Mapema mwaka 2016, Rais John Magufuli akiwa hajafanya uteuzi wake wa wakuu wa mikoa tangu alipoingia madarakani Novemba 5, 2015, alimsifia Paul Makonda kwa utendaji kazi mzuri. Wakati huo Makonda alikuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Akasema: “Mtu kama huyo akipanda cheo mtasema anapendelewa?”
Machi 2016, Rais Magufuli alipoteua wakuu wa mikoa jina la Makonda lilikuwa kati ya yaliyokolezwa wino.
Kijana mdogo, ambaye hakuwa na uzoefu mkubwa kiuongozi, aliteuliwa kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam. Jiji lenye kuongoza uchumi wa nchi.
Hata hivyo, hakukuwa na kushangaa sana. Nyota njema huonekana asubuhi. Na dalili ya mvua ni mawingu. Sifa ambazo Rais Magufuli alimpa zilishabeba matarajio chanya upande wake.
Miaka mitatu na miezi sita imeshakatika. Makonda bado mkuu wa mkoa wa Dar as Salaam. Watu hawaulizani tena kuhusu kulimudu jiji au kushindwa kama ambavyo swali liliulizwa wakati anateuliwa. Lugha imebadilika.
Ndani ya miaka mitatu ya ukuu wake imeshuhudia wengi wakiondolewa au kuhamishwa. Wengi mno. Wengine wazoefu na wasomi wa kiwango cha juu. Makonda yupo.
Pia Soma
- Kigogo wa ‘Twita’ na Mange ni Sunche na Kapeto
- Mwanamke Uganda ahukumiwa kifungo kwa kumlisha mtoto hedhi
- 292 waumwa na mbwa wilaya ya Ulanga, Malinyi 2019
Wakati huu, inaonekana Tanzania imekuwa na presha kubwa ya kiuongozi kwa sababu Rais Magufuli ameshika kitovu cha utawala, anatikisa ili kila mtu serikalini awajibike kwa kiwango anachotaka kuona.
Bila shaka presha ya Dar imeongezeka kuliko wakati wa Yusuf Makamba, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, William Lukuvi, Abbas Kandoro, Said Sadiki na wengine wote.
Pamoja na presha hiyo, Makonda yupo. Si kwamba anatembea ardhi tambarare, hapana. Anapanda milima, anashuka mabonde. Hakuna kiongozi ndani ya Serikali ya Magufuli, aliyeandamwa na anaendelea kusakamwa kama Makonda, lakini anaendelea kuwapo. Mwishoni mwa mwaka 2016, Makonda alionywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu utendaji wake. Akamwambia ajirekebishe awe na vitendo kuliko maneno.
Siku chache baadaye, Rais Magufuli alimpigia simu Makonda akampongeza kwa utendaji, pale alipokuwa anazungukia vitongoji Dar kusikiliza kero za wananchi. Rais alipenda alichofanya. Alimpigia akiwa katikati ya mkutano na wananchi.
Januari 2017, Makonda alianza vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya. Namna alivyoiendesha aliibua manung’uniko mengi. Wengi walipinga. Wasomi wazoefu wa masuala ya upelelezi na ukamataji, akiwamo aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Adadi Rajab, walikosoa.
Makonda alikuwa na mtu aliyemtia moyo aendelee. Sakata la dawa za kulevya kabla halijaisha, liliibuka la tuhuma za kuvamia ofisi za Clouds TV na kulazimisha kurushwa hewani kwa maudhui yaliyokataliwa na uongozi wa kituo hicho.
Watabiri na wabashiri wengi wakajipa uhakika kuwa Makonda angeng’oka lakini Rais Magufuli akamtoa wasiwasi, akamwambia afanye kazi, maana yeye hapangiwi mtu wa kuteua au wa kuondoa.
Nape Nnauye, akiwa waziri wa habari alipotaka haki itendeke kwa Makonda, alijikuta anang’oka yeye.
Rais anamlea Makonda na hataki aguswe? Jibu ni hapana. Mwaka jana Rais Magufuli alikuwa mbogo katika mzozo wa samani zilizodaiwa kuwa za msaada kwa walimu, ambazo Makonda alitaka zipite bandarini bila kulipiwa ushuru wakati zimeandikwa jina lake. Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango alizuia.
Kile ambacho Rais Magufuli alikisema kuhusu samani hizo, hadi kujenga shaka kuwa pengine ulikuwa mkakati wa kukwepa kodi, kilifanya watabiri na wabashiri kuamini kwamba zamu ya Makonda kung’oka ilikuwa imewadia.
Ikaja awamu ya Dk Bashiru Ally, katibu mkuu wa CCM kumweleza wazi Makonda kwa kukosa uwezo wa kuongoza. Bashiru ameeleza kuwa sababu ya makosa kadhaa ya Makonda ni kukosa mafunzo ya uongozi.
Bashiru alifika mbali na kutangaza kuwa Makonda pamoja na Albert Chalamila, mkuu wa Mkoa wa Mbeya watakuwa viongozi wa kwanza mwakani kurudishwa chuo kusoma uongozi.
Nyakati zote za mashambulizi, mitandaoni na vyombo vya habari. Shutuma anazotupiwa kutoka ndani ya viongozi wa chama chake mpaka wapinzani, Makonda amekuwa kama mti mbichi, nyakati za upepo mkali, unainama mpaka unaweza kudhani umekatika, upepo ukiacha, mti hurejea wima.
Hata sasa, Rais Magufuli kwa mara nyingine ameibuka na kumsema Makonda hadharani. Ni kuhusu utendaji wake. Amemgusa waziwazi kuwa humfanyia maonyesho kwa kutembelea sehemu zenye kero lakini baada ya kuondoka hali hubaki vilevile.
Kamgusa kwenye machinjio ya Vingunguti, akambagaza katika mradi wa uendelezaji wa ufukwe wa Coco, Oysterbay, Dar. Ni kipindi ambacho watabiri na wabashiri walimtangulia Rais Magufuli na uamuzi wake. Wakadhani kijana wake anang’oka. Lakini bado yupo.
Ubakiaji wake si sawa na ule wa Cleander, kijana pendwa wa aliyekuwa Mfalme wa Roma, Karne ya pili, Commodus. Cleander, mtumwa aliyeuzwa Roma kutoka Uturuki, alipendwa na Commodus, akamfanya msaidizi wake.
Cleander kwa kujiona ni kijana pendwa wa mfalme, akaota meno ya juu. Akafanya mengi ya hovyo mpaka kuharibu heshima ya utawala. Waroma walichukizwa, lakini Commodus alimlinda Cleander kwa kila ovu.
Rais Magufuli hafanyi kama Commodus kumlimda Makonda, wala Makonda si Cleander. Rais Magufuli huuona upungufu wa kijana wake na kumsema waziwazi, ila ameendelea kudumu ofisini.
Kwa kumbukumbu ya waliotumbuliwa na Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani, kwamba kosa moja ni kuwekwa pembeni. Unaweza kutafsiri kuwa Makonda ni mwenye bahati kubwa.