Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Magari yanapopewa kipaumbele kuliko kugharimia elimu

48672 Magaripic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mjadala wa ubora wa elimu umekuwa ukiwagusa watu wengi wakiwamo marais wastaafu wawili.

Novemba 11, 2017, Rais wa Serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya kuutafakari upya mfumo wa elimu na kushauri kuanzishwa kwa mjadala utakajumuisha makundi mbalimbali.

Alitoa kauli hiyo katika kongamano la wanataaluma lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Aprili 18, 2018, Rais aliyemfuatia Jakaya Kikwete akagusia suala hilo alipokuwa akizungumza katika kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Havard cha nchini Marekani.

Wakati Watanzania wakiwa na shauku ya lini mjadala huo utafanyika na nini kiwe ajenda, mhadhiri mwandamizi kutoka Shule kuu ya elimu ya Chuo Kiku cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa amefanya mahojiano maalumu na Mwananchi ambapo pamoja na mambo mengineyo amesema kinachokwaza sekta ya elimu ni matumizi ya fedha za elimu yasiyozingatia vipaumbele.

Licha ya Serikali kujitahidi kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti za hivi karibuni, Dk Kahangwa aliyebobea kwenye menejimenti na sera za elimu, anasema kiasi kikubwa hakiwafikii walengwa huku kukiwa na matumizi yasiyo na ulazima ikiwamo ununuzi wa magari ya kifahari.

Kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018/19, jumla ya Sh 1.4 trilioni ziliombwa na wizara, huku zaidi ya Sh 476.5 bilioni zikitengwa kwa ajili ya shughuli za kawaida za wizara.

‘’Unakuta fedha zinakwenda ngazi za juu ambazo ni za kiutawala kuliko kwenda shuleni. Ukiangalia matumizi ya wizara au matumizi ya halmashauri yanayokwenda kwenye sekta ya elimu, ni makubwa lakini yanaishia kwenye matumizi ya viongozi na magari yao,’’ alisema na kuongeza:

“Ni bora Waziri asiwe na usafiri kuliko kuwa na shule isiyo na vifaa, kwa sababu yeye akiwa na usafiri halafu kule chini watoto hawasomi hayo ni matatizo.”

Dk Kahangwa anasema ili bajeti hiyo ikidhi mahitaji inatakiwa zaidi ya asilimia 50 itumike kuwekeza kwenye miundombinu, walimu na vifaa vya kufundishia.

Anasema kwa sasa kiwango hicho kinachukuliwa na wasimamizi wa elimu, kuanzia maofisa elimu wa wilaya, mkoa, mawaziri, makaatibu wakuu na wakurugenzi.

Akitoa mfano wa nchi zilizoendelea, ansema viongozi wa nchi hizo hawana maisha ya anasa na wamewekeza zaidi kwenye ubora wa elimu.

“Kwa nini Waziri ahitaji gari aina ya VX kutoka nyumbani kwake pale Dodoma kila siku kwenda ofisini wakati angeweza kutumia gari la kawaida tu?

“Haya ni magari yenye matumizi makubwa, yaani gharama za kuyatunza ni kubwa mno na siyo waziri tu anayetumia; kuna naibu waziri, katibu mkuu, naibu katibu mkuu, makamishna na wakurugenzi wote,” anasema.

Akitaja changamoto zinazoambatana na udogo wa bajeti katika sekta ya elimu, Dk Kahangwa anasema ni pamoja na uhaba wa walimu na waliopo kutokuwa na ubora unaotakiwa.

“Inafahamika kwa miaka mingi tumekuwa tukiwatayarisha walimu kwa kuangalia, kwa mfano wale wanaomaliza kidato cha nne na kingine katika ualimu ni wale waliokosa kwenda pengine. Maana yake ualimu ni kazi isiyo na mvuto kwa vijana. Hakuna ambaye angependa kuwa mwalimu kwa sababu ya masilahi na uzito wa kazi ulivyo,” anasema.

Hali ya elimu ya juu

Ufinyu wa bajeti kwa mujibu wa Dk Kahangwa unaiathiri pia elimu ya juu aanayosema kwa sasa hata muda wa kuwatayarisha wanafunzi umepunguzwa.

“Hata ukija kwenye ngazi za juu kwa sisi tunaofundisha walimu wa shahada ya kwanza; siku za nyuma tulikuwa tunawafundisha kwa miaka minne lakini kwa sababu ya kubana matumizi tukajikuta tunalazimika kushusha kwa miaka mitatu,” anasema.

Kibaya zaidi anasema hata wamalizapo mafunzo wengi hawaajiriwi kwa wakati jambo linalowakatisha tamaa zaidi.

Uhaba wa walimu

Kuhusu utoshelevu wa walimu, alisema licha ya viwango vinavyotakiwa kitaaluma kwa mwalimu mmoja ni kufundisha kati ya wanafunzi 40 hadi 45, lakini hali ni tofauti nchini .

“Tumekuwa tukitembea mikoani unaweza kukuta darasa lina wanafunzi 200 mpaka 300, kiasi kwamba sasa lile siyo darasa tena bali ni mkutano. Hata kumwelekeza mwanafunzi aelewe inakuwa shida,” alisema.

Alisema kutokana na mlundikano huo idadi kubwa ya wanafunzi hasa wenye uelewa mdogo, wamekuwa wakifeli mtihani kwa kutoelewa masomo.

“Hata zile mbinu shirikishi huwezi kuzitumia, badala yake mwalimu anafundisha kupitia mhadhara kama chuo kikuu,” alisema.

Alitaja pia changamoto wa mtalaa wa elimu kutoelekeza ufundishwaji wa ukuzaji wa vipaji vya wanafunzi, badala yake alisema elimu imejielekeza zaidi kwenye nadharia zaidi na ndiyo maana hata maswali ya mitihani inauliza mwanafunzi kujua anakumbuka nini.

“Elimu yetu ingelenga kumjengea mtu stadi mbalimbali na kukuza vipaji vyake. Sasa elimu ya kukuza vipaji na stadi za kazi bado hatujaelekea huko,” alisema.

Akizungumzia suluhisho la elimu, Dk Kahangwa amesema ni lazima walimu wa shahada ya kwanza wakamilishe kozi kwa kusoma hadi mwaka wanne ili waive vizuri.

“Mwaka wa nne ndiyo utakuwa wa vitendo na itasaidia pia kupunguza uhaba wa walimu kuliko walimu kumaliza mapema halafu wanakaa muda mrefu bila kuajiriwa,’’ alisema.



Columnist: mwananchi.co.tz