Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Makosa ya uwanjani yanavyozigharimu timu za Afrika

9957 Goshashi+allan TZW

Mon, 25 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashabiki wa soka sehemu mbalimbali barani Afrika tulikuwa na matumaini kwamba moja ya timu zilizotuwakilisha katika Fainali za Kombe la Dunia 2014 ingeweza kufika hatua ya nusu fainali.

Hilo lilishindikana, kwani timu zilizokuwa zikituwakilisha katika fainali hizo ambazo ni Algeria, Nigeria, Ghana, Ivory Coast na Cameroon zilitolewa. Ghana, Ivory Coast na Cameroon zilitolewa katika hatua ya makundi wakati Nigeria na Algeria zilitolewa katika hatua ya 16 bora ambayo ni hatua ya mtoano.

Kwa matokeo hayo, katika fainali za Kombe la Dunia 2014, Afrika ilishindwa kuingiza timu katika hatua ya robo fainali wakati katika fainali za 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini tuliingiza timu moja katika hatua ya robo fainali ambayo ni Ghana.

Kwa kushindwa kufika hatua ya nusu fainali katika fainali za 2014 ilimaanisha ndoto ya Afrika kuweka rekodi ya kuingiza timu katika hatua ya nusu fainali imeyeyuka na historia imeendelea kuonyesha hakuna timu ya Afrika iliyowahi kufika hatua ya nusu fainali ya Fainali za Kombe la Dunia tangu zilipoanzishwa 1930.

Nalipenda bara la Afrika na nawapenda wachezaji soka wa Waafrika, lakini huwa naona kuna mambo muhimu kuhusu soka la Afrika ambayo kwa muda mrefu sasa yamekuwa hayafanyiwi kazi na hivyo kusababisha timu za Afrika kushindwa kutamba katika Fainali za Kombe la Dunia.

Ni wazi wachezaji wa Afrika wamekuwa wakicheza kwa nguvu, huku wakishindwa kutumia akili, inayotakiwa kutwaa ubingwa wa dunia au kufanya vizuri na kuhakikisha wanafikisha timu zao katika hatua ya nusu fainali ya Fainali za Kombe la Dunia.

Soka halihitaji nguvu tu, ila linahitaji akili ya juu, nadhani hii ndiyo sehemu wachezaji wa Afrika wanatakiwa kuifanyia kazi kwa kiwango cha juu ili kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Dunia, hasa hizi za 2018 zinazoendelea nchini Russia.

Najua wachezaji wa Afrika wanaweza kufanya vizuri zaidi katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 kama wakitambua umuhimu wa matumizi ya akili ya juu uwanjani, nidhamu, shauku, uamuzi na heshima.

Baadhi ya wachezaji wa Afrika wanashindwa kuzichezea timu zao za taifa kwa shauku, heshima na unyenyekevu kama wanavyozitumikia klabu zao za Ulaya kwa wale wanaocheza soka Ulaya.

Ninakumbuka katika fainali za 2014 niliona, makosa katika safu ya ulinzi kwa timu za Afrika, pia ubunifu katika kiungo na ujanja katika pasi za mwisho ulikuwa sababu kubwa kwa timu za Afrika kushindwa kutamba nchini Brazil katika Fainali za Kombe la Dunia 2014.

Timu za Afrika katika fainali hizo, pia zilishindwa kuzuia mbinu za pasi za mwisho, mipira ya kona na hata mipira ya adhabu na kuwafanya washindwe kuwa bora mbele ya timu za Ulaya na Amerika Kusini.

Suala lingine nililoliona ni wachezaji wa Afrika kukosa umakini muda wote uwanjani, wakifanya vizuri kidogo baada ya muda mfupi baadhi ya wachezaji katika timu wanapoteza umakini hivyo timu pinzani kutumia mwanya huo kupata ushindi.

Kubwa zaidi nililoliona ni wachezaji wa Afrika kufanya makosa mengi katika mechi. Sawa soka ni mchezo wa makosa, lakini makosa yaliyofanywa na wachezaji wa timu za Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia 2014 ndiyo yaliyozigharimu timu zote tano za Afrika na hivyo kuaga mapema fainali hizo.

Ni wazi timu za Afrika zinazotuwakilisha katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazoendelea ambazo ni Nigeria, Misri, Morocco, Senegal na Tunisia hazitafanya makosa yaliyotugharimu 2014.

Kikubwa kinachotakiwa ni kujipanga, kujiandaa kisaikolojia kuona kuwa wanaweza.

Ajabu ni kwamba hawa wazungu wako nao kila siku lakini linapokuja Kombe la Dunia wanawasumbua.

Columnist: mwananchi.co.tz