Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Nyerere aenda kuonana na Karume ziara ya Zanzibar - 11

53199 Pic+muungano

Sat, 20 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati vuguvugu la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar likiendelea, balozi wa Marekani mjini Dar es Salaam, William Leonhart alianza kuwa na kazi nyingi za kutoa taarifa za matukio ya siku kwa siku.

Balozi wa Marekani nchini, William Leonhart alituma ujumbe kueleza kinachoendelea.

“Mradi wa Tanganyika-Zanzibar sasa umefikia hatua muhimu sana,” aliandika na kueleza matukio hayo kuwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kambona kwenda Tabora na Kigoma na amri ya kupeleka ndege Zanzibar.

Askari walipatao 300 walipelekwa Zanzibar kulinda amani mara baada ya mapinduzi. hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na hofu kuwa John Okello, aliyeshiriki mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na wafuasi wake, pia walikuwa tishio kwa viongozi wengine wa ASP.

Hiyo ndiyo iliyokuwa kama nguvu ya Nyerere katika kujadiliana na Karume kwa kuwa wakati huo Zanzibar ilikuwa bado haijaunda vikosi imara kwa ulinzi na usalama na hivyo kuitegemea Tanganyika.

Kwa hiyo, baada ya wawili hao kuonekana hawajafikia muafaka, ndipo ilipotoka amri hiyo ya kuondoa askari Zanzibar, amri ambayo ingekuwa mbaya kwa viongozi wa visiwa hivyo.

Related Content

Kwa hiyo, balozi Leonhart alikuwa akitoa taarifa njema kuwa mradi wao ulikuwa unaendelea vizuri.

Jambo la pili lililoelezwa na Balozi Leonhart ni kuhusu safari ya Karume, Tanganyika.

“Karume aliwasili mjini Dar es Salaam Aprili 18 majira ya jioni kwa ndege ya Tangov’t ambayo inaelekea ilitumwa kwa ajili ya kumchukua Kassim Hanga. Hadi sasa, kwa kadiri tunavyoona, Karume aliendelea kukaa mjini Dar es Salaam kutwa nzima ya Aprili 19. Hakukuwa na taarifa kwa umma iliyotolewa kwa Karume kuja au kuwa mjini Dar,” alisema Lonhart.

Pia Leonhart alitoa taarifa kuhusu kurejea kwa Kambona Dar es Salaam baada ya safari yake ya mikoa ya Tabora na Kigoma kukatizwa ghafla na Rais Nyerere.

“Kambona alirejea Dar Aprili 19, siku moja kabla tofauti na ilivyokuwa imepangwa na kuwaambia waandishi wa habari aliokutana nao uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kwamba Nyerere amemwita arudi. (Ali Mwinyi) Tambwe pia alirejea Dar Aprili 19, siku moja kabla ya siku iliyopangwa.”

Siku iliyofuata, yaani Aprili 21, Mwalimu Nyerere alimuapisha Sir Ralph Wildham kuwa Jaji Mkuu wa Tanganyika na kumwambia moja ya kazi zake za kwanza iwe kuwashughulikia kikamilifu wanajeshi waliotaka kuipindua serikali yake Januari 19, 1964.

Ndipo Sir Wildham akatangaza rasmi kuwa wanajeshi wa kambi ya Colito waliotaka kuiangusha serikali watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, yaani Aprili 27, 1964.

Rais pia alimteua Kapteni Abdallah Twalipo wakati huo akiwa na miaka 35 na Kapteni Lukias Shaftaeli (39) kuwa wajumbe wa mahakama ya kijeshi. Sir Wildham akawa rais wa mahakama hiyo. Mkurugenzi wa mashtaka, Herbert Wiltshire Chitepo, alisema angewaita mashahidi 25.

Uasi huo ulifanyika wakati hali pia ikiwa si nzuri visiwani Zanzibar. Waasi walishikilia sehemu kadhaa muhimu, zikiwemo kambi za jeshi kabla ya Rais Nyerere kuomba msaada kwa Malkia wa Uingereza aliyetuma askari wake kuja kutuliza.

Hata kabla ya kutulia, baadhi ya waasi walianza kujisalimisha na baadaye hali kutulia kabisa katika kipindi cha wiki moja.

Lakini uasi huo ndio uliofanya serikali baadaye kuanzisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ, ambalo limekuwa imara zaidi kulinganisha na lile lililoachwa na mkoloni.

Siku hiyo ya Aprili 21, balozi mdogo wa Marekani visiwani Zanzibar, Frank Carlucci, pia alituma ujumbe kwa waziri wake wa mambo ya nje nchini Marekani.

“Vyanzo vya habari vinasema wazee wamemwambia Karume kuwa USG (Serikali ya Marekani) na HMG (Serikali ya Malkia ya Uingereza) ni marafiki wa tangu kale ambao wameisaidia Zanzibar siku zilizopita na wamemhakikishia kwamba Serikali ya Zanzibar lazima iwape nafasi (USG na HMG) kuwaonyesha kuwa wao bado ni marafiki,” aliandika.

“Vijana wa mrengo wa kushoto walizidiwa ujanja na wamelazimika kuunga mkono mawazo ya Karume kwa imani yake mpya kwa nchi za Magharibi. Chanzo hicho kinasema Karume hakuwa mtu wa kuonyesha shukrani kwa zawadi ya USG ya ujenzi wa ‘Mradi wa Mercury’ na majenereta yake.”

Alieleza kuwa uamuzi wa Karume kumpeleka mtoto wake kwenda kusoma Marekani ni tafsiri dhahiri kwamba ana imani na taifa hilo.

Siku iliyofuata, Mwalimu Nyerere alisafiri kwenda Zanzibar kwa “ziara ya kirafiki kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuonana na Rais Abeid Aman Karume”.

Hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza visiwani humo tangu Serikali ya Mapinduzi ilipotwaa madaraka Januari 12, 1964 kutoka kwa utawala wa Kisultani.

Awali alizuru Zanzibar Februari 5, 1957 wakati wa sherehe za miaka minane tangu kuzaliwa kwa ASP.

Columnist: mwananchi.co.tz