Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Magufuli amerusha jiwe, limenipata

33066 Jpm+pic Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimeona niandike makala hii siku ya leo ili kusaidia kujibu swali la Dk John Magufuli, Rais wa Tanzania, aliloliuliza wakati akizindua mradi wa ujenzi wa barabara 8 – 12 ambazo zinaanzia Ubungo hadi Chalinze. Nimevutiwa kujaribu kujibu swali hili kwa sababu nimependa aina ya swali aliloliuliza Rais JPM huku nikiamini majibu yake ni ufafanuzi mrefu unaoweza kujaza kurasa za vitabu.

JPM ameuliza swali hili akilinasibisha na hali ya sasa ya nchi ambapo Serikali yake imejijengea uwezo mkubwa wa kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo. Ni majuzi tu mradi wa matrilioni ya fedha umezinduliwa, ambao utawezesha taifa lipate umeme wa megawati 2100 pale Stiglers Gorge. Desemba 20, Rais JPM alizindua mradi mwingine wa ujenzi wa barabara ya baharini ya zaidi ya kilomita saba ambayo itakuwa inaelekea mjini.

Desemba 21, 2018 alielekeza Serikali itoe Sh7.7 bilioni kwa ajili ya kusimamia shughuli za ujenzi wa nyumba za askari wa Jeshi la Polisi. Leo tunajua kuwa JPM ataliongoza taifa kupokea ndege mpya aina ya AirBus 220 – 300 ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za Serikali ya awamu ya tano kufufua sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania. Ni majuzi tu Serikali ilifanya uamuzi mwingine mkubwa wa kuokoa hasara kwa wakulima halisi wa zao la korosho kwa kuamua kuzinunua korosho na kuziwekea utaratibu ambao utafanya ziuzwe chini ya usimamizi wa Serikali kwa maana ya kuwalinda wakulima.

Uhalisia wa Hoja ya JPM

Hoja ya JPM iko wazi na dhahiri, anawazindua Watanzania wajiulize kwa nini Serikali yake ina uwezo wa kusimamia masuala yote haya ndani ya miaka mitatu, na anataka tutafakari zaidi kwa nini hivi sasa miradi mikubwa inasimamiwa kwa kasi zaidi kuliko ilivyokuwa huko zamani. JPM anataka tujiulize fedha yeye anazitoa wapi na zamani zilikuwa wapi. Kwa ujumla anatuhitimishia kuhusu kodi, kwamba kodi zimekusanywa tangu nchi yetu inapata uhuru, kwa nini kodi hizo hazikuanza kusimamia miradi hiyo tangu zamani.

Swali kuu la JPM ni swali halisi ambalo Watanzania wamejiuliza kwa miongo kadhaa, Watanzania wamekuwa wakililalamikia sana, kwamba kodi zao zinakwenda wapi? Mbona wanalipa kodi lakini tija yake ni ndogo sana, mbona serikali haiwawekei miundombinu ya kuendelea kujenga uchumi na maisha yao kiasi kwamba hawaelewi kwa nini wanalipishwa kodi? Maswali haya ya wananchi nayo ni halisi sana, halisi kwa maana ya uwepo wake.

Tunaweza kulijibu swali la JPM

Ndiyo, ni rahisi sana kulijibu. Kwa mtizamo wangu na hasa nimekuwa nikiandika sana kuhusu masuala haya. Serikali yoyote inayoweza kusimamia miradi mikubwa na ya kihistoria ya maendeleo ni Serikali inayokusanya kodi kweli kweli na kisha inazitumia kodi hizo ipasavyo, kwanza kwa kubana matumizi na pili kwa kuelekeza fedha kwenye maeneo ambayo yatasababisha au kuongeza kasi ya ufanyikaji wa shughuli ambazo zinakuza uchumi kwa haraka, na tatu kwa kuacha kabisa kutumia fedha za umma kwa masuala yasiyokuwa kipaumbele au msingi kwa taifa.

Tangu JPM ameingia madarakani aliweka wazi msimamo wa Serikali yake juu ya masuala ya ukusanyaji kodi, kupambana na rushwa na ufisadi, kuondoa matumizi hewa na ubadhirifu ndani ya Serikali na mengineyo. Kwa mfano, wakati JPM analihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, alieleza kiwango cha mabilioni ya fedha ambacho kilikuwa kimetumika kusafirisha watu mbalimbali kwenda nje ya nchi kwa miaka mitano ya mwisho ya Serikali ya awamu ya nne. JPM alisisitiza kuwa Serikali yake inaachana kwa kiasi kikubwa na kushangilia hali ya fedha nyingi za Serikali kutumika kusafirisha watumishi wa Serikali na viongozi kwenda nje ya nchi katika misafara mikubwa bila kujali kuwa safari hizo zinaweza kupunguzwa na fedha za Serikali zikaokolewa.

Kusema ni jambo moja, kutenda ni jambo lingine

Serikali nyingi za Afrika zinashindwa kufikia malengo yake kwa sababu ya kasumba ya kusema hivi na kutekeleza vile. Kinachofanya JPM anatusuta kuhusu kodi zetu za zamani na za sasa ni ukweli kuwa Serikali yake imeweza kwa kiasi kikubwa kutimiza masuala ambayo iliyaahidi, panaweza kuwa na mapungufu ya hapa na pale lakini kwa kweli ndani ya miaka mitatu mambo makubwa sana yamefanyika.

Kwa hiyo, kasumba ya JPM ya kusema jambo hili na kutenda jambo hili ndiko kumemfikisha hapa, na ndiko kumelifikisha hapa taifa. Serikali ya CCM chini yake iliahidi kutoa elimu bure kwa ngazi ya shule za msingi, jambo hilo linafanyika tangu mwaka wa kwanza akiwa madarakani.

Aliahidi kupambana na rushwa na ufisadi, sote tunakubaliana kuwa mafisadi na wala rushwa wakubwa wanatafutana. Aliahidi kupunguza kabisa masuala ya safari za nje ya nchi ambazo zitaikwangua hazina, na kweli sote tunaona yeye ndiye wa kwanza kusimamia ahadi hiyo, safari zake nyingi ambazo angelibeba misafara ya walinzi wengi na wafanyakazi lukuki anamtuma Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje na wengineo. Ni viongozi wachache sana barani Afrika wanaweza kusema na kutenda jambo lilelile walilosema, viongozi wengi wanaongea sana na wanatenda kinyume.

Wakati Serikali ya JPM inakusanya zaidi ya Sh1.3 trilioni kwa mwezi, sehemu kubwa ya fedha hizo haziishi mifukoni mwa watu, zinaenda kutatua shida za umeme, maji, barabara, afya na mengineyo. Katika vijiji vingi nilivyozunguka, wananchi wanaanza kuona tofauti ya maamuzi ya kisiasa yenye tija dhidi ya yale ya kuwanufaisha viongozi.

Zamani kodi zilikusanywa, zikaliwa kabla ya kufika hazina, leo kodi zinakusanywa zinanunua ndege, zinajenga barabara, zinaleta umeme, zinashughulikia elimu, zinatatua changamoto za afya na kadhalika. Leo taifa letu linaweza kuthubutu kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo kwa sababu tuna uongozi unaothubutu, tuna kiongozi anayethubutu, mwaminifu na mwadilifu.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtaalamu Mshauri wa Miradi, Utawala na Sera na ni Mtafiti, Mfasiri, na Mwanasheria, . Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])



Columnist: mwananchi.co.tz