Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mara ngapi tumepora muda wa watoto?

10658 Joseph+Chikaka TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika makala haya tafsiri ya mtoto, ni yule aliye chini ya miaka 18 na ambaye bado yuko chini ya uangalizi wa mzazi au mlezi.

Ili nchi yoyote iweze kuendelea inahitaji rasilimali watu ambao imeiandaa vema kuweza kumudu wajibu wao kwa jamii.

Rasilimali watu hiyo haishuki tu kutoka mbinguni, huzaliwa, kukua na kupitia hatua mbalimbali za maandalizi kulingana na uwezo wa nchi husika.

Katika hatua zozote za maendeleo, hatua ya awali huwa ni ya msingi na haina mbadala.

Hii ni hatua ya utoto. Utoto ni kipindi muhimu kwa maandalizi ya mustakabali wa nchi yoyote katika nyanja zote.

Kwa mfano, mtu anapozungumzia uwajibikaji, ubunifu, michezo na mengineyo, hivi huchochewa tangu utotoni katika ngazi ya familia na vyombo vingine vya kijamii kama shule na maeneo ya ibada.

Ukitazama maeneo kama elimu, michezo, utamaduni na hali ya kupenda amani na nchi, vyote vinawezekana kama msisitizo utaanza kujengwa katika hatua za utotoni hasa kuanzia ngazi ya familia, jamii na vyombo vingine vya kijamii

Mzazi anavyopora muda wa mtoto

Shughuli mbalimbali zinazoandaliwa na mzazi zenye lengo la kumfurahisha mtoto wakati mwingine zimekuwa zikipora muda wa watoto kufanya kazi zao za nyumbani za masomo.

Watoto kuwa na uhuru wa kucheza na watoto wenzao wa rika lao katika mitaa yao huweza kuporwa kutokana na aina ya kuta na mageti yanayojengwa kutoruhusu mchangamano huo.

Kwa kitendo hiko kuna haki kadhaa za watoto huvunjwa kutokana na mifumo ya maisha pasipo watu kujua au kuzingatia.

Mifumo ya maisha ya kisasa imekuza staili mpya ya malezi ya usasa ya kwamba kila familia kulea na kushughulika na watoto wa familia yake tu.

Kwa mtindo huo, inakuwa siyo rahisi kwa mzazi kuamini kuwa shangazi au mjomba; jirani au rafiki anaweza kumlelea mtu mtoto wake kama ambavyo yeye mwenyewe anaweza kufanya.

Jambo hili wakati mwingine siyo sahihi kulishikilia kwa sababu hakuna mtu aliye na hakimiliki ya kuishi daima.

Kwa hiyo, mzazi anapomzuia mtoto kuchangamana na watoto wenzake katika kipindi cha utoto, atambue wazi kuwa anapora muda wa mtoto wa ukuaji na ujifunzaji katika kipindi hicho.

Saikolojia ya hatua za ukuaji wa mwanadamu ziko wazi kuwa hatua yoyote ya ukuaji inaporukwa au isipotimizwa ipasavyo, mara nyingi madhara yake huja kuonekana katika hatua za ukubwani.

Hivyo ni vema wazazi watahidi kutoa uhuru wenye mipaka kwa watoto wao katika kujifunza kwa kucheza na wengine au kutoka nje katika mazingira yao; kuliko kuwafungia ndani kwa kisingizio kuogopa eti watafundishwa tabia mbaya na watoto wa majiriani au kwamba watachafuka.

Wakati mwingine wazazi wasipokuwa makini kufuatilia mambo yanayojiri nyumbani wasipokuwapo, watoto wanaweza kunyimwa uhuru wa kucheza na dada wa kazi wanaowalea

Mwalimu anavyoweza kupora muda wa mtoto

Katika hatua za ukuaji wa binadamu kila hatua huwa na mabadiliko yake kulingana na mahitaji ya hatua hiyo.

Watoto ambao kwa bahati nzuri wako katika shule au madarasa ya awali wanahitaji uangalizi wa pekee ili waweze kukua na kujifunza vema.

Kwa mfano, mwalimu anapokuwa darasani na watoto tangu saa mbili mpaka saa sita mchana pasipo kuwa na shughuli za ujifunzaji na ufundishaji zenye vitendo, huwakosea sana watoto.

Madarasa hayo ya chekechea ujifunzaji wake hupaswa kuwa wa vitendo vingi vya kutenda au unaweza kusema kucheza.

Watoto walio katika madarasa ya awali mpaka darasa la pili, miili yao haina nguvu nyingi ya kuwakalisha darasani na kuwafundisha kama wanafunzi wakubwa wa sekondari au vyuo. Kufanya hivyo ni kupora muda wao wa ujifunzaji sahihi.

Jamii inavyopora muda wa watoto

Wapo watoto wanaoitwa wa mitaani, ilhali mitaa haina uwezo wa kuzaa watoto. Kundi hilo la watoto linaloishi katika mazingira magumu ni kundi lililoporwa muda wao wa utoto.

Jamii inaweza ikawa inawatazama tu na kufikiri kundi hili haliwahusu, lakini ni kundi linalohitaji jamii kwa ujumla kufikiria kupunguza visababishi.

Jamii inapaswa kupunguza matendo yanayotokea katika familia ambayo husababisha watoto hao kuishi mitaani.

Katika kundi hili, walio hatarini zaidi ni watoto wa kike. Wapo ambao utoto wao umekatishwa kwa sababu ya mimba za utotoni.

Jamii haina budi kuzidi kulipazia sauti suala la mimba hizi, kulikemea na kuweka mikakati kulingana na mazingira husika kulifuta.

Sehemu nyingine tamaduni zimekuwa chanzo cha watoto kuporwa muda wao wa kuwa shuleni kwa sababu ya mwamko mdogo wa elimu wa jamii hiyo au mtoto wa kike kuozwa.

Pia, watoto kutumikishwa katika shughuli za kilimo na ufugaji kumepora muda wao wa kuwa shuleni.

Aidha, changamoto za usafiri, ukosefu wa huduma ya mabweni na chakula shuleni, uduni wa miundombinu ya shuleni, haya nayo yanachangia wanafunzi wetu kuporwa muda wao wa utoto.

Jamii kwa ujumla ina wajibu wa kuona mtoto analindwa awapo katika ngazi ya kaya, mtaa mpaka taifa.

Ujumbe wa makongamano yanayofanyika kuhusu watoto, uzidi kusambazwa kwa watu wengi zaidi.

Kwa mfano, kila mwaka kumekuwa na maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, hivyo maazimio na ujumbe wake vizidi kuiamsha jamii kuhusu kulinda muda wa watoto ili usiporwe kwa sababu zozote zile.

Columnist: mwananchi.co.tz