Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mabindo, mwanafunzi mzee anayetetea wasiojua kusoma

Mabindo, mwanafunzi mzee anayetetea wasiojua kusoma

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Napenda kuwa mwanaharakati ili niweze kuwatetea watu wasiojua kusoma na kuandika kwani wanadhulumiwa haki zao huku baadhi yao wakiingizwa kwenye vishawishi vya rushwa.”

Ni maneno yake, Abdllah Mabindo (52) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Nyamagana B ya jiji Mwanza ambaye amejitosa kuanza kusoma toka serikali ilipoanzisha elimu bila malipo.

Mabindo ni baba wa mtoto mmoja ambaye tayari alishahitimu elimu ya chuo kikuu toka mwaka 2016 na ana mke mmoja, ni mkazi wa mtaa na kata ya Igogo jijini Mwanza ameelezea dhima yake ya kuanza shule kuwa ni baada ya kuona haki zake zinadhulumiwa na watu wachache wasiokuwa na nia njema.

Hakika wahenga walisema elimu haina mwisho ama elimu ni uhai ndio naweza kutumia maneno hayo wakati naandika makala haya.

Akizungumza na gazeti hili akiwa katika shule hiyo hivi karibuni, Mabindo anasema kilichomshawishi kuanza kusoma ni baada ya Rais John Magufuli kutangaza elimu bure.

“Mtu asiyejua kusoma na kuandika anaweza akaingia hata choo cha wanawake kwa sababu hajui lakini pia anaweza akashawishiwa kufanya jambo baya na likamletea madhara baadaye,” anasema Mabindo

Maendeleo yake kielimu

Kwa mjibu wa Mabindo anasema alianza shule akiwa hajui kusoma, kuandika wala kuhesabu na wakati huo alipata wakati mgumu kwani walimu na hata wanafunzi walikuwa wanamwogopa.

Anasema kutokana na changamoto hiyo aliwaeleza walimu kuwa nia yake ni kujua kusoma na ndipo walipomchukulia kama mwanafunzi wao wa kawaida.

Mabindo anasema sasa anaweza kusoma na kuandika na kwamba wanafunzi anawachukulia kama watoto wake na hata anapoenda mapumziko hucheza pamoja.

Aliwataka Watanzania wasiojua kusoma kutumia fursa hii kujifunza katika kuleta maendeleo endelevu ikiwamo kufikia uchumi wa kati huku akiwaonya kuwa suala hilo wasilichukulie kisiasa.

Kipi kilimshawishi kuanza shule?

“Kila kukicha dunia inabadilika na Tanzania ya sasa si ya zamani kwani kila kitu kinahitaji elimu, ukitaka kuanzisha biashara lazima uwe na elimu,” anasema Mabindo.

Anasema wakati anazaliwa suala la elimu halikuwa kipaumbele kwao, huku akitolea mfano kuwa hakuwahi kujua kuimba wimbo wa Taifa na wala hakujua kama umeandikwa kwenye kitabu.

Kitu kingine ambacho kimemshawishi kuanza masomo ni baada ya kudhulumiwa haki yake na aliyekuwa mwajiri wake katika kiwanda fulani jijini Mwanza.

Anasema aliandikiwa kulipwa kiasi cha Sh3 milioni lakini fedha hizo hakupewa badala yake ofisa utumishi wa kiwanda hicho alichana hayo makaratasi na kusababisha hela hiyo kupotea.

Suala jingine lililomfanya aingie shule ni kuwepo kwa masuala ya rushwa ambapo watu wengi wasiojua kusoma wanashawishiwa kufanya mambo yaliyo kinyume na hayo.

Mabindo ambaye anajiandaa na mitihani ya taifa ya darasa la nne utakaofanyika Novemba mwaka huu, anasema endapo atafanikiwa kufaulu atazunguka mikoa mbalimbali kueneza habari ya watu kurudi shule kuanza kusoma.

Changamoto zipi anapitia?

Suala la uchumi kwake ni kikwazo kikubwa kwani inachangia hata mahudhurio yake kuwa hafifu.

Anasema wapo watu waliokuwa wanajitolea kumsaidia lakini kwa sasa wamepunguza hali inayosababisha ashindwe kuhudhuria masomo yake kikamilifu na hivyo kulazimika kwenda kufanya kibarua.

Kikwazo kingine ni mawazo juu ya familia yake kwani hawataki kumuunga mkono akiwamo mkewe na baadhi ya ndugu na majirani kwa kile anachotaka kukifanya na anampiga vita kiasi kwamba anashindwa kuzingatia masomo yake.

Anasema wengi wanasema elimu yake kwa umri huo haina maana, hivyo ni bora akafanya shughuli zingine za kumuingizia kipato.

Walimu wanamzungumziaje?

Mwalimu wa darasa la nne katika shule hiyo, Abella Julius anasema maendeleo ya Mabindo ni mazuri na kwamba wanamsaidia kuhakikisha anatimiza ndoto yake.

Anasema Mabindo asipokuwepo shuleni siku akienda huchukua notisi za wenzake na kujisomea lakini pia wanamsaidia pale asipokuwepo.

Abella anabainisha changamoto zinazowakabili ni kuwa anapokosea hawezi kumkanya kama mtoto mdogo badala yake wanamfuata na kumwelekeza namna ya kufanya.

Lakini pia huwa wanampatia ushauri pale anapokuwa na matatizo ya kifamilia.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa Shule hiyo, Theresia Kivuma alisema elimu haina mwisho kwani umri wowote unaojisikia kwenda shule unaenda.

Aliwataka wale ambao hawakubahatika kusoma wasione kuwa wamepitwa na wakati madarasa bado yako wazi.

Ofisa elimu wa Jiji la Mwanza, Ephrahim Majinge alisema toka aajiriwe hajawahi kupokea mwanafunzi mwenye umri mkubwa kama wa mzee Mabindo na kwamba kinachofanyika kwa sasa wanachanganywa humo kati ya wanafunzi wazima na wadogo.

Ofisa elimu huyo alisema, halmashauri, imetenga kiasi cha Sh1.7 bilioni kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule zote 80 za msingi jijini humo.

Majinge alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 1,500 na madawati 12, 000 kwa shule zote.

“Kutokana na upungufu huo, halmashauri imeweza kununua mashine za kufyatulia tofali ambapo kila siku tofali 4, 000 zitakuwa zinafyatuliwa lengo ni kuhakikisha kwa mwaka tutakuwa tunakamilisha ujenzi wa vyumba 500 vya madarasa,” alisema Majinge.

Anasema mwaka huu wameandikisha watoto10, 000 watakaofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi huku matarajio yao ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kufaulisha kwa asilimia 100.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema wametenga kiasi cha Sh120 milioni kwa ajili ya kutengenezea madawati.

Kibamba alisema tayari fedha hizo zimeanza kusambazwa kwenye kila shule za halmashauri hiyo na kwamba zaidi ya madawati 54,000 yanahitajika kukidhi idadi ya vyumba vya madarasa 1,800 ambavyo vinahitajika kujengwa katika halmashauri hiyo.



Columnist: mwananchi.co.tz