Dar es Salaam. Wanasema kazi ndiyo msingi wa maisha, lakini ili uifanye kwa ufanisi huku ukiwa na amani, yapo mambo ya kufuata.
Lakini baadhi ya wadau wa masuala ya kazi wametaja mambo 10 ya namna ya kuwa na amani kazini.
Mambo hayo yanamwelekeza mfanyakazi yeyote juu ya kipi cha kufanya ili awe na amani na ufanisi awapo kazini.
Katika orodha hiyo jambo linaloongoza ni lile linalomwelekeza mfanyakazi likisema; “Usimuamini yeyote, lakini heshimu wote.”
Kuhusu hilo, William Kasembe (61) aliyefanya kazi na mashirika mbalimbali nchini ikiwamo serikalini na binafsi kabla ya kustaafu alisema; hili ni jambo la msingi wa amani kazini.
“Unaweza kuamini umepata rafiki kazini, wakati mwingine hata bosi wako, kumbe ndiye adui yako na siku moja atakuchoma,” alisema.
Alisema ni bora kuweka heshima kwa mkubwa na mdogo lakini kuepuka kumsengenya mfanyakazi mwenzako au kumuongelea kwa lolote.
“Mara nyingi hili huweza kukurudi na kukusababishia msongo hata ukaacha kazi,” alisema.
Wameitaja jambo lingine kuwa ni; “Kinachotendeka kazini, kibaki kazini. Usipeleke mambo ya kazini nyumbani au ya nyumbani ofisini.”
Jambo la tatu linasema; “Ingia kazini kwa wakati, ondoka kwa wakati. Kompyuta yako haiwezi kuimarisha afya yako.”
Hili linathibitishwa na utafiti uliofanywa mwaka 2012 na Taasisi ya Saikolojia ya Uingereza.
Utafiti huo ulibaini kuwa wanaofanya kazi kwa zaidi ya saa 12 kwa siku, wapo hatarini kupata maradhi ya moyo au kiharusi.
Kadhalika, Chuo Kikuu cha London kilifanya utafiti mwingine mwaka 2014 na kubaini kuwa wanaofanya kazi kwa zaidi ya saa 55 kwa wiki, wapo hatarini kupata maradhi ya moyo.
“Usidhani bosi wako anaguswa zaidi na unavyokaa sana ofisini, hata kidogo, anaangalia ufanisi,” unasema utafiti huo.
Jambo lingine ni; usijenge uhusiano kazini, mara nyingi hukurudi.
Thomas Jefferson wa kitengo cha Saikolojia Chuo Kikuu cha Munich, Ujerumani anasema katika utafiti wake wa ‘mabaya, mazuri ya uhusiano kazini’ changamoto ni pale mnapoachana.
“Mkiachana, utajikuta ukimuona mpenzi wako wa zamani kila siku. Hii ni ngumu kwa yule ambaye hakutaka uhusiano uishe. Hali hii itaharibu utendaji wake na kujenga chuki,” anasema.
Katika utafiti huo, Jefferson anasema bosi wako anaweza kutumia uhusiano wako kama fimbo ya kuwa wewe si mfanisi kazini.
Jambo lingine ni mfanyakazi kuwa na amani; “Usitegemee lolote. Kama ukisaidiwa, shukuru, kama hukusaidiwa utajifunza kujua mwenyewe.”
Amos Chalamanda, (78) aliyefanya kazi tangu enzi za ukoloni alisema ukisubiri kupewa msaada kazini utaua taaluma yako na kisaikolojia unadunisha uwezo wa ubongo wako kuchangamka.
“Hii kisaikolojia, ikishajengeka kuwa unapenda ‘free lunches’ basi hutakuwa na uwezo wa kujifunza, bali kutegemea hisani. Hii ni mbaya zaidi kwa wanawake,” alisema.
Alisema kuna vitu vya kusaidiwa lakini si sahihi kuishi kazini ukitegemea kushikwa mkono.
Nyingine ni ile isemayo; “Usikimbilie nafasi kazini. Ukipandishwa cheo, hongera. Kama hukupandishwa, haijalishi. Utakumbukwa kwa ujuzi wako si kwa cheo chako.”
Nyingine inasema; “Usikimbilie kufanya mambo yaliyo nje ya wajibu wa kazi.”
Kadhalika, jambo la nane linasema; “Usiyachukulie mambo kibinafsi. Mshahara wako ni muhimu. Tumia mshahara huo kupata furaha na si kukutesa.”
Jambo la tisa linasema; “Usijali kampuni au bosi wako anakufanyia nini. Kuwa mnyenyekevu.”
Jarida la uchumi la Forbes limewahi kuchapisha makala isemayo ‘Kwa nini ni muhimu kuwa mnyenyekevu kazini’.
Katika makala hayo, mwandishi ameandika; “Unyenyekevu siku hizi unaonekana kama udhaifu hasa kwa wenye vyeo, lakini unyenyekevu ni bidhaa muhimu.”
Inaeleza kuwa unyenyekevu ni pamoja na kuuliza, kuzungumza mara chache na kusikiliza zaidi, kukiri makosa na kujua kuwa hutakuwa kwenye nafasi ya juu milele.
“Ukimya unakusaidia kuelewa na kuchambua mambo kabla ya kujibu, kuomba ushauri, taratibu mambo haya huchangia utendaji wenye tija.”
Jambo la 10 linasema; “Mwisho wa siku, hakuna cha muhimu kama familia, marafiki na amani ya moyo.”
Dk Jeffrey MacMaster ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi wa Marekani, katika moja ya maandiko yake alisema alipoteuliwa kuwa kiongozi mkubwa katika kampuni moja alitumia nguvu nyingi kufanya kazi na almanusura aiweke rehani familia.
“Lakini nikagundua baadaye sana kuwa ninaweza kupoteza kazi au kuacha ikiwamo kupoteza zile sifa na kutambuliwa kwangu, lakini familia bado itabaki palepale, nikagundua kuwa familia ni muhimu kuliko kazi,” alisema.
“Nikajifunza kufanya kazi kwa muda wake na kutenga muda mwingi na familia,” alisema.