Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Makontena ya Makonda, siasa za vinyonga nchini

15680 Pic+makontena TanzaniaWeb

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Niko maeneo yangu ya kujidai. Sihitaji barua ya serikali za mitaa wala kitambulisho cha mpiga kura kujidhamini. Nakula na kunywa chochote kwa kusaini kama karani wa mahakama, hukumu ni mwisho wa mwezi.

Ni nyakati za jioni ubongo wangu ukiwa na akili za mchana. Kinywaji hakijapata nafasi ya kunivuruga. Bado sijaanza kuvutiwa na maumbile wala sura za wahudumu. Naangalia kila kitu kwa umakini kuliko fundi saa.

Mbele yangu kuna runinga ikionyesha taarifa ya habari. Nafuatilia baada ya kusikia habari za kampeni huko Ukonga. Mwanasiasa mmoja anawaponda wanasiasa wawili wa kike kwa kulala chumba kimoja wakiwa Dar na bungeni Dodoma.

Nashindwa kuendelea kutazama, naanza kuyatafakari maneno yake. Kajuaje kuwa wanalala chumba kimoja? Ni dhambi wasichana kulala chumba kimoja? Je, hao ni wagombea ubunge huko Ukonga? Je, hizo ndiyo sera za chama chake?

Nakosa majibu na nachoka zaidi kusikia wafuasi wake wakimshangilia kwa nguvu. Wasichana kulala chumba kimoja ndiyo majibu ya kero za wana Ukonga? Hizi siasa tumeziacha zifike hapa zilipo sisi wenyewe.

Angalau mashabiki wa Simba na Yanga wanajielewa kiasi cha kuweza kupongezana. Lakini, mashabiki wa siasa ni kama wale wa Diamond na Alikiba. Fuatilia mijadala yao siasa kuanzia mitaani mpaka mitandaoni utapata jibu.

Imefikia kwamba lolote linalofanywa na CCM hata kama lina manufaa kwa taifa, ni ngumu wafuasi wa Chadema kupongeza. Na kiongozi wa Chadema akipongeza ni kesi kubwa kwao na kumuona msaliti wa chama chao.

Pia, wafuasi wa CCM hata iweje hawaoni jema lolote kutoka Chadema au upinzani kwa ujumla wake. Ni kama mashabiki wa Diamond kutomuelewa Alikiba. Huku wafuasi wa Alikiba wakishindwa kutambua uwepo wa Diamond.

Hii leo kwenye siasa lolote likifanywa na mwanasiasa atashangiliwa na wafuasi wa chama chake. Siyo kwa sababu ni jambo lenye manufaa, hapana. Kwa sababu ni mwenzao hivyo anapongezwa tu.

Kama lilifanywa na mtu wa ngazi ya chini kichama na akashangiliwa sana na kupongezwa. Likirekebishwa au kuzuiwa na mtu wa ngazi ya juu, wale waliompongeza wa ngazi ya chini watabadili gia bila aibu na kumpongeza zaidi wa ngazi ya juu.

Sakata la Makonda

Hivi karibuni wakati kontena 20 za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda zikitakiwa kupigwa mnada kwa agizo la Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango kuna watu walimpongeza sana waziri huyo kwa msimamo wake huo.

Akaonekana kiongozi ambaye haangalii sura ya mtu. Yupo kwa ajili ya kulinda na kukusanya mapato ya Serikali kwa haki, uaminifu wenye utiifu ndani yake. Wachache wakaona kama anajitafutia matatizo kwa kugusa asiyegusika.

Walewale tena kwa kiwango kilekile wakampongeza Makonda, alipotoa ‘vitisho’ vya laana kwa atakayenunua makontena hayo akidai ni vifaa vya ofisi za walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ukiwa msaada kutoka kwa Watanzania waishio Marekani.

Akiwa mkuu wa mkoa tu, alienda mbali zaidi kwa kusema ‘hao TRA na huyo waziri wenu’ (Philip Mpango) wakitimiza wanachotaka (kupiga mnada kontena zake), angeshtaki kwa Rais John Magufuli. Walewale wakamuunga mkono tena Makonda kwa nguvu.

Waziri Mpango akapigilia msumari, kwamba kama mtu akinunua makontena atapata laana basi anatamani yeye angekuwa na pesa ili anunue yote. Watu walewale kwa umoja wao wakampongeza tena Mpango.

Ilionekana kama utani kama siyo maajabu, lakini pia kwa nyakati hizi hakikuwa kitu cha ajabu mgongano wa kauli kwa viongozi wetu. Imetokea mara kadhaa DC kufanya kazi za TRA, au RC kufanya kazi inayotakiwa kufanywa na jeshi la polisi.

