Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo matano ya kuzingatia unapojieleza mbele ya watu

10073 Cristian+Bwaya TZW

Tue, 26 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika nyakati tofauti sote hujikuta tunalazimika kujieleza mbele ya watu.

Unaweza kwenda kwenye mikusanyiko ya kijamii kama sherehe, misiba na matukio mengine na bila hata kutarajia ukaombwa kusema jambo.

Kwa upande wa wanafunzi, unaweza kupewa kazi ya kufanya utafiti wa maktaba ili kujibu swali ulilopewa na mwalimu wako na kisha kutakiwa kueleza kile ulichokipata mbele ya wanafunzi wenzako.

Wakati mwingine utalazimika kuchangia mawazo kwenye mijadala inayofanyika mbele ya kadamnasi ukishuhudiwa na walimu, wataalamu, wanafunzi wenzako na watu wengine wanaokuzidi uelewa.

Sote, bila kujali wapi tumetakiwa kuzungumza mbele ya watu, tungetamani kufanya vizuri. Hakuna mtu angependa kujikuta akifedheheka mbele ya kadamnasi.

Makala haya yanalenga kukusaidia kuelewa kanuni rahisi za kuwa mzungumzaji mahiri. Hapa ninakuletea baadhi ya maswali muhimu unayohitaji kuyajibu kabla na wakati unapozungumza mbele ya watu.

Unaaminika?

Huwezi kueleweka kama hadhira yako haikuamini. Watu wanaokusikiliza wanahitaji kujiridhisha kuwa unazo sifa za kuzungumza kile ulichonacho. Ili wakusikilize, unahitaji kuheshimu na kukidhi kiu hii ya kukufahamu.

Anza kwa kujitambulisha kwa ufupi. Sema sifa chache ulizonazo zinazoweza kuwashawishi watu kuwa kweli unajua kile unachotaka kukisema.

Unapojitambulisha, hata hivyo, kuwa makini usionekane unajigamba au una sifa zinazofanya usiaminike. Ukijipambanua kama mfuasi wa mrengo fulani wa kisiasa/kidini usitarajie kuwa watu wenye mrengo tofauti na wako watakusikiliza.

Ikiwa unazungumza na hadhira ya watu waliosoma, pengine watahitaji kujua kiwango chako cha elimu na uzoefu ulionao kwenye eneo unalotaka kulizungumzia.

Kwa hadhira ya watu wasiosoma sana mwonekano mzuri ni mtaji. Watu wa kawaida mara nyingi huangalia mambo madogo kama mavazi, mtindo wako wa kunyoa, namna unavyoongea na mambo kama hayo. Jiweke kwenye mwonekano nadhifu.

Nini kiini cha ujumbe wako?

Kabla hujataka watu wakuelewe, ni muhimu uelewe kwa hakika unataka kusema nini na kwa sababu gani.

Jiulize kipi hasa ni kiini cha ujumbe wako? Je, ni kuwafariji wasikilizaji, kuwashawishi wabadili mtazamo wao au kuwahamasisha wafanye kitu fulani? Kitu gani hasa ungependa kitokee baada ya mazungumzo yako?

Unapokuwa na uhakika nini hasa unataka kukifikisha kwa wasikilizaji wako hutawapotezea watu muda wao. Utatoa mifano inayoendana na ujumbe wako mkuu, utatulia kwenye ujumbe mkuu na hivyo wasikilizaji wako watakuelewa zaidi.

Unayaelewa matarajio ya wasikilizaji?

Pamoja na ujumbe mzuri ulionao, hakikisha unaelewa na kuheshimu matarajio ya hadhira yako. Fanya utafiti kuelewa wasikilizaji wako wanajitambulisha na kitu gani.

Uelewa huo ni muhimu kwa sababu utakusaidia kujipanga vizuri namna utakavyoweza kuufikisha ujumbe wako bila kuamsha hisia za kukupinga.

