Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MKUTANO MKUU 2019: Jinsi harakati za ukombozi zilivyozaa Sadc

69022 Pic+sadc

Wed, 31 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katikati ya mwaka 1979, viongozi wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi za kusini mwa Afrika walikutana jijini Arusha.

Haikuwa kawaida kwa marais wa Tanzania, Zambia, Botswana, Angola na Msumbiji kukutana kwenye mji huo wa kitalii.

Lakini vikao hivyo pia vilikuwa vikifanyika katika miji mikuu ya nchi hizo au katika miji mingine iliyokuwa karibu na uwanja wa mapambano.

Inawezekana kikao hicho cha mwaka 1979 hakikutiliwa maanani sana kwani wakati huo Tanzania ndiyo ilikuwa imetoka kwenye vita vya kumng’oa nduli Idi Amin nchini Uganda.

Vita hivyo, vilivyodumu kwa takriban miezi tisa kuanzia Oktoba mwaka 1978, viliitumbukiza Tanzania katika matatizo makubwa ya kiuchumi.

Lakini, kikao hicho cha viongozi wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele chini ya uenyekiti wa Mwalimu Julius Nyerere kilimalizika kwa tangazo la kuanzishwa kwa taasisi muhimu.

Pia Soma

Ilijulikana kama Sadcc, yaani Taasisi ya Kuratibu Maendeleo ya Nchi Zilizo Kusini mwa Afrika. Hivi sasa inajulikana kama Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).

Vyombo vya habari vya nchi za magharibi ambazo zilikuwa na ofisi za kikanda Afrika Kusini, havikuwa nyuma kuangazia taasisi hiyo mpya.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi wa nchi hizo kuacha kutoa matamko makali juu ya vita vya ukombozi na badala yake kuzungumzia ushirikiano wa kiuchumi.

Hiyo ilifanyika licha ya kwamba baadhi ya wadadisi wa mambo waliona ni mapema mno kwa viongozi hao kuanza kufikiria masuala ya uchumi wakati vita vilikuwa bado vinarindima dhidi ya utawala wa wachache katika nchi kadhaa Kusini mwa Afrika.

Uhuru wa Zimbabwe, iliyojulikana awali kama Rhodesia, ulikuwa umekaribia na maandalizi yote ya mazungumzo ya Lancaster House yalikuwa tayari, lakini nchi hiyo ilikuwa chini ya viongozi wa Kiafrika waliokuwa vibaraka kama vile Askofu Abel Muzorewa.

Angola ilikuwa huru tayari (tangu mwaka 1975), lakini hali ilikuwa tete zaidi kuliko wakati wa vita vya ukombozi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa zaidi ya miongo miwili.

Nchini Afrika Kusini, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa utawala wa watu wachache weupe ambao ulikuwa umejikita vizuri, kutishia na hata kuanza mashambulizi katika nchi za mstari wa mbele zilizokuwa zinaunga mkono harakati za ukombozi.

Wakati huo, Namibia ilikuwa chini ya utawala wa Afrika Kusini licha ya vita vya ukombozi vilivyokuwa vikiongozwa na wapiganaji wa Swapo ili kuwaondoa makaburu.

Ingawa umoja huo wa ukombozi wa Afrika ulidumu hadi mwanzoni mwa miaka ya tisini, kuundwa kwa Sadcc kuliweka mwelekeo mpya katika siasa za Kusini mwa Afrika. Kuna baadhi waliona kuwa kuanzishwa kwa umoja huo kulikuwa mwanzo wa ukanda huo kujiandaa kwani mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ulikuwa ukikaribia.

Hisia zilijengeka kuwa iwapo nchi zote za ukanda huo, zilizokuwa chini ya ukoloni zingekombolewa aidha kwa mtutu wa bunduki au mazungumzo, ulikuwa wakati muafaka kushughulikia ushirikiano wa kiuchumi.

Ingawa Sadcc ilibuniwa jijini Arusha mwaka 1979, ilikuwa mwaka uliofuatia (yaani 1980) ndipo ilipoanzishwa rasmi na makao yake makuu kuwa Gaborone, Botswana.

Mwaka 1980 ulikuwa wa muhimu sana katika harakati za ukombozi. Ni mwaka huo Zimbabwe ilipata uhuru baada ya vita vikali vya ukombozi vilivyodumu kwa miaka kadhaa.

Chini ya kiongozi wake machachari wakati huo, Robert Mugabe, Zimbabwe ilijiunga si tu na Sadcc pekee yake, bali ikawa mwanachama wa sita wa nchi zilizo mstari wa mbele katika ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Nchi tisa, ikiwemo Tanzania, zilitia sahihi Tamko la Lusaka la Kuanzishwa rasmi kwa Sadcc. Nchi nyingine ni zile zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele na zilizokuwa huru katika ukanda huo.

Moja ya majukumu ya umoja huo yalikuwa ni kuhamasisha umoja wa kisiasa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya eneo hilo. Hata hivyo, wakati huo Afrika Kusini na Namibia zilikuwa chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Mnamo mwaka 1992, Sadcc iligeuzwa kuwa Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) baada ya nchi wanachama kutia saini Tamko la Windhoek na Mkataba wa Sadc.

Mwaka 2001, Mkataba wa Sadc ulifanyiwa marekebisho makubwa na mifumo mingi ya taasisi hiyo ilibadilishwa ili kwenda na wakati.

Mwaka juzi (yaani 2017) Comoro ilikuwa nchi ya 16 kujiunga na umoja huo wakati wa mkutano wa 37 uliofanyika Afrika Kusini.

Kesho katika safu hii tunaendelea na mfululizo wa makala za Sadc kwa kukuletea makala inayosema Bila Tanzania Sadc Isingekuwapo.

Columnist: mwananchi.co.tz