Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mambo 6 ya kuyafahamu mwanao wa miaka 5 akipotea

73783 Mtoto+pic

Mon, 2 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki chache zilizopita mtoto wa mwenzetu alipoteana na mama yake katika tamasha akiwa katika kusheherekea. Kwa dakika kadhaa mama yake alipata hofu akidhani kampoteza mwanae. Baada ya muda mfupi alimpata mwanae na ikagundulika, taratibu alikwenda kwenye moja ya ofisi aliyoizoea alipokutana na ‘anti’ yake (rafiki wa mama). Tukio hili likatufanya tujiulize nini kingetokea endapo angepotea kweli, angefanyaje? Baaada ya mjadala tukaja na orodha ya mambo 6 muhimu kwa mtoto wa miaka 5 kuyafahamu ili kumsaidia kama atapotea.

Jina kamili la mzazi. Ni muhimu kwa mtoto kufahamu kuwa “baba “na “mama” wanayo majina. Katika umri wa miaka mitano, mtoto wako anapaswa kujua majina yako, na kama huwatembelea bibi na babu ni vyema akayajua majina yao pia. Hii itamsaidia endapo amepotea, arudishwe nyumbani kwa urahisi. Mara nyingi wazazi na walezi huwa na majina maarufu yanayofahamika kwa majirani zaidi, hayo ndiyo hasa muhimu mtoto kuyajua.

Namba za simu za mzazi/mlezi. Ingawa ni rahisi kwa mtoto wa umri huu kuyafahamu majina, kukariri namba inaweza kuwa changamoto lakini jitahidi kumsaidia kukariri angalu namba yako mojawapo. Namba nyingine muhimu zinaweza kuandikwa kwenye kadi ambayo mwanao hutembea nayo mara kwa mara na anaweza kuzirejelea wakati wa dharura. Haitakuwa rahisi kuzikumbuka lakini unaweza kutumia hata wimbo kumsaidia azikariri.

Kufahamu anuani ya nyumbani na sehemu maarufu karibu na nyumbani. Mfundishe jina la mtaa na eneo analoishi. Kama ni karibu na shule, msikiti, kanisa, hospitali, hoteli, soko nk, msaidie afahamu majina ya sehemu hizo, inaweza kumsaidia hata kupelekwa ofisi za serikali za mitaa.

Mahali unapofanya kazi. Watoto huwa na maswali juu ya wapi wazazi hushinda siku nzima. Wanaenda wapi na kwa nini wanaenda huko kila siku? Wanafanya nini hasa? Ni rahisi kuwaaga watoto wetu na kuwaambia tunaenda ofisini. Muhimu mtoto afikapo miaka mitano afahamu kazi unayoifanya kwa namna rahisi ambayo ataweza kuelewa. Ni muhimu kuhakikisha anafahamu jina la ofisi au eneo iliyopo. Hii itakuwa njia rahisi ya kukutafuta endapo mwanao amepotea.

Kuomba msaada kwa umakini. Kwa usalama wetu, zamani tulikatazwa kuongea na tusiowafahamu. Muhimu mwanao makini, anaweza kuhitaji msaada wa mtu asiyemjua wakati mwingine ili kurudishwa nyumbani. Baadhi hushauri kuomba msaada kwa mama mwenye watoto. Anaweza pia kuomba msaada kwa muuza duka kutegemea na eneo alilopo, mfanyabiashara hasa wa vyakula na matunda hususani mwanamke.

Pia Soma

Advertisement   ?
Piga namba 116. Hii ni namba ya huduma ya simu kwa mtoto nchini. Ni namba isiyotoza gharama, inayotoa huduma kwa watoto wanaohitaji ulinzi nchi nzima. Kama mwanao amepotea na hawezi kukupata wala kukumbuka namba yako ya simu, basi anaweza kupiga 116 au kumuomba mtu mzima amsaidie kupiga namba hii. Kupitia namba hii atajieleza na tutaweza kufanya kila lililopo ndani ya uwezo wetu kumhudumia kwa kushirikiana na watoa huduma za watoto nchini ikiwemo maofisa ustawi wa jamii, maofisa wa polisi wa dawati la jinsia na watoto pamoja na maofisa wa serikali za mitaa, kuhakikisha mwanao anarejeshwa nyumbani salama.

Ni matumaini yetu kuwa njia hizi zitasaidia endapo mwanao atapotea. Kumbuka kuwa vitu muhimu zaidi kwa mtoto kufahamu kila wakati ni jina lake, shule anayosoma, majina ya wazazi wake na namba zao za simu na mahali wanapofanya kazi.

Columnist: mwananchi.co.tz