wazoefu wanaoaminika? Ingawa ni kweli watu wanaweza kutofautiana na wewe na huenda wasielewe vyema mazingira yako, lakini bado watu hawa wanaweza kukusaidia kuyatazama mambo kwa mtazamo mpana.
Mawazo yao yanaweza kukufanya ugundue kuwa kumbe huna sababu ya kuacha kazi uliyonayo isipokuwa kuangalia namna ya kutatua changamoto ulizonazo hapo hapo ulipo.
Pia inawezekana unaacha kazi kwa kulazimishwa na mazingira ya kazi hali inayoweza kuambatana na maumivu makubwa. Hisia za kuonewa na taasisi au kampuni inayomlazimisha kuacha kazi; hofu ya aina ya maisha atakayoishi baada ya kuacha kazi; wasiwasi wa kukosa hadhi aliyokuwa nayo kama mfanyakazi ni baadhi ya sababu zinazoweza kumfanya mtu aache kazi kwa moyo mzito. Je, umeonana na watalaam wa unasihi wakusaidie kuchukuliana na taarifa hizi?
Unamuenzi mwajiri unayemwacha
Huenda unaondoka eneo unaloamini ulinyanyasika, ulionewa na kudhalilika na ukafika mahali ukajiona una haki ya kumkejeli mwajiri unayemwacha. Furaha ya kupata kazi mpya bora zaidi inaweza kukufanya ukapungukiwa na hekima.
Jiulize, hivi kweli mwajiri wako wa sasa hana mchango wowote kwako? Hakuna namna mwajiri huyo unayemdhihaki amekulea na kukufikisha hapo ulipo?
Katika wasifu wako wa kazi ulimtaja mwajiri huyu usiyempenda leo. Uzoefu na ujuzi aliouvutiwa nao mwajiri mpya umeupata kwa kufanya kazi na mwajiri huyu unayeachana naye. Hilo angalau likusaidie kuwa mtulivu kwa maneno na vitendo.
Mkataba wa ajira unasemaje?
Kupata kazi bora zaidi ya hiyo uliyokuwa hakupaswi kukupa kiburi cha kuacha kazi bila kufuata taratibu. Kufukuzwa kazi, kwa upande mwingine, kunaweza kukuchanganya kiasi cha kukufanya uamue kuacha kazi kinyume na mkataba wa kazi. Usifanye hivyo. Rejea mkataba wako na mwajiri. Jiulize, mkataba wako unasemaje katika mazingira ya kuacha kazi?
Mikataba mingi inamtaka mwajiriwa kutoa notisi ya kuacha kazi kwa muda wa kuanzia mwezi mmoja hadi miezi mitatu kabla ya tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri wako. Kimsingi, notisi ya kuacha kazi inalenga kumpa mwajiri muda wa kumtafuta mtu atakayechukua nafasi yako. Inakusaidia na wewe kukabidhi majukumu yako pamoja na vitendea kazi ulivyokabidhiwa.
Kadhalika, inawezekana mwajiri wako wa sasa alikudhamini kupata mkopo katika taasisi za fedha. Pengine mlikuwa ya makubaliano ya muda maalum wa kufanya kazi kufidia gharama za masomo yako. Mtu mzima anayejitambua huheshimu makubaliano anayoyafanya na watu wengine.
Umetoa taarifa rasmi kwa mwajiri?
Umejiridhisha kuwa sasa unaacha kazi. Je, unaanza kuzungumza holela kwenye vikao vya chai kuwa unaondoka bila kumjulisha bosi wako? Epuka kueneza taarifa hizo kabla hujawasiliana rasmi na mwajiri.
Andika barua ya kuacha kazi inayoainisha nia yako kuwa unaacha kazi na kutaja bayana tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri wako.
Kisha shukuru kwa kutaja kwa ufupi fursa ulizopata tangu umeanza kazi unazoamini zilizokujenga kiweledi na kiuzoefu.
Malizia barua yako kwa kuomba kujulishwa taratibu zozote za makabidhiano ya ofisi. Unaweza pia kuonyesha uko tayari kwa usaili wa kuacha kazi.
Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia na Unasihi, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya , 0754 870 815
DONDOO ZA AJIRA
Utaratibu wa Kufuata Unapoachishwa Kazi
Sheria ya ajira na mahusiano kazini Namba 6 ya mwaka 2004 inaainisha mazingira kadhaa yanayoweza kusababisha mwajiriwa aachishwe kazi na mwajiri. Mazingira haya ni kama vile mwajiri kuwa na sababu halali za kuchukua hatua za kusitisha mkataba kwa kufuata utaratibu; mwenendo mbaya na utovu wa nidhamu kazini pamoja na vitendo vinavyoonesha ukosefu wa maadili.
Unapopewa taarifa rasmi kuwa umeachishwa kazi, hatua ya kwanza ya kuchukua ni kujiridhisha kuwa ni kweli utaratibu halali wa kisheria umefuatwa katika kukuachisha kazi. Hapa kuna mambo mawili. Kwanza, mwajiri analazimika kuthibitisha kuwa kuna kosa limefanyika na lina uzito wa kutosha kuhalalisha kuachisha kazi.
Jambo la msingi ni kwamba hata kama umefanya kosa, mwajiri analazimika, kwa mujibu wa sheria, kufanya juhudi za kurekebisha nidhamu yako kwa unasihi (ushauri) na maonyo. Kuonywa kunalenga kukusaidia kuelewa kuwa unapofanya kosa kama hilo unaweza kuchukuliwa hatua zaidi za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Sheria hii, mfanyakazi anapofanya kosa na mwajiri akaona kuna haja ya shauri kufanyika, basi mwajiri analazimika kumpatia hati ya mashtaka mfanyakazi husika iliyoandikwa katika lugha ambayo mfanyakazi ataielewa. Kisha mfanyakazi atapewa muda wa kutosha (si chini ya masaa 24) kuandaa utetezi. Katika kutekeleza haki hii ya kusikilizwa, mfanyakazi anaweza kujitetea kwa msaada wa vyama vya wafanyakazi au mfanyakazi mwenzake.
Katika mazingira ya kuachishwa kutokana na utendaji mbovu, utaratibu kama huo utachuliwa isipokuwa hapa mwajiri atahitajika kumwezesha mfanyakazi kujifunza kazi kabla ya kuchukua hatua zozote. Kadhalika, pale ambapo mfanyakazi ameachishwa kazi kutoka na ugonjwa au ameonekana hawezi tena kudumu kazi zake shauri ya ugonjwa, mwajiri atahitaji kuongozwa na maoni ya daktari.