Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo matano yaliyoibeba Singida Nakuru

8912 Pic+singida TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

SINGIDA United imeibuka washindi watatu wa michuano ya SportPesa Super Cup 2018 baada ya kuichapa Kakamega Homeboys kwa mikwaju 4-1.

Mechi hiyo iliyoanza majira ya saa sita mchana ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90, ambapo Wicklif Opondo alifunga la Kakamega na Danny Lyanga akiifungia Singida la kusawazisha.

Singida iliingia kwenye mikwaju ya penalti kwa kujiamini na kumaliza kwenye nafasi hiyo ya tatu ambayo inawapatia Dola 7,500 (Sh16 milioni)

Mwanaspoti ambalo liko mjini hapa linakuletea sababu tano zilizoibeba Singida United kwenye mashindano ya mwaka huu.

 

Peter Manyika JR

Kama kuna kitu ambacho Singida United itajivunia kwenye michuano ya mwaka huu ni kiwango cha golikipa, Peter Manyika JR. Kipa huyo alionyesha umahiri mkubwa kwenye michuano hiyo katika mechi zote.

Kipa huyo aliibeba Singida kwenye pambano la robo fainali dhidi ya AFC Leopards ambapo walishinda kwa penalti kabla ya kuonyesha uwezo wa juu tena kwenye mikwaju hiyo katika mechi ya mshindi wa watatu dhidi ya Kakamega.

 

Wachezaji wako fiti

Kucheza na timu za Kenya siyo jambo la wepesi hata kidogo. Unahitaji kuwa fiti kwa mapambano ya dakika 90 ama 120.

Wachezaji wote wa Singida walionyesha utimamu huo wa mwili. Walikuwa fiti kwenye mechi zote. Walipambana kwa dakika zote na kuweza kushinda mechi mbili japo ni kwa mikwaju ya penalti.

Straika wao Danny Lyanga na winga, Deus Kaseke walikuwa na kasi kwenye mechi zote. Walizisumbua timu pinzani na kuifanya timu yao iwe mchezoni.

 

Wachezaji wa benchi

Kama kuna kitu ambacho Singida United inajivunia ni uwepo wa wachezaji wenye viwango vya juu kwenye benchi lao. Uwepo wa Salum Chuku, Elinywesia Sumbi, Lubinda Mundia na wengineo uliipa Singida nguu.

Mfano kwenye mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Kakamega Homeboys, Sumbi aliingia na kubadilisha mchezo kabisa ikiwemo kutoa pasi ya bao la kusawazisha lililofungwa na Danny Lyanga.

Chuku naye alibadilisha mchezo kwa kiasi kikubwa kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Leopards na kuifanya timu yao kuwa tishio.

 

Mbinu za Morocco

Yawezekana kocha Hemed Morocco bado anaendelea kuizoea timu hiyo taratibu lakini kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup alikuwa na maamuzi sahihi.

Morocco alikuwa sahihi kwenye kupanga kikosi na hata kufanya mabadiliko kwenye mechi hizo. Alisoma mchezo kwa haraka na kubadilisha mambo.

Kocha huyo ambaye alianzia kazi yake kwenye mashindano haya ya SportPesa, huenda akafanya makubwa na timu hiyo.

 

Kiungo wao mpya

Kiungo mpya wa Singida United, Amara Diaby naye ni miongoni mwa watu waliofanya kazi kubwa kwenye ushindi wa Singida.

Kiungo huyo ameiziba vizuri nafasi ya Mudathir Yahya na kuifanya timu hiyo icheze kwa utulivu mkubwa.

Diaby ni mgeni kwenye timu lakini alicheza kwa kiwango kikubwa kwenye mechi zote tatu, alipunguza majukumu ya ulinzi yaliyokuwa yakifanywa na Kennedy Juma, Malik Antri na Salim Kipaga.

Columnist: mwananchi.co.tz