Ikiwa hadhira yako inaungwa na watu wenye kiwango kikubwa cha elimu, utakuwa na kazi ya kuonesha uelewa mpana kuhusu hicho unachotaka kukieleza, kwa sababu wasomi wana tabia ya kuchambua mambo kwa kina.

Kwa watu wasiosoma fikiria kuufanya ujumbe wako uwe wa kuleta matumaini na kuonyesha bayana nini cha kufanya kuliko kuchambua. Ukijikita kwenye uchambuzi unawachosha wasikilizaji.

Pia kuna suala la umri. Watu wazima huwa na misimamo mikali kwa mambo yanayowagusa kuliko vijana. Badala ya kutaka wabadilike, jenga kwenye misimamo ile ile waliyonayo na chukua tahadhari unapoeleza jambo wasilolifahamu. Kwa vijana ni rahisi kuwashawishi lakini ni muhimu uwe na uwezo mkubwa wa kuonyesha kuwa unatambua changamoto wanazopitia.

Unafanyeje kuongeza ushawishi wako?

Huwezi kufurahia kuzungumza jambo na bado upingwe. Mzungumzaji mzuri hutamani wanaomsikiliza wakubaliane na kile anachokisema.

Huo unaitwa ushawishi. Ukitaka kuwa na ushawishi kwa wasikilizaji wako kuna mambo kadhaa ya kuzingatia. Kwanza, onyesha uelewa kwa kile wanachokiamini hata kama hukubaliani nacho.

Mfano unalenga kuwashawishi vijana waache ngono kabla ya ndoa. Hapa una kazi ya kuwafanya waamini unaelewa upande wao na epuka kuwazodoa kwa tabia zao. Ukifanikiwa hilo, ndipo ueleze upande wa pili wa namna wanavyoweza kupambana na mihemuko ya mwili.

Pili, unapotaka kuwashawishi wasikilizaji wako usiwe mbali sana na kile wanachokiamini. Tuchukulie unataka wasikilizaji wako wabadili tabia fulani. Fahamu binadamu huwa tunajitambulisha kwa tabia zetu hata kama hatuzipendi kimsingi.

Unapokejeli tabia hizo ni sawa na kuwadhalilisha. Si watu wengi wanaweza kuafikiana na mtu anayeonekana kuwadhalilisha. Badala ya kujionyesha ulivyo tofauti na wao, jitahidi wayaone maisha yao kupitia mazungumzo yako, kwa maana ya kukuona kama mwenzao na sio malaika au mtu anayekuja kuwabadilisha.

Jambo la tatu, jenga kwenye uzoefu wako zaidi. Simulia mambo unayokutana nayo na namna unavyokabiliana nayo. Wasikilizaji wako watakusikiliza kwa sababu ni vigumu mtu kupingana na kitu unachokiishi.

Pale unapolazimika kueleza mambo ya kitaalam (facts) ambayo pengine huyaishi, basi tumia takwimu na matokeo ya tafiti mbalimbali kuishawishi hadhira yako kuwa unachokizungumza sio mawazo yako binafsi.

Ufanyeje unapokuwa na hofu?

Kila mmoja wetu, bila kujali haiba yake, anaweza kuwa mzungumzaji mzuri akifuata kanuni. Changamoto kubwa, hata hivyo, ni hofu. Ingawa kiwango fulani cha hofu kinahitajika ili kukufanya ujiandae zaidi, lakini hofu ikizidi itakunyang’anya ujasiri.

Katika kukabiliana na hofu ya kuzungumza hadharani, jifunze kuwachukulia wasikilizaji wako kama watu wa kawaida. Usitishwe na wasifu, elimu wala uzoefu walionao.

Tumia dakika za mwanzo vizuri kuwavuta wasikilizaji wako. Mara nyingi tunashauriwa kuanza kwa kusimulia jambo lililowahi kutukuta lenye uhusiano na kile tunachotaka kukieleza. Unaweza pia kutumia kichekesho kama namna ya kuzoeana na hadhira yako. Unapofanya hivi, kuna namna fulani unapata ujasiri.

Columnist: mwananchi.co.tz