Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Dean Rusk alikuwa amekata tamaa ya kuiingiza Zanzibar katika muungano wa Afrika Mashariki na hofu yake ilizidi kiasi cha kuanza kufikiria mpango mahsusi wa kuvamia visiwa hivyo, yaani Zanzibar Action Plan.
Ndipo Rusk alipomuandikia barua Rab Butler, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kuhusu mpango huo ikiwa ule wa kuiunganisha Tanganyika-Zanzibar ungeshindikana.
“Nina matumaini makubwa kwamba mipango hii itafanyika haraka sana na itasaidiwa na serikali zote mbili (Marekani na Uingereza) na ambayo inaweza kutumiwa haraka iwezekanavyo,” anasema Rusk katika ujumbe wa telegramu.
“Kwa uamuzi wangu binafsi ni kwamba tunalazimika kuchukua hatua bila kukawia ili kuondoa kabisa hali isiyoridhisha inayoendelea Zanzibar.”
Katika telegramu iliyotumwa baadaye, ambayo nayo ilitumwa kwa siri, Rusk alitoa pendekezo la kumhusisha Dk Hastin Kamuzu Banda, Rais wa Malawi ili aongee na Karume kuhusu suala la kujiunga katika “Familia ya Afrika Mashariki”.
Kile ambacho Wamarekani na Waingereza walitaka kuwa na hakika nacho—ingawa kila nchi moja ilikuwa inatumia njia yake tofauti ya kuhakikisha kwamba Zanzibar inatiwa ndani ya nchi nyingine—ni kwamba Wakomunisti waliokuwa Zanzibar, kama Abdulrahman Mohamed Babu na wafuasi wake wanakosa nafasi muhimu za uongozi.
Related Content
- MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Marekani yaanza kukwama mpango wa Muungano - 6
- MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Neno muungano laanza kutajwa-4
- MUUNGANO WA TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: CIA ilivyoanza kuingilia siasa za Zanzibar -3
- MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Jasusi CIA atinga Zanzibar kama ofisa ubalozi -5
Wakati fulani, Frank Carlucci aliwahi kutoa pendekezo lake kwa CIA kwamba ilipaswa kubadili mtindo wake wa kuendesha propaganda—hasa propaganda dhidi ya Babu.
“Ingawa Idara (CIA) inaweza kuamua kwamba ni kwa maslahi yetu kuendesha na kuendeleza kampeni dhidi ya Babu na kumfanya aonekana kama tishio kwa nchi zisizofungamana na upande wowote, badala yake napendekeza Idara iunde jeshi, washauri na wanadiplomasia kuliko kutumia mtu mmoja mmoja kumshughulikia,” alishauri.
Carlucci alijaribu kutazama mbali zaidi. Alisema swali ambalo watu wengi wanaweza kujiuliza “ni kwanini kisiwa kidogo na kilicho mbali kama Zanzibar kilazimike kuanzisha jeshi linalohitaji vifaa vya kivita, wakati kina polisi wa kutosha, ikiwa hakuna hali ya uchokozi na uchochezi wowote kutoka nje inayokusudiwa dhidi ya kisiwa hicho?”
Wakitazama hali ya mambo kuanzia hapo, hatua hiyo ingeweza kuivuta Afrika kuifikiria zaidi Zanzibar kuliko kujaribu kuwashawishi Waafrika waamini kwamba mtu mtanashati, ambaye wanamjua sana, yaani Abdulrahman Babu, ni tishio kwa nchi zisizofungamana na upande wowote.
Kwa hivyo Wamarekani wakaona kuwa ikiwa wangejaribu kutengeneza mazingira fulani yaonekane kana kwamba Abdulrahman Babu anataka kuanzisha jeshi visiwani Zanzibar yangeushtua sana ulimwengu kiasi kwamba hapo ndipo angeonekana kuwa tishio kuliko kuendesha propagana za kusema kwa maneno matupu tu kwamba yeye ni tishio.
