Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MWANANCHI JUKWAALA FIKRA: Mbinu hizi zitawawezesha wahitimu kujiajiri wenyewe

76177 ELMU+PIC

Wed, 18 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ripoti ya soko la ajira kwa vijana kutoka Shirika la Kazi Duniani, (ILO) ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa takriban vijana milioni 71 duniani hawana ajira. Hii ni sawa na asilimia 13.1 ya vijana.

Vilevile utafiti wa elimu katika nchi za Afrika Mashariki uliofanywa mwaka 2018 na Chama cha Waajiri cha Afrika Mashariki (EAEO), ulionyesha kuwa nusu ya wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za ukanda huo hawana sifa na ujuzi wa kuajiriwa.

Utafiti huo unaonyesha kuwa vyuo vikuu na vya kati katika nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania, vinatoa elimu isiyowasaidia vijana hao kuajiriwa.

Nchini Tanzania changamoto ya ajira kwa vijana ni kubwa. Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Ajira imeweka mikakati mbalimbali katika kuandaa na kulinda ajira za vijana ikiwamo jitihada za Ofisi ya Waziri Mkuu inayoendesha programu ya kukuza ujuzi nchini. Programu hii iliyoanza mwaka 2016 ina lengo la kuwafikia takribani vijana milioni 4.4 nchi nzima ili kuwapa ujuzi na stadi mbalimbali zitakaowawezesha kujiajiri na kuajiri vijana wengine.

Lakini, pamoja na uwepo wa sera na programu hizo nzuri changamoto ya ajira kwa vijana nchini bado ni kubwa.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/17, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kwa mujibu wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2014 nguvu kazi ya Taifa ilikuwa watu 25,750,116, sawa na asilimia 57 ya watu wote Tanzania Bara. Aidha, kati ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi, walioajiriwa walikuwa watu 20,030,139 na wasioajiriwa walikuwa 2,291,785.

Pia Soma

Advertisement
Kwa mujibu wa utafiti huo watu wenye ajira katika jiji la Dar es Salaam walikuwa 1,927,367 sawa na asilimia 9.6 na katika maeneo mengine ya mijini walikuwa watu 5,131,422, (sawa na asilimia 25.6) na maeneo ya vijijini walikuwa watu 12,971,350, (sawa na asilimia 64.8).

Kutokana na utafiti huo, ilibainika kuwa idadi kubwa ya kundi la watu walioajiriwa lilikuwa na umri kati ya miaka 35 hadi 64 (asilimia 42.5).

Hivyo, ingawa uchumi wa Tanzania unaonekana kukua kwa wastani wa asilimia 7.1 kwa mwaka bado uchumi huu umekuwa na changamoto katika kutengeneza ajira zenye tija kwa wahitimu wetu.

Tunapasawa kujiuliza kama elimu tunayowapatia vijana wetu inawawezesha kujiajiri au kuajiriwa tu? Kwa nini wahitimu wengi wanasubiri ajira badala ya kujiajiri? Tatizo nini? Kama Taifa inaelekea bado tunapaswa kuwa makini zaidi ili kuandaa vijana wenye uwezo wa kujitegemea na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Sababu ya vijana kutojiajiri

Kwa nini changamoto hii bado ni kubwa hivi? Kunaweza kuwa na sababu nyingi lakini mojawapo ni mfumo wetu wa elimu ambao bado kwa kiasi kikubwa unawaandaa wahitimu kwa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa kuliko kujiajiri.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema elimu ni mchakato unaomuandaa mtu aweze kukabiliana na mazingira anayoishi.

Falsafa yake ya Elimu ya Kujitegemea ililenga kumuandaa mhitimu kuwa na ujuzi na maarifa ili kuweza kufanya kazi mbalimbali za kiuchumi na kujipatia kipato.

Je, wahitimu wetu katika ngazi mbalimbali za elimu wana uwezo, maarifa, ujuzi na stadi za kuwawezesha kuyakabili mazingira wanayoishi sasa?

Ili kukabiliana na changamoto hii sasa hatuna budi kuandaa mipango ya kuwafundisha vijana wetu kulingana na mazingira na fursa zilipo.

Aidha, yatupasa kuandaa mitalaa inayoendana na soko la ajira na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika kilimo, ufugaji na biashara ambavyo vina fursa nyingi nchini.

Ni jambo la kushangaza kuwa ingawa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini ambako kilimo na ufugaji ndizo shughuli kubwa za uchumi, bado masomo ya kilimo na ufugaji hayajatiliwa mkazo katika mitalaa ya elimu kuanzia ngazi ya chini.

Uwepo wa masomo ya kilimo na ufugaji utawawezesha wahitimu wetu kuwa na maarifa ya kujiajiri pindi wanapohitimu katika shule na vyuo mbalimbali badala ya wote kusubiri ajira chache na zenye ushindani mkubwa kwa sasa.

Pia, ili kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana, inatupasa kutilia mkazo elimu ya ufundi kuanzia ngazi ya elimu ya sekondari.

Miaka ya 1970 hadi 1990 tulikuwa na shule maalumu za sekondari za ufundi kama Mtwara, Moshi na Ifunda. Sina uhakika kama shule hizi bado zinatoa mafunzo hayo.

Kuwapo kwa shule hizi kulisaidia kupata wahitimu ambao waliweza kufanya shughuli mbalimbali za ufundi mara baada ya kumaliza masomo. Serikali inapaswa kuziimarisha shule hizi na pia kuanzisha shule nyingine zenye michepuo ya ufundi, hususani shule za sekondari za kata.

Pamoja na kuwashauri na kuwahimiza vijana walio vyuoni kuchagua kozi zinazoendana zaidi na vipaji vyao, ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi za elimumsingi, ulenge kutambua mapema vipaji vya watoto na namna ya kuwasaidia kufikia matamanio na malengo yao ya baadaye.

Aidha, inatubidi kuwekeza katika aina nyingi za utafiti unaolenga kujua changamoto za maendeleo ya vijana nchini kwa kuwashirikisha wadau kutoka sekta binafsi.

Kwa vijana wanaohitimu katika shule na vyuo vyetu, siyo vibaya wakaiga mfano wa Rwanda ambako baada ya kuhitimu shahada ya kwanza, wahitimu hujiunga na vyuo vya ufundi stadi, kujifunza fani mbalimbali kama vile upishi, kuchomelea, useremala, mitindo, umakenika, kilimo, ufugaji, ujenzi na nyinginezo.

Hatua hii imewasaidia wahitimu wa vyuo vikuu kuwa na uwezo wa kujiajiri, badala ya kusubiri ajira za ofisini ambazo ni chache.

Ni dhahiri kuwa ongezeko kubwa la wahitimu wasiokuwa na ajira wala maarifa na utayari wa kujiajiri litakwamisha jitihada za kufikia matarajio yetu ya kufikia kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Taifa la kesho litajengwa na vijana wa sasa!

Columnist: mwananchi.co.tz