Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mali ya umma inahitaji uwazi kuilinda

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Suala la uwazi katika mali ya umma ni jambo ambalo linajirudia akilini mwangu tangu Juni Mosi baada ya kusikia majibu ya Serikali kuhusu hoja ya wabunge waliohoji malipo ya fedha za fidia kwa serikali katika biashara ya makinikia.

Kauli hiyo ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Pallamagamba Kabudi akijibu hoja za Saed Kubenea (Ubungo) na Rashid Shangazi wa Jimbo la Mlalo, waliotaka kujua yalipofikia mazungumzo kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick kuhusu makinikia na mikataba ya uwekezaji.

Bila kufafanua wala kuingilia undani wa suala hilo, Waziri Kabudi aliliambia Bunge kuwa mazungumzo hayo yamefikia pazuri na yanaweza kufikia hitimisho Juni au Julai.

Katika majibu hayo, Waziri huyo akasema serikali inaendelea kufanya majadiliano na makampuni mengine 10 ya uchimbaji madini ili kuhakikisha utajiri na maliasili hiyo inanufaisha Watanzania.

Binafsi sina tatizo na mkakati wa kujadiliana na kampuni hizo, na ninaipongeza Serikali kwa maendeleo mazuri katika majadiliano hayo ambayo hitimisho lake linaweza kuihakikishia Taifa mapato ya mabilioni ya shilingi.

Mapato hayo ni kutokana na fidia au malipo ya mapunjo yaliyotokana na mikataba isiyojali masilahi ya umma tuliyoingia na wawekezaji katika sekta ya madini.

Profesa Kabudi, alikwenda ndani akalieleza Bunge kuwa Serikali inachelea kuweka hadharani taarifa na kiwango cha fedha kitakacholipwa na wawekezaji hao, eti kwa kuogopa watu “wasiolitakia mema Taifa kufungua kesi ya madai dhidi ya Serikali.”

Kauli hiyo ikanifanya nikumbuke hadithi moja niliyowahi kuisikia kutoka kwa mmoja wa viongozi wa dini nchini kuhusu uwazi kwenye mali ya umma.

Katika simulizi yake ambayo leo imekuwa wazo langu kuu la makala haya, kiongozi huyo anasema akiwa mwanafunzi katika moja ya shule za seminari nchini, mwanafunzi mmoja kutoka mataifa yaliyoendelea alijiunga shuleni hapo.

Katika shule nyingi, chakula kikuu ni ugali kwa maharage, chakula ambacho kiongozi huyo wa dini anahadithia kuwa kilimshinda mwanafunzi huyo wa kigeni akalazimika kutafuta namna ya kupata mchele kwa ajili ya wali.

Kupitia kwa kiongozi wa chakula, mwanafunzi huyo wa kigeni alifadhili ununuzi wa magunia matatu ya mchele kwa sharti la msaada huo kufanywa siri kati yake na uongozi wa shule. Ombi lililokubaliwa na mchele ukanunuliwa.

Anasema baada ya mchele kununuliwa, wali ulipikwa na wanafunzi waliokuwa wakihoji mabadiliko hayo ya ghafla ya ratiba ya chakula walijulishwa kuwa ni msaada kutoka kwa mfadhili asiyetaka kujulikana.

Kutokana na maelezo hayo, zogo kubwa liliibuka shuleni wanafunzi wakiweka msimamo wa kutokula hadi wamjue mfadhili wao.

Wanafunzi hao walitaka kumjua mtu aliyenunua mchele huo na kuweka masharti, walihofu kuhusu usalama na nia ya msaada wake.

“Hatutaki misaada ya masharti. Tutajuaje katoa gunia tatu lakini mawili katia sumu itakayotudhuru baadaye?” walihoji wanafunzi hao.

Kuona hivyo, uongozi wa shule haukuwa na ujanja mwingine zaidi ya kutoboa siri kwa kumtaja mfadhili ambaye kitendo hicho kilimsononesha kwa sababu hakutaka kujulikana.

Hadithi hii ndiyo imenikumbusha umuhimu wa mali ya umma kuhitaji uwazi, kama kichwa cha makala haya inavyoelezwa.

Kupitia hadithi hii, napenda kuisihi Serikali kupitia na Profesa Kabudi kuacha usiri katika masuala yanayohusu mali na fedha za umma. Watanzania ndio wamiliki wa madini na hivyo wanatakiwa kujua kila kitu kinachoyahusu.

Kisheria, fedha na mapato yote ya umma yanapangiwa matumizi na kuidhinishwa na Bunge ambalo ndicho chombo cha uwakilishi wa wananchi.

Kupitia Bunge la Bajeti, makadirio, mapato na matumizi ya Serikali hujadiliwa na kupitishwa, sasa iweje mapato hayo ya madini yawe siri. Nani atayapangia matumizi yake?

Baada ya matumizi ikiwemo malipo ya uendeshaji wa shughuli za Serikali na miradi ya maendeleo kupangwa na Bunge, matumizi ya fedha hizo hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye taarifa huwasilishwa Bunge, kupitiwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na hatimaye mjadala wa Bunge zima.

Kauli ya Profesa Kabudi kuwa Serikali haitaweka wazi malipo yatokanayo na mjadala kati yake na wawekezaji kwenye sekta ya madini inazua hofu kuwa hata matumizi yake yatakuwa siri.

Hali ikiwa hivyo, maana yake ni kwamba matumizi hayataidhinishwa na Bunge na huenda hayatakaguliwa na CAG.

Nachelea kusema kuwa kama hali ni hivyo, basi fedha hizo hazitakuwa za umma kama inavyo takiwa kuwa.

Kwa sababu naamini malipo na fedha hizo ni za umma, basi Serikali inalazimika kuyaweka wazi kwa sababu ‘mali ya umma inahitaji uwazi’

0757708277

Columnist: mwananchi.co.tz