Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo ya kufanya unapokuwa na bosi msiyeelewana

76390 AJILAPIC

Thu, 19 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bila shaka wafanyakazi karibu wote tungependa kufanya kazi chini ya bosi mzuri, anayetusaidia kufikia malengo ya taasisi, anayetuwekea mazingira ya kutekeleza wajibu wetu kwa furaha, anayetuthamini, na zaidi ya yote mwelewa na mtenda haki pale tunapofanya makosa ya kibinadamu.

Lakini kwa bahati mbaya mambo katika ofisi zetu saa nyingine huwa tofauti.

Unajikuta ukifanya kazi na bosi msiyeelewana, mbaguzi, asiyejua aongee nini na wapi, lakini wakati mwingine anayefurahia kuonea watu bila sababu.

Si hivyo tu, wakati mwingine anaweza kuwa bosi asiyeamini mtu na hivyo anakuwa kama mtu anayetaka kufuatilia karibu kila kitu kinachofanywa na watu wa chini yake, mkorofi, hajui kudhibiti hasira zake au hana uwezo wa kiuongozi.

Hapa ninakuletea mapendekezo machache ya mbinu unazoweza kuzitumia kukabiliana na bosi mwenye hulka hizi.

Mwelewe kwanini yuko vile alivyo

Pia Soma

Advertisement
Huwezi kukabiliana na tabia usiyoielewa. Hatua ya kwanza ni kuelewa kilicho nyuma ya tabia. Jiulize, kwa nini bosi ni mkali? Kwa nini anapenda kubagua watu? Ugomvi wake unatokea wapi?

Je, anachokifanya bosi ni makusudi au kuna kisababishi kilicho nje ya uwezo wake? Je, inawezekana ni matatizo ya kifamilia yanayoathiri tabia yake, shinikizo analolipata kutoka kwa walio juu yake au ni tabia zako pia zinachangia?

Hoja yangu hapa ni kwamba ni muhimu uelewe kuwa kila tabia ya mtu ina sababu nyuma yake. Tena mara nyingi watu huwa hawaoni upungufu wao.

Ukifahamu kinachochangia haya yote itakuwa rahisi kujua hatua zaidi za kuchukua.

Usiruhusu tabia ya bosi iathiri kazi yako

Haijalishi tabia ya bosi ni mbaya kiasi gani, usiipe nafasi ikaathiri kazi yako.

Kwa vyovyote iwavyo, unahitaji kufanya kazi na bosi wako. Huyu ndiye mtu anayekupa maagizo utakayolazimika kuyatekeleza, ndiye atakayepokea taarifa ya kazi yako na maoni yake yana nguvu ya kuamua kiwango cha utendaji wako.

Badala ya kulalamika na kupoteza ari ya kazi, jifunze namna ya kukaa naye bila kuathiri utendaji wako.

Kwa mfano, kama ni mtu mkali, usitarajie atakuwa mpole. Kubali ukweli kuwa hivyo ndivyo alivyo na itakusaidia kwa kiasi kikubwa kulinda moyo wako.

Kama anapenda kufuatilia kila kitu kwa karibu, jifunze kuwa mbele ya makataa (deadline) na kufanya kazi kwa umakini na ubora.

Pambana kuhakikisha anapata kazi mapema kabla ya wakati, taratibu tabia ya kukufuatilia kupita kiasi itapungua. Hoja yangu hapa ni kwamba unapomfahamu mtu inakuwa rahisi kukwepa mazingira ya kukwazika.

Bosi hawezi kujua kila kitu

Nafasi na madaraka havimfanyi mtu ajue majibu yote kwa wakati wote. Kuteuliwa kuwa mkuu wa kitengo haimaanishi mtu ghafla anageuka kuwa mjuzi wa kila kitu kwenye taasisi.

Mtu anaweza kuwa bosi lakini hajajifunza namna ya kuwasilisha mawazo yake.

Wapo wanaoamini kuwa ukweli lazima usemwe hata kama kwa kuusema wanaudhi watu. Hawa hawajajifunza namna ya kusema ukweli kwa upendo bila kuumiza wengine.

Wapo wanaofikiri ukishakuwa bosi lazima ujitutumue kuonyesha nguvu zako. Wanaamini usipofanya hivyo unaowaongoza watakudharau na mambo hayataenda.

Unapogundua kuna kitu bosi hakijui na kinaweza kuathiri kazi, tafuta uwezekano wa kupata hadhira naye ikiwa mazingira yanaruhusu. Wakubwa wengi ni wasikivu ukijifunza namna ya kuwashauri.

Onesha uongozi

Kila mfanyakazi ni kiongozi, Unaweza usiwe na madaraka lakini ukawa kiongozi. Uongozi ni kuonyesha njia. Uongozi ni uwezo wa kuwashawishi wengine wapambane kufikia malengo uliyonayo.

Unapofanya kazi na bosi asiyeweza kazi, kwa mfano, hiyo ni fursa ya wewe mwenyewe kuwa kiongozi. Fahamu eneo lako vizuri, simamia malengo ya nafasi yako kisha onyesha matokeo.

Unapofanya hivi bila hila na kujionyesha watu watakuheshimu. Uongozi wa taasisi utakuona hata kama huna nafasi yoyote ya uongozi.

Linda mipaka yako

Huwezi kufanya kila kitu ofisini. Kila mfanyakazi ana mipaka ya majukumu yake. Unahitaji mipaka pia kwenye namna unavyohusiana na watu.

Fahamika unaamini nini; kitu gani huwezi kukifanya bila kujali amri imetokewa na nani. Wapi huwezi kwenda na kitu gani huwezi kamwe kujihusisha nacho hata iweje. Chora mstari ambao mtu yeyote hawezi kuuvuka.

Lakini upande mwingine, mipaka ni pamoja na wewe kufahamu kanuni za kuishi na watu wenye tabia zisizofaa.

Mfano mtu anakwambia vitu vya kijinga na haonekani kujali, jifunze kumwomba arudie kile alichokwambia.

“Bosi ndicho unachomaanisha?” akikubaliana na kile ulichorudia, mwombe afafanue. Unapofanya hivi, unamsaidia kujisikiliza zaidi na kugundua ujinga wake bila wewe kumjibu.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi.Twitter: @bwaya, 0754 870 815

 

 

Columnist: mwananchi.co.tz