Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Zijue sifa za kufundisha Kiswahili nje ya nchi

22544 Erasto+Duwe TanzaniaWeb

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara kadhaa tumekuwa tukishangilia tusikiapo kuwa mataifa ya kigeni ndani na nje ya Afrika yanapanga kuanza kufundisha Kiswahili.

Tuna kila sababu ya kufanya hivyo. Mosi, bila shaka tunashangilia kwa kuwa Kiswahili ni lugha yetu,. Kwa hivyo kufundishwa kwa Kiswahili katika mataifa hayo ni ishara ya kutumainisha kwamba Kiswahili kinazidi kusambaa na kujiongezea thamani.

Pili, tunafanya hivyo pia bila shaka tukiwa tunawazia nafasi za ajira za ufundishaji wa Kiswahili katika mataifa hayo husika.

Sina shaka pia wengi wangetamani kuzipata nafasi hizo za ajira katika mataifa hayo ya kigeni kwa sababu mbalimbali.

Mara kadhaa, kupitia safu hii tulipoandika kuhusu kusambaa kwa Kiswahili ulimwenguni na kuongezeka kwa mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili, baadhi ya wasomaji wetu waliuliza namna wanavyoweza kupata nafasi hizo za ajira ingawa lengo letu ni kutoa elimu kuhusu Kiswahili na kