Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Magufuli amechora mstari sahihi wa kumpima 2020

89905 Magufulipic Magufuli amechora mstari sahihi wa kumpima 2020

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwaka mmoja umesalia kwa Rais John Magufuli kurudi kwa wananchi kuwauliza “niendelee au nisiendelee?”

Kupitia Ilani ya uchaguzi, kama ilivyokuwa kwa vyama vingine, CCM iliahidi mambo kadhaa ambayo itayatekeleza kwa kipindi cha miaka mitano.

Watanzania nao wameanza kutayarisha kalamu zao kwa ajili ya kuhakiki ahadi za CCM ambayo ilimtuma Magufuli kuzisimamia.

Kwa kuangalia historia ya nyuma, ilikuwa vigumu kuamini kuwaCCM itakuwa chini ya Magufuli ingeweza kutekeleza iliyoyaahidi kutokana na mnyukano wa uteuzi wa mgombea ndani ya CCM.

Katika makala yangu moja niliwahi kuzungumzia viashiria vya Magufuri na CCM kutimiza asilimia kubwa ya ahadi zake tofauti na miaka iliyopita.

Niliifananisha ilani ya uchaguzi ya CCM na mpango mkakati wa biashara wa shirika kwa wadau wake, ambao utapimwa mwaka 2020 ili kuhakikisha kuwa “hatujaingizwa chaka”.

Leo mwaka mmoja kabla ya kujieleza kwa wananchi nini kuhusu walichofanya na nini watafanya katika miaka mingine mitano, nayaangalia baadhi ya mafanikio kama ifuatavyo:

Umoja wa CCM

Si rahisi kuizungumzia Serikali ya awamu ya tano bila kuitaja CCM, ambayo iliyotupatia Magufuli na kuhakikisha anashinda.

Mojawapo ya mafanikio ya Magufuli ni pamoja na kuhakiksha CCM inaendelea kuwa moja. Kama kungekuwa na mpasuko ndani ya CCM, tusingezungumzia mafanikio zaidi ya vikao vya kusutana na kukosoana miongoni mwa makundi ya kimaslahi. Magufuli amefanya juhudi kuhakikisha CCM inabaki moja na yenye nguvu.

Hali ilionekana tete sana baada ya minyukano na rabsha za uteuzi wa mgombea wa CCM. Wapiga ramli walikuwa wakibashiri na kumwona Magufuli akielemewa na mzigo aliopewa kutokana na minyukano na rabsha hizo.

Lakini dua la kuku halikumpata mwewe na CCM imeendelea kuwa moja na kuhakikisha Magufuli anaungwa mkono ili atimize ahadi zake kwa wananchi.

Tumeshuhudia akiingalia zaidi CCM ya siku zijazo kwa kutoa kipaumbele kwa vijana na akinamama katika uteuzi wa nafasi za uongozi serikalini na ndani ya chama. Haya ni mafanikio si tu kwa CCM bali kwa Taifa.

Ameweka wanataaluma wa siasa katika nafasi nyeti za uongozi ndani ya CCM nafikiri kwa kutaka kuipa CCM uhalisia wa chama cha siasa kulingana na mazingira ya leo na kupunguza ubabaishaji.

Ujenzi wa miundombinu

Tunamkumbuka Magufuli kama kinara wa ujenzi wa miundombinu, hasa barabara, akiwa waziri katika Serikali zilizopita. Katika miaka yake minne aliyokaa madarakani, tumeshuhudia ujenzi wa barabara katika maeneo tofauti zikiwemo za mitaa, mijini, wilaya, mikoa, na kitaifa.

Tukiliangalia Jiji la Dar es Salaam kama mfano wa jinsi ujenzi wa barabara za mitaani, ni wazi Rais Magufuli atapata alama za kutosha kwa hili. Barabara ambazo zilihukumiwa miaka mingi iliyopita kuwa hazistahili kuwa nzuri, tumeshuhudia zikitengenezwa kiwango cha lami. Sina haja ya kuzungumzia barabara kuu zinazounganisha mikoa na nchi za jirani, hili liko wazi.

Tumeona maamuzi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo inaelekea kufika Morogoro na matarajio yakiwa ni kufika Mwanza na Kigoma. Dhamira yake ya kuona Tanzania inaunganishwa na reli na masoko ya Rwanda, Burundi, Uganda na DRC iko wazi na ina uhalisia.

Pamoja na SGR, ukarabati wa reli ya kati na ile ya Kilimanjaro, Tanga, na Arusha unaendela.

Rais Magufuli na CCM waliahidi kuifufua ATCL. Pamoja na kejeli zilizotolewa mara baada ya ndege mbili za kwanza kuwasili, aliendelea kutimiza azima yake. Mara ikaja Boeing Dreamliner, Airbus mbili na nyinginezo.

Suala la muhimu hapa ni jinsi Magufuli alivyotuhakikishia kuwa atanunua ndege na kuijenga ATCL kwa pesa yetu ya ndani. Tuliguna na kukejeli,mmaana tulizoeshwa na kuaminishwa kuwa pesa ya ndani ni kiduchu sana kuweza kugharamia miradi mikubwa.

Kumbe pesa zilikuwapo la zilikuwa zinahudumia safari zisizo za lazima na ubadhirifu; na kodi ilikuwa ikikusanywa kidogo kutokana na uhalalishaji wa ukwepaji kodi na rushwa.

Tumeona alivyolifungi kibwebwe suala la ujenzi wa miundombinu ya maji. Tunakumbuka huku ndiko kulikuwa ni chaka la wapigaji wa fedha za miradi. Amelifumua chaka hili na kuhakikisha kila senti inatumika kama ilivyotarajiwa na kufikia malengo yaliyopangwa.

Si tu kuwa kafanikiwa kuleta tija, bali tumeona matokeo ya juhudi zake. Majiji, miji, na vijiji sasa zinanufaika na maji kutokana na kukamilika kwa miradi ambayo wapigaji walihakikisha haikamiliki au inakamilikia bila kutoa maji.

Swala la miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa umeme lilikuwa ni mojawapo ya komedi za nchi hii. Tulipigwa pesa, tuliibiwa, tulidanganywa, tulikatiwa umeme kama wanavyotaka, yaani tulikuwa kichekesho. Leo umeme umekuwapo na hakuna mgawo. Nguzo zinatoka Iringa na kuuzwa kwa Tanesco moja kwa moja badala ya kwenda kwanza Afrika Kusini.

Wakala wa Umeme Vijijini wanachanja mbunga kuhakikisha Tanzania yote inakuwa na mwanga na nishati ya umeme kwa matumizi ya maendeleo. Ametafuta suluhisho la kudumu la upatikananji wa umeme nchini kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Stigler’s Gorge.

Huduma za afya, elimu

Naikumbuka Tanzania ya wananfunzi kukaa chini na wagonjwa kukosa dawa, vifaa tiba, na vitanda na kuishia kulala chini.

Magufuli alianza na kasi kubwa kutatua matatizo haya sugu kwa umma na ameendelea nayo.

Tunakumbuka swala la vitanda na x-ray za Muhimbili. Leo tunajionea jinsi vituo vya afya, zahanati na hospitali za wilaya zinavyojengwa na kufunguliwa. Lengo ni kuwa na kituo cha afya kila kata.

Madini

Kama kuna eneo ambalo watanzania wa kizazi hiki na vingine vijavyo watamkumbuka na kumshukuru Magufuli ni hili la mabadiliko katika sekta ya madini. Tulikosa umiliki wa madini yetu na kuonekana kama walinzi wa mali za wageni. Madini yalikuwa si halali ya Watanzania pamoja na kuwa ni ridhiki yetu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hakuna aliyejali hilo na ilionekana kama vibarua wa waheshimiwa wa nje kwa jina la wawekezaji. Walitudanganya kama mazuzu kuwa wanasafirisha makinikikia yasiyo na thamani kwa mamia ya makontena huku tukiwa tumeziba midomo na kuwaangalia tu.

Mwandishi ni Mbunge wa Viti maalumu (CCM).

Columnist: mwananchi.co.tz