Futari Chapchap
Jaribu uji wa viazi vitamu ufurahie futari yako
Kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kinywaji aina ya uji kinatumika sana na imekuwa kawaida katika kipindi cha mfungo.
Kuna aina mbalimbali za uji, kwa ufupi wapo wanaokunywa wa unga wa sembe na maziwa, unga wa ulezi, unga na wa unga wa muhogo.
Leo wafuatiliaji wa kolamu hii nitawaelekeza jinsi ya kupika uji wa viazi vitamu.
Mahitaji:
Viazi vitamu vikubwa viwili au kulingana na ukubwa wa familia.
Maziwa freshi (ya maji) kikombe kimoja na nusu
Sukari nusu kikombe
Iliki ya unga robo kijiko cha chai
Karanga zilizosagwa kulingana na wingi wa viazi.
Jinsi ya kutayarisha
Chemsha viazi hadi viive vizuri.
Menya maganda kisha kiponde hadi kiwe laini kwa kutumia mwiko au kisage kwenye mashine (blenda)
Weka viazi vilivyosagwa kwenye sufuria utakayotumia kupikia, weka maziwa, karanga na sukari kisha changanya vizuri hadi vichanganyike.
Punguza moto, weka iliki na koroga tena na uache uchemke kwa dakika 10 hadi 15 kwa moto mdogo sana kisha uipue tayari kwa kunywewa.
Mchemsho wa samaki
Kwa kuwa futari huliwa na watu waliofunga inahitaji kuwe na kitoweo kidogo hivyo kutokana na changamoto ya muda, mchemsho wa samaki na mbogamboga unafaa.
Mahitaji
Samaki wawili wakubwa kiasi
Karoti
Pilipili hoho
Pilipili mbuzi (pilipili kali)
Vitunguu maji
Chumvi
Nyanya
Ndimu
Jinsi ya kuandaa
Osha samaki vizuri.
Osha nyanya, hoho, kitunguu maji na karoti kisha katakata kila kimoja katika vipande vidogo.
Weka vitu vyote katika sufuria isipokuwa chumvi na pilipili mbuzi (pilipili kali).
Funika na acha vichemke kwa nusu saa. Kisha weka
chumvi na pilipili mbuzi, utaangalia maji yaliyomo kwenye mchemsho wako wa samaki kama yanatosha supu, kama hayatoshi ongeza kidogo, acha ichemke na itakuwa tayari kwa kuliwa.
Hizi ni futari tatu unazoweza kuzipika kwa haraka ukiwa na saa moja na nusu zitakuwa tayari kwa kuliwa.
Muhimu: Siyo vibaya ukitumia majiko mawili ili kuokoa muda.