Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Maendeleo ni kodi zetu si hisani ya chama

9518 Pic+chama TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati ninaandika mada hii nimepata taarifa kwamba mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Kheri James ameomba radhi kutokana na kauli zake zilizoibua mjadala mkali kuanzia wiki iliyopita.

Kwa waliomsikiliza au kumtazama, video iliyorekodiwa katika mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Bagara mkoani Manyara, Nicodemus Tlaghasi, inaonyesha James alitoa kauli yake kwa kujiamini sana.

“Ngojeni niwaambie ukweli. Nchi hii hakuna maendeleo bila CCM kuamua. Sisi tukiamua yanakuja na tukiamua hayaji na cha kutufanya hakipo, eeeh,” alisema Kheri James.

Hata hivyo, licha ya kufafanua hoja yake akisema Serikali kupitia Ilani ya CCM ndiyo inapewa dhamana na ikatoa ahadi ya kutekeleza iliyoyaahidi kwa Watanzania, nukuu hiyo ina sentensi zilizoibua maswali.

Sentensi ya kwanza ni kwamba nchi hii hakuna maendeleo bila CCM kuamua. Sentensi ya pili ni kwamba CCM ikiamua maendeleo yanakuja na ikiamua hayaji. Sentensi ya tatu ni kwamba CCM isipoleta maendeleo, Watanzania hawana uwezo wa kukuchukua hatua yoyote .

Ni kauli nzito sana licha ya kwamba zote zinazunguka kwenye ukweli uliokuwa hauzungumzwi ama kwa busara au kwa kutotaka wananchi wengi walifahamu hili kutokana na athari zake. Kwa ufafanuzi, James ametoa ya uvunguni na ndiyo maana hakuna kalipio au onyo lolote lilitolewa dhidi yake na chama au Serikali.

Ukweli wake ni kwamba, suala la maendeleo siyo hisani. Watanzania hawatakiwi kupiga magoti kuomba maendeleo wanayoyataka kupitia bajeti inayotokana na kodi zao. Pili, wanasiasa wanatakiwa kufahamu kwamba, kuwapelekea wananchi miradi ya maendeleo siyo mbadala wa kura wanazoziomba bali ni jukumu la lazima la Serikali.

James anatakiwa kufahamu kwamba, CCM inatakiwa kujipima kwa Watanzania katika dhamana ya kuongoza Serikali kwa namna inavyowaongoza. Ni wapi CCM imewatoa na inawapeleka wapi kwa kukusanya na kutumia kodi zao. Je, kodi zao zinatumika ipasavyo? CCM ndiyo inatakiwa ijitetee kwa Watanzania kama alivyofanya Katibu Mkuu mstaafu, Abdulrahman Kinana na kikosi chake kabla ya uchaguzi wa 2015.

Kilichonishangaza kwa James bila kuhofia mbele ya hadhara anasema tangu Tlaghasi alipoanza kuongoza kata hiyo chini ya Chadema, Serikali haikuwahi kupeleka maendeleo kwa sababu wananchi wake walikataa kuichagua kwenye uchaguzi wa 2015.

Tlaghasi alikuwa diwani kata hiyo kwa tiketi ya Chademu kabla ya kujiuzulu na kuhamia CCM, ambako amepewa tena fursa ya kugombea.

Hii inamaanisha kwamba, Serikali ya CCM isipeleke fedha za miradi ya maendeleo katika kata na majimbo 69 yanayoongozwa na wabunge wa upinzani kwa sababu wananchi wake hawakuichagua katika uchaguzi wa 2015.

Kwamba, kundi la Watanzania milioni sita lililotoa kura kwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa halitakiwi kushiriki maendeleo ya serikali ya CCM kwa mujibu wa kauli ya James, jambo ambalo limekuwa likikemewa sana na Rais John Magufuli akisema maendeleo hayana vyama.

Kwamba, wananchi wasichague viongozi wa upinzani kwa kuwa serikali ya CCM ndiyo inakusanya kodi na kupeleka fedha hizo popote inakoona panafaa kwa maslahi ya kundi la Watanzania waliowachagua. Hii siyo sahihi hasa kwa kuwa CCM yenyewe ilikubaliana na mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992.

Kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tano, viongozi wake wote wamekuwa wakishirikiana na vyama vya upinzani. James na wengine wanaofikiri kama yeye wanatakiwa kujifunza busara ya viongozi waliowatangulia.

Baadhi ya wachambuzi wa duru za kisiasa niliozungumza nao baadhi wanasema msingi wa kauli ya James unachagizwa na mambo manne ambayo ni uchanga katika siasa, ulevi wa madaraka, malezi duni ya uongozi ndani ya CCM pamoja na presha ya ushindani wa chaguzi hizi za ‘msimu’.

Hoja ya kiburi cha madaraka haileti afya katika siasa safi na utamaduni uliojengwa na waasisi wa taifa hili.

Athari na tahadhari

Kauli ya mwanasiasa huyo inajirudia, wengi wakidhani ukichagua CCM pekee ndio maendeleo yanakuja.

Athari zake ni kupandikiza makundi makubwa mawili yanayowarudisha Watanzania kwenye maumivu ya uchaguzi wa 2015.

Athari nyingine inaweza kujenga chuki dhidi ya Serikali licha ya kuwa na dhamira njema kwa Watanzania wote bila kuwabagua. Kuna baadhi ya majimbo ya upinzani yenye changamoto za muda mrefu au kukwama kwa miradi ya maendeleo, watajisikia kwamba wanabaguliwa na serikali ya CCM.

Kisiasa ni kauli ambayo haiwezi kuwa karata nzuri ya kujenga ushawishi wa kukubalika kwa CCM bali kutengeneza majeraha zaidi kwa siku za usoni. Kinachotakiwa ni CCM kukemea kauli za aina hii kwa wanachama na viongozi wake wanaotoa matamko na kauli zinazoweza kutia dosari juhudi za Rais Magufuli.

0716186074

Columnist: mwananchi.co.tz