Uvumilivu wa Dean Rusk ulielekea kumshinda. Alianza hata kushindwa kuwavumilia washirika wake wa Uingereza. Alitaka ZAP (Zanzibar Action Plan) kuanza na kutumiwa haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wa Marekani, hali ya mambo ilionekana kana kwamba ilikuwa ikiendeshwa taratibu kuliko ilivyokusudiwa. Jumapili ya Machi 29 Dean Rusk aliandika ujumbe mwingine wa siri na kuutuma kwa balozi wake aliyekuwa mjini London, Uingereza, David Bruce.
“Tunasikitishwa na kuingiwa na wasiwasi sana juu ya kile kinachoonekana kama ulegevu na kuridhika kwa Waingereza kuhusu hali ya kisiasa ya Zanzibar,” aliandika Rusk.
“Zanzibar peke yake, kwa kweli, ni jambo lenye umuhimu mdogo sana kwetu, lakini Zanzibar kama kituo cha shughuli za kikomunisti katika Afrika Mashariki ni jambo tofauti kabisa na tunapata tabu sana kuelewa kwanini Uingereza haina wasiwasi na hili jambo la mwisho (la Zanzibar kuwa kituo cha Wakomunisti).
“Sisi, kwa kweli, tunatambua kuhusika kwa Serikali ya Uingereza katika kuingilia kati masuala yake ya Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe). Hata hivyo, kama kwa kweli tukifanya kazi pamoja katika jambo hili, inaonekana kwamba kutakuwa na nafasi nzuri zaidi—angalau tunapaswa kuongeza jitihada kubwa zaidi—kwamba ombi la msaada wa Uingereza lingeweza kupatikana nje ya Zanzibar.
“Kuna jambo moja la wazi kabisa kwamba, kama tungelazimika kuwaambia Waingereza kuwa kama hatuwezi kupata ushirikiano wao na kama hawataliongoza jambo hili na sisi tukaja nyuma yao, tutasonga mbele na kulifanya sisi wenyewe katika kushughulikia tatizo la Zanzibar na majirani zake wa Afrika Mashariki. Uingereza itaogopa na itaamua kuucheza mpira huo.”
Marekani walikuwa wakiwashawishi Waingereza walifanye jambo hilo wakati Wamarekani wakiwa wamejificha nyuma yao. Huenda walikuwa wakitoa ushawishi huo kwa sababu Tanganyika na Zanzibar zilikuwa makoloni ya Uingereza kabla hazijapata uhuru. Wamarekani waliona kuwa ikiwa Uingereza ingeingilia haingesababisha gumzo kubwa kama ambavyo Marekani wangeingilia.
Wakati yote hayo yakiendelea, Carlucci alikuwa akifanya kazi kwa bidii katika visiwa vya Zanzibar—pengine kuliko mwanasiasa mwingine yeyote duniani kwa wakati huo.
Alihakikisha kwamba alipokea taarifa zozote za mambo yaliyohusu siasa za visiwa hivyo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hakupuuza habari yoyote aliyopokea—hata kama ilikuwa uvumi—lakini hakuamini habari yoyote, hata kama ilikuwa ya kweli, mpaka alipoifanyia uchunguzi wa kutosha yeye mwenyewe na kuwa na uhakika wa kutosha kabla hajaipasha habari Serikali ya Marekani.
Kadiri Wamarekani walivyojitahidi kuwasisitiza Waingereza waongeze kasi yao ya kulishughulikia suala la Zanzibar, ndivyo Waingereza nao walivyoonekana kupunguza kasi katika kushughulikia suala hilo.
Hali hiyo iliwafanya Wamarekani kuhangaika zaidi. Kilichowafanya wawasukume Waingereza ni kwa sababu Tanganyika na Zanzibar ni nchi zilizokuwa chini ya koloni la Waingereza. Lakini inaelekea kuwa Ukomunisti katika visiwa vya Unguja na Pemba uliwatisha zaidi Wamarekani kuliko ulivyowatisha Waingereza.
Itaendelea kesho