Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Marufuku ya Makonda Marekani kuna siri hatujaambiwa

94150 Makonda+pic Marufuku ya Makonda Marekani kuna siri hatujaambiwa

Mon, 3 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya tangazo la Marekani kuwa Tanzania ingeunganishwa na mataifa mengine sita kuwekewa vikwazo vya usafiri juzi Januari 31, tamko rasmi limetolewa.

Rungu lililoikumba Tanzania ni pamoja na raia wake kunyimwa fursa ya kushiriki bahati nasibu ya kupata vibali vya kuishi Marekani. Vibali hivyo hutolewa kupitia mpango unaoitwa Diversity Immigrants Visa au kwa umaarufu kama Green Card Lottery.

Kupitia mpango huo, Wizara ya Mambo ya Nje Marekani huchagua watu 55,000 kutoka kwenye nchi zenye rekodi ndogo ya kuhamia Marekani ndani ya miaka mitano.

Kwa mfano, takwimu za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa watu milioni 23 hushiriki bahati nasibu hiyo kila mwaka ili kuwania nafasi 55,000.

Kwa uamuzi wa sasa wa Marekani, Watanzania wamenyimwa haki ya kushiriki bahati nasibu hiyo. Hata hivyo, hawazuiwi kutembelea nchi hiyo au kuomba vibali kupitia mpango mwingine.

Suala la kujadili ni kuhusu sababu iliyotumika kuwazuia kushiriki bahati nasibu hiyo. (Hili tutalijadili baadaye).

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Mbali na suala hilo, uamuzi ambao umekuwa gumzo sana ni taarifa kuhusu Paul Makonda, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kupigwa marufuku yeye na mkewe kuingia Marekani.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje Marekani, imeeleza sababu ya kumzuia Makonda kuingia nchini humo kuwa ni ushiriki wake katika uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.

Taarifa hiyo iliyowekewa mkazo na ‘tweet’ ya Michael Pompeo, waziri wa Mambo ya Nje Marekani, imesema Makonda amekuwa akishiriki vitendo vya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, lakini hajaeleza kafanya matukio yapi.

Kwa vile hayajaelezwa, tunayo nafasi ya kuunda maswali; Makonda kafanya nini? Uamuzi uliochukuliwa una athari gani kwake na familia? Nini gharama ya nchi kwa uamuzi huo?

Swali kuhusu gharama ya nchi haliwezi kujibiwa bila kujiuliza kwanza Makonda ni nani katika nchi hii?

Kwa maudhui ya barua, Waziri Pompeo ametumia mamlaka aliyopewa na Sheria ya Operesheni za Kigeni, Ibara ya 7031 (C), kumpiga marufuku Makonda kukanyaga Marekani, kwa sababu ya ushiriki wake wa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.

Nashawishika kunukuu aya hii ya taarifa iliyotolewa na ofisi ya Pompeo: “Due to his involvement in gross violations of human rights, which include the flagrant denial of the right to life, liberty, or the security of persons.”

Kwa tafsiri ni kwamba; ni kwa ushiriki wa Makonda katika uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, ikiwemo kudhulumu haki ya kuishi, uhuru wa kujiamulia, au usalama wa watu.

Nimeshawishika pia kunukuu na aya zifuatazo: “Specifically, the Department has credible information that Makonda was involved in such violations in his capacity as the Regional Commissioner of Dar es Salaam.

“In that role, he has also been implicated in oppression of the political opposition, crackdowns on freedom of expression and association, and the targeting of marginalized individuals.”

Ni kwamba “Wizara ya Mambo ya Nje Marekani inazo taarifa zisizo na shaka kuwa Makonda amekuwa akihusika na vitendo hivyo kwa nafasi yake ya Mkuu wa Mkoa wa Dar ea Salaam.

“Na katika uhusika wake huo Makonda anahusishwa kunyanyasa wapinzani wa kisiasa, kukandamiza uhuru wa mawazo na kulenga (kushambulia) kundi la wachache.

Katika yote yaliyoelezwa, tuhuma nzito zaidi ambayo Marekani wameitoa ni ile ya kusema Makonda amehusika na dhuluma dhidi ya haki ya kuishi.

Swali; Makonda amedhulumu maisha ya nani? Hapa ndipo ukipatazama, unaona Marekani wamewaficha Watanzania siri nzito.

Kwa vipi wampe Makonda tuhuma nzito halafu waache kuzisema waziwazi? Mathalan, wangeeleza alimdhulumu nani na nani hiyo haki ya kuishi. Wamesema wanazo taarifa zisizo na shaka. Kwa hiyo wanalo jina au wanayo majina. Hii ni siri ambayo Watanzania wamefichwa. Wameachwa gizani.

