Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maneno wanayotumia wanawake na maana zake

43488 Pic+maneno Maneno wanayotumia wanawake na maana zake

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna maneno yanaposemwa na mwanamke, huwa na maana tofauti na ile iliyoandikwa kwenye kamusi. Tuyaongelee machache.

Dakika tano

Kimsingi maneno dakika tano yanatakiwa kumaanisha ‘dakika tano’. Na hutumika mmoja anapomuahidi mwingine kuwa aidha atamuhudumia ndani ya dakika tano, au atafanikisha jambo ndani ya dakika tano.

Lakini mwanamke anaposema dakika tano, wakati wa kujiandaa kwa safari, maana yake atakuwa amekamilisha ndani ya dakika 30 au saa nzima.

Endelea

Kwa kawaida mtu anapokwambia endelea anamaanisha uko sahihi na unachokifanya hivyo unaweza kuendelea. Lakini kwa mwanamke, ina maana mbili, niamini mimi. Ya kwanza ni pale anaposema huku uso wake ukiwa kama haujabeba hisia yoyote, au anapoisema akiwa amepandisha juu nyusi zake, au mara baada ya kuisema tu akanyamaza. Hapa anachomaanisha ni amechoka na tabia yako au jambo mlilokuwa mnaongelea, kwa hiyo sasa anakupa uhuru wa kufanya zaidi, lakini ujiandae kupokea malipizo ya kufanana na hicho.

Anaposema endelea, akiwa na huzuni, mathalani kulia kabisa. Anamaanisha unachomfanyia si sahihi, lakini kwa sababu anakupenda au anakuhitaji, hana budi kuvumilia, na kukuacha ufanye unavyotaka. Kwa hiyo maana ya ndani hapa ni kukuomba ubadilike, si uendelee.

Asante sana

Asante inaweza kuwa na maana ya kawaida ya asante, kwamba anashukuru kwa ulichomfanyia. Lakini unatakiwa uipime na jambo ulilomfanyia. Kama ni jambo zuri, hiyo ni asante. Kama ni la hovyo na bado umepewa asante, hiyo ni suala jingine.

Lakini sasa ikifikia hatua hadi akakwambia asante sana, elewa hamaanishi kwamba anakupa shukrani kubwa, hapana. Anachomaanisha ni ulichomfanyia ni kibaya kupita maelezo, lakini kwa sababu kuua ni kosa kisheria na dhambi kwa Mungu hatokuua, lakini kisanga na songombingo atakachokusababisha siku za mbeleni, utalia na kusaga meno.

Kuguna kwa sauti ya juu

Kuguna si neno ila ni neno kukifanywa na mwanamke. Na mara nyingi linatumika wakati wewe umeongea sana, halafu ukanyamaza.

Mfano, mpo mnabishana jambo, mathalani unajitetea juu ya kosa fulani au suala la kufanya maamuzi yanayohusu nyote wawili. Halafu wewe ukataka kuonyesha uanaume wako, utawale malumbano kwa kuzungumza zaidi, yeye akakuelewa, akanyamaza, akupe nafasi ya kuinjoi. Kisha unapomaliza kuzungumza tu akaguna kwa sauti ya juu.

Anachosema ni kwamba, kwa jinsi alivyotathmini akili zako wakati unazungumza, haelewi ni kwa nini mpaka dakika hiyo upo ndani ya nyumba kama mume wake, au mpenzi wake. Kwa akili zako, ulitakiwa upewe kitanda Milembe.

Sawa

Mkiwa mnazungumza, hasa mnabishana kuhusu jambo lenu wawili, mwanamke akisema sawa, hamaanishi amekubaliana na mtazamo wako juu ya jambo. Sawa ya mwanamke sehemu kama hizi ni kwamba; ‘Mimi niko sawa, Ila nimechoka kelele, nataka ufunge bakuli lako.”

Ndiyo maana, usijiroge hata siku moja mwanamke avae afu akuulize, unaonaje hapa? Halafu wewe umjibu ‘uko sawa’ – Ni kiama unajitafutia.



Columnist: mwananchi.co.tz