Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MSIMU 2018/19: Changamoto ya timu 20 Ligi Kuu hizi hapa

9458 Pic+changamoto TZWeb

Mon, 18 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Msimu wa Ligi Kuu Bara wa 2017/18 umemalizika kwa Simba kutwaa ubingwa ikiwa ni mara ya kwanza baada ya misimu minne kupita.

Simba ilijipanga, imelazimika kufanya usajili ghali ili kutwaa ubingwa huo na kukata tiketiya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia Desemba mwaka huu.

Michuano hiyo itaanza Desemba baada ya kumalizika hii inayoendelea na ni kutokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufanyia mabadiliko uendeshaji wa mashindano yake.

Michuano ya klabu Afrika sasa itaanza Desemba na kumalizika Mei na mashindano mengine yataanza Septemba 2019 hadi Mei 2020.

Mabadiliko mengine ambayo CAF imeyafanya ni ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo sasa fainali zake zitakuwa zikifanyika kati ya Juni na Julai ya mwaka wa mashindano.

Hayo ni mambo ya Simba na Mtibwa kwa mashindano yao ya klabu Afrika.

Kikubwa hapa ni kumalizika kwa Ligi Kuu na sasa klabu zimeingia kwenye mapambano ya kunyang’anyana wachezaji na timu hutumika kuimarisha vikosi vyao.

Kwa wachezaji hasa wale ambao walifanya vizuri wakati msimu unaendelea, huu ni wakati wa mavuno kwao kwa kupata vitita vya fedha za kujiunga na timu nyingine au kuongeza mikataba ya kuendelea kuchezea klabu walizozitumikia msimu ilioisha.

Inatakiwa mchezaji ajiulize, mchezaji mwenzake au wenzake walikuwa timu moja, kwanini wagombewe? Kwanini asiwe yeye na anakuwa huyu. Bila kutafakari hapo, kwa mchezaji atakuwa na walakini.

Na kwa kutafakari, lazima kuonyesha utofauti ili msimu ujao unapomalizika, wavune mamilioni.

Mbali na usajili, kipindi kama hiki pia hutumiwa na timu kama wakati wa kufanya tathmini ya mwenendo na ufanisi wa kikosi katika msimu uliomalizika na ndio wakati wa kuandaa mipango mikakati kwa ajili ya msimu unaofuata kwenye ligi.

Hata hivyo tofauti na nyakati za nyuma, hesabu na mipango ya timu kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu vinatakiwa kuandaliwa kwa umakini mkubwa ili klabu ziweze kukabiliana na changamoto ambazo zitakumbana nazo kwenye ligi.

Hii ni kwa sababu idadi ya timu ambazo zitashiriki Ligi Kuu msimu ujao ni 20 hivyo ni wazi lazima kutakuwepo na changamoto ambazo timu itakayoshindwa kuzitatua itajiweka kwenye athari ya kushuka daraja.

Spoti Mikiki inakuletea changamoto kadhaa kwa namna moja au nyingine zina uwezekano mkubwa wa kuikabili ligi yetu msimu ujao kutokana na ongezeko la timu kutoka 16 hadi 20.

Gharama za uendeshaji

Ligi Kuu imepanuka wigo, kutoka timu 16 hadi 20 baada ya Alliance, JKT Tanzania, Lyon, KMC, Biashara Mara na Coastal Union kupanda Ligi Kuu.

Timu hizo zitaungana na hizi zilizopo za Ligi Kuu kutengeneza timu 20.

Hata hivyo, idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu hazina wadhamini binafsi na nyingi zinategemea fedha kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi ambao ni kampuni za Azam Media, Vodacom na Benki ya KCB ambazo hutolewa kwa kila timu inayoshiriki ligi kama utaratibu ulivyo.

Hata zile ambazo zina udhamini binafsi, bado fedha wanazopata hazitoshi kuzifanya zimudu gharama za kuendesha timu kwa msimu mzima wa ligi katika kusimamia masuala kama usafiri, huduma za malazi, chakula, posho na mishahara kwa wachezaji, makocha na watendaji wengine wa timu.

Kuongezeka kwa idadi ya timu kwenye Ligi Kuu kutoka 16 hadi 20 kunamaanisha ongezeko la gharama za uendeshaji kwa kila timu ambayo itashiriki ligi hiyo.

Kuna uwezekano mkubwa baadhi ya timu zikajikuta zinakwama kujiendesha kabla hata ligi haijaisha na kikubwa hapo ni kufanya vibaya sambamba na kushindwa kuleta ushindani kwenye ligi.

Mashindano ya kimataifa

Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji mashindano wa CAF unamaanisha kuwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakuwa zinachezwa sambamba na mechi za kimataifa kwa klabu ambazo zitawakilisha Tanzania.

Pamoja na hilo, pia timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na ile ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ zitakuwa zinakabiliwa na mechi mbalimbali za kimataifa za kirafiki na zile za kimashindano.

Mechi hizo za kimataifa zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ratiba ya ligi kupanguliwa mara kwa mara jambo ambalo linaweza kupunguza ushindani na uhondo wake. Panguapangua ya ratiba itachukua nafasi kubwa kwa jinsi inavyoonekana.

Viwanja vibovu

Katika msimu uliopita, tumeshuhudia viwanja vichache tu ambavyo vina hadhi ya kutumika kwa mechi za Ligi Kuu huku idadi kubwa ya viwanja vilivyobakia vikiwa ni vibovu na vina hadhi ndogo ya kuchezeka kwa mechi za mashindano makubwa kama Ligi Kuu.

Idadi kubwa ya viwanja pia vina miundombinu isiyoridhisha ya utoaji maji taka lakini pia havina mazingira mazuri yanayoweza kusaidia na kurahisisha urushaji wa matangazo ya mechi kwenye luninga.

Kabla hata changamoto ya ubovu wa viwanja haijatatuliwa, Ligi Kuu imekutana na ongezeko la timu jambo ambalo huenda likachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uchakavu wa viwanja kwani vitalazimika kutumika kwa mechi za mfululizo bila kupata nafasi ya kufanyiwa ukarabati mdogo.

Kungekuwa na kamati ya kukagua viwanja, kamati huru na kutoa uamuzi wake ikiwemo hata kufungia viwanja husika.

TFF, Bodi ya Ligi na Kamati, ingefanya ukaguzi wa viwanja vya timu hizo 20 na kutoa mapendekezo ya haraka nini kifanyike.

Hivi mkoa wa Morogoro na raslimali zote ilizonazo, wanashindwa kuwa na pitch iliyosimama! Ligi zimemalizika hadi Agosti, kwanini viwanja visikarabatiwe? Uwanja wa Namfua, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ni mfano mzuri.

Inatakiwa Uwanja wa Biashara Mara wakati huu unakuwa katika hatua za mwisho mwisho tayari kwa Ligi Kuu. Itashangaza kuona uwanja unakuwa na vipara.

Kamati ingewasiliana na wamiliki wa viwanja katika mikoa husika pamoja na halmashauri kwani mechi zikichezwa sio wanakimbilia asilimia za mapato, pia maboresho yanatakiwa.

Hali ya kijiografia na miundombinu

Idadi kubwa ya timu zinatoka katika mikoa na maeneo tofauti ya nchi hivyo hulazimika kusafiri umbali mrefu kufikia vituo kwa ajili ya kucheza mechi husika.

Kutokana na idadi kubwa ya timu kutokuwa na nguvu ya kiuchumi, hulazimika kutumia usafiri wa ardhini ambao hukutana na changamoto za ubovu wa miundombinu hasa barabara jambo linalowalazimisha wasafiri umbali mrefu na kusababisha uchovu kwa wachezaji.

Hapo wachezaji wanatumia muda mrefu barabarani na wakifika saa 48 mechi, bila kujiandaa. Baadhi ya timu zinafungwa kwa mengi ukiacha masuala ya kiufundi.

Pamoja na hilo, changamoto nyingine ni hali ya hewa ambapo kuna nyakati ratiba ya ligi huangukia wakati wa masika na huwa na mvua nyingi ambazo husababisha mechi kuahirishwa mara kwa mara jambo ambalo huchangia kupanguliwa kwa ratiba ya ligi.

Majeraha & uchovu

Uwingi wa timu utalazimisha wachezaji kucheza idadi kubwa ya mechi mfululizo pasipo kupata nafasi ya kupumzika, kuweka fiti miili sambamba na kufanya programu za maandalizi kwa ajili ya michezo inayofuata.

Idadi kubwa ya timu hazina nguvu ya kiuchumi kuajiri wataalamu wa afya kwa ajili ya kuweka sawa miili na afya za wachezaji pindi wanapomaliza mechi.

Hili kwa kiasi kikubwa litachangia kuzalisha majeruhi sambamba na kusababisha uchovu kwa wachezaji jambo litakalozidhoofisha na kupunguza ushindani wa ligi.

Columnist: mwananchi.co.tz