Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MUSTAKABALI WA TAIFA: Wapatanishwe

99280 Dini+pic MUSTAKABALI WA TAIFA: Wapatanishwe

Tue, 17 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam/Moshi/Mwanza. Msuguano wa kisiasa uliozuka hivi karibuni nchini kati ya viongozi wakuu wa Chadema, kauli za wanasiasa na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola, unaweza kutatuliwa iwapo pande hizo zitapatanishwa.

Wachambuzi wa siasa na viongozi wa dini walioulizwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo, walipendekeza kutafutwa haraka suluhisho la mgogoro huo na kushauri pande hizo zipatanishwe.

Watu hao wamependekeza kufanyika kwa mjadala wa kitaifa kwa ajili ya upatanisho na kutafutwa suluhisho la kuondokana na mbegu za chuki na mgawanyiko unaolinyemelea taifa kwa sasa.

Kwa takribani siku tano kuanzia Machi 10, baada ya hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya viongozi tisa wa Chadema, taifa limeshuhudia matukio na kauli kali za viongozi wa dola na kisiasa.

Viongozi wa Chadema walihukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh350 milioni baada ya kupatikana na hatia ya kufanya makosa 12 kati ya 13 yanayohusu maandamano yasiyo halali na ya uchochezi.

Siku ya hukumu, polisi walitumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa Chadema na siku chache baadaye Jeshi la Magereza lilitumia nguvu kuwatawanya wafuasi na viongozi wa Chadema.

Pia Soma

Advertisement
Wafuasi hao na viongozi walikuwa wamejitokeza eneo la magereza kumpokea mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ambaye alikuwa wa mwisho kutoka gerezani baada ya kulipiwa faini ya Sh70 milioni, Ijumaa iliyopita.

Katika matumizi hayo ya nguvu, baadhi ya viongozi wa chama hicho walijeruhiwa.

Matukio hayo yaliifanya Mwananchi kutafuta maoni ya jinsi ya kuondoa hali hiyo katika jamii na wachambuzi walipendekeza namna ya kuondokana na tatizo hilo.

Viongozi wa dini

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alisema vyombo vya dola nchini vinatakiwa kutumia mamlaka yake kwa uadilifu na kuwa na hofu ya Mungu.

“Inasikitisha sana,” alisema Askofu Shoo, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini.

“Ninajiuliza na ninatamani kila Mtanzania ajiulize, ‘tunaelekea wapi kama taifa’. Wanasiasa waache kutumia nafasi zao vibaya.

“Tofauti zao zisiwe sababu ya kuchukiana kiasi cha kuumizana. Kuna chuki mbaya inajengeka, kuna migawanyiko kati ya vyama, na katikati ya vyama. Panahitajika haraka sana hatua za upatanisho.”

Askofu Shoo alisema kunahitajika upatanisho baina ya vyama na akatumia maneno ya kitabu cha Waebrania 12:14 katika Biblia kusisitiza ujumbe wake kwa taifa.

“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote,... shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua,” alinukuu.

Naye sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema kinachotakiwa ni wananchi na wanasiasa kutii sheria bila kushurutishwa na vyombo vya dola, akisema vyombo hivyo vina uwezo wa kufanya jambo lolote bila kuulizwa.

“Tusiviwekee ujeuri vyombo vya dola kwa sababu haviulizwi. Lakini vyombo hivi vya dola vinapaswa kutumia nguvu kiasi pale inapobidi kulingana na jambo lenyewe lakini si wakati wote vinapaswa kutumia nguvu,” alisema Sheikh Alhad.

Akizungumzia suala hilo, katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda alisema anachoona ni watawala wanatekeleza mpango wa kuvibana vyama vya upinzani.

“Ni muhimu viongozi waliopo madarakani watambue kuwa Watanzania wote wana haki ya kikatiba ya kuongoza taifa. Hivyo nawashauri wawaache wapinzani wafanye siasa na wao kupitia chama chao wafanye halafu wananchi wataamua kupitia sanduku la kura,” alisema Sheikh Ponda.

Maoni ya wasomi

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amewasihi viongozi wakuu wastaafu kujitokeza na kutoa ushauri .

Ngurumwa amewaomba marais wastaafu, Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wakemee yanayoendelea bila woga. “Pia wananchi wenyewe waamke na kupinga matendo ambayo yako nje ya sheria,” alidai Ole Ngurumwa.

Ole Ngurumwa alisema makundi yote ya jamii yanatakiwa yaanze kupaza sauti kukemea mbegu za chuki ambazo alisema zinaenea kwa kasi.

Naye mchambuzi wa siasa na mtetezi wa haki za binadamu, Edwin Soko alisema jukumu la kulinda na kutetea utaifa, utu wa mwanadamu, amani, upendo na mshikamano ni la watu wote kuanzia viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na Watanzania wa kada zote bila kujali tofauti zao.

“Watanzania wote bila kujali vyeo, itikadi wala maeneo yetu tutambue na kuamini kwanza katika utaifa; vyama vya siasa na makundi mengine ya kimaslahi yaje baadaye. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuliponya Taifa kutoka katika mihemko na migawanyiko inayoanza kujitokeza nchini,” alisema Soko, ambaye pia ni mwanafunzi wa sheria.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) Mwanza, Dk Kanaeli Kaale aliwashauri wanasiasa wa pande zote kuanzia wale wa CCM na upinzani kuzingatia na kutii sheria wakati wa kutekeleza haki ya kidemokrasia ya vyama vingi.

“Katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kila upande unatetea na kuvutia kwake, lakini ni vema yote hayo yafanyike kwa kufuata na kuzingatia misingi ya sheria na kuwaachia wapigakura kuamua katika sanduku la kura. Wanasiasa wakifanya hivyo ndipo watalitendea haki Taifa,” alisema Dk Kaale.

Dk Kaale alisema panapotokea makosa, walioko madarakani na vyombo vya dola waepuke kutumia nguvu kupita kiasi.

Imetayarishwa na Daniel Mjema, Peter Saramba na Bakari Kiango.

Columnist: mwananchi.co.tz