Nje ya taarifa ya Pompeo, kwenye mitandao tangu taarifa ya Marekani ilipotolewa, kumekuwa na maoni kadhaa baadhi wakisema sababu ya Makonda kuzuiwa kuingia Marekani ni lile vuguvugu alilolianzisha la kupambana na watu wa mapenzi ya jinsia moja.

Ukweli ni kuwa katika taarifa ya Pompeo, suala la ushoga halijatajwa, labda kama limeunganishwa pale ilipoandikwa “targeting marginalized individuals,” yaani kulenga au kushambulia makundi maalumu.

Lakini kabla ya hapo kuna mambo mazito yanazungumzwa kama kudhulumu haki ya kuishi, uhuru wa kujiamulia, usalama wa watu na kunyanyasa wapinzani wa kisiasa.

Hata katika tuhuma kuwa amedhulumu uhuru wa kujiamulia, labda pia ikitafsiriwa kuwa ni matokeo ya kupambana na watu wa mapenzi ya jinsia moja. Pamoja na hivyo, eneo la kudhulumu haki ya kuishi ni linasalia kuwa kubwa, pia la kunyanyasa wapinzani linafuata, lakini yote hayo yangetakiwa kufafanuliwa zaidi.

Athari zake kwa Makonda

Sasa turudi kwenye swali la pili; uamuzi wa Marekani una athari gani kwa familia yake? Jibu ni kwamba athari ni kubwa. Zipo nchi ambazo Makonda na mkewe watapata wakati mgumu kuingia, hususan zile ambazo zina mkondo mmoja wa mfumo wa uhamiaji na Marekani.

Kwa uamuzi huo, Makonda hawezi kukubaliwa kuingia Canada na Australia ambazo zinachangia mfumo wa uhamiaji na Marekani, vilevile itampa wakati mgumu kuruhusiwa Uingereza.

Shida kubwa zaidi ni kuwa tuhuma za Marekani ni kubwa. Hivyo jina la Makonda litasomeka katika mitandao ya uhamiaji kuwa ni mtenda uhalifu hatari ambaye Marekani imempiga marufuku kuingia nchini mwake.

Athari zake kwa nchi

Nchi itapata athari gani kwa uamuzi wa Marekani? Kama nilivyosema awali, jibu linapaswa kufuata baada ya kumfahamu Makonda ni nani. Huyu ni mkuu wa mkoa na juu yake kuna viongozi wengi.

Athari ya nchi inaweza kuja kwenye eneo hili; wakati Makonda akifanya hayo ambayo Marekani wameyaona na kuona ni mtu hatari wa kumfungia na familia yake kuingia kwenye taifa hilo, viongozi wa juu yake wamekuwa wapi kumkemea? Tanzania ina vyombo vyenye mikono mirefu na macho mengi, kwa nini havijaona hadi waone Wamarekani?

Hapo ndipo taswira ya nchi inapoweza kuingia doa. Makonda anaweza vipi kudhulumu haki za watu za kuishi bila kuchukuliwa hatua na vyombo vya nchi?

Marekani wamejuaje?

Ingawa hawajaweka wazi wamejuaje hayo, inafahamika Marekani wana shirika lao ujasusi (CIA) ambalo maofisa wake kutawanywa katika mataifa mbalimbali duniani ili kufanya ujasusi. Maofisa wa CIA kwenye nchi ya kigeni, huripoti kwa mkuu wao ambaye huitwa Chief of Station.

Kila taarifa inayokusanywa kwenye nchi hupelekwa kwa Chief of Station ambaye huripoti kwa mkurugenzi wa CIA, Washington DC. Kisha taarifa hupelekwa kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Marekani.

Je, taarifa ya Pompeo kuhusu Makonda ni matokeo ya ujasusi wa CIA hapa nchini? Kama sivyo, amepataje, maana taarifa yake inasema wana ushahidi ambao hauna shaka kumhusisha Makonda na matukio ya uhalifu.

Kuzuia Greena card

Sababu zilizotolewa kuzuia Watanzania kushiriki Green Card Lotery ni matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini.

Unapata tafsiri kubwa kwamba Tanzania imeshachafuka katika eneo la utunzaji haki za binadamu. Makonda kosa lake ni kushiriki vitendo vya uvunjaji haki za watu na zuio la Green Card ni haki za binadamu.

Wapo watu wanasema kwani Marekani ni peponi? Turudi kwenye hoja ya msingi, hapa nchi imeingia kwenye rekodi ya kuvunja haki za binadamu. Ni doa kubwa kimataifa.

Na bado kuna utata wa masuala ambayo yameimbwa sana kimataifa kama kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda, kada wa Chadema Ben Saanane na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye na matukio mengine.

Kutokana na utata uliopo kuhusu masuala mbalimbali, Marekani ingeingia zaidi kwa kina ili kuweka picha iliyo wazi zaidi.

Columnist: mwananchi.co.tz