Waziri wa fedha anatishwa na mkuu wa mkoa? Wapo waliodhani ni sinema inachezwa. Kumekuwa na mawazo kwamba kukiwa na jambo fulani zito, Serikali inaibua jambo la kupumbaza watu wasahau au wapuuze mengine. Ilikuwa rahisi kuhisi hivyo.

Ingawa siyo rasmi lakini ukweli ni kwamba waziri wa fedha ni mtu mzito sana. Hata kimahesabu unaweza kuanza na Rais, makamu wake, waziri mkuu kisha akafuata waziri wa fedha. Wizara ya Fedha ni roho ya nchi yoyote duniani.

Wote wateule wa rais. Lakini mmoja mipaka yake inaishia Bunju, Mbagala kama siyo Kitunda na Maramba Mawili. Mwingine mipaka yake haina mipaka ndani na nje ya nchi. Yule ni waziri wa fedha mtendaji, mwingine ni mtawala wa mkoa mmoja.

Hata kimapato binafsi, waziri anakwenda mpaka kwenye milioni ishirini kwa mwezi, mkuu wa mkoa akiishia na milioni 4.5 yake. Yule ni waziri na mbunge kwa wakati mmoja, hilo tu ni jawabu tosha kuwa yuko juu yake kwa kila kitu.

Kisheria waziri wa fedha ndiye mwenye idhini ya kupokea au kusaini misaada kutoka nje na siyo mkuu wa mkoa wala waziri mwingine. Hilo Makonda na watu wake wa karibu hawakugundua au kujua au walipuuza.

Hakuna msaada wa namna ile ukaja kwa jina la mtu binafsi. Makontena yamekuja kwa jina la Makonda, mwenye jina la Makonda anakana kuwa siyo makontena ya Makonda, bali ya waalimu wa mkoa wa Makonda. Kontena zingeingia kwa jina la ofisi siyo mtu binafsi.

Yawezekana kweli ni vifaa lengwa kwa ajili ya ofisi za waalimu. Lakini kutaka sifa ziende kwake bila figisu, Makonda akaamuru liandikwe jina lake badala ya ofisi zinazopewa msaada husika. Kijana alitaka shavu lake kwa uhakika.

Ama pengine ni kujiamini kwake kulikopitiliza kwa kuwa ni kipenzi cha Rais Magufuli kutokana na utendaji wake wa kazi. Lakini anasahau kuwa hata Waziri Mpango, ni kipenzi cha Rais kwa utendaji kazi wake.

Wakati Makonda akiteuliwa kutoka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mpaka RC Dar es Salaam, Waziri Mpango ndani ya mwezi mmoja alipandishwa kutoka Naibu Kamishna kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, kisha Waziri wa Fedha. Nani kipenzi zaidi cha Rais hapo?

Huu ni mwaka wa tatu Waziri Mpango anasimamia bajeti ya Serikali ya Rais Magufuli. Yeye ndiye injini ya mambo yote ya bajeti ya uendeshaji wa Serikali ya awamu ya tano. Siyo mtu mdogo au wa kukurupuka tu kwenye maamuzi kama hayo.

Makonda alikuwa na nafasi kubwa ya kuongea na waziri na mambo yasingefikia hapa. Na Rais asingetoa maelezo juu ya sakata hilo si ajabu Makonda angeendelea kutikisana na waziri. Makonda hakusoma alama za nyakati.

Rais Magufuli siku zote anapenda kutumia neno kwa mujibu wa sheria anapoelezea jambo. Sakata hili amelimaliza kwa maelezo ambayo ni ya kwa mujibu wa sheria. Walewale waliomshangilia Makonda kisha Waziri Mpango, ndiyo walioshangilia zaidi ufafanuzi wa Rais.

Bado tutaendelea kuwa wajinga mpaka pale tutakapopata mwalimu wa kutufundisha tukapata akili. Kwa sasa bado sana maana mwalimu wetu hata hajamaliza chuo ili aje sasa kutusomesha. Ndiyo maana tunashangilia kila kitu bila kuhoji wala kudadisi.

Sasa hapa wengi wetu ndio mwisho wetu, hatutaki kuingia ndani zaidi kwa kuunganisha ‘doti’ juu ya mnada wenyewe wa makontena hayo. Kivipi unashindikana kwa mara ya pili? Tunasubiri wengine wafikirie kwa niaba yetu.

Sababu kubwa ni watu kutofika bei elekezi kutoka TRA. Kwanini hawafiki bei? Kuna uwezekano TRA wamekurupuka kukadiria kodi isiyoendana na thamani halisi ya mzigo uliopo kwenye makontena?

Waziri alikurupuka bila kutathmini mzigo na kiasi cha fedha kilichotajwa kama kilivyo? Hapa kuna mambo mengi ya kutafakari. Lakini sisi wafuasi tumeamua kufanya kazi moja rahisi sana, kushangilia matamko ya viongozi wetu.

Columnist: mwananchi.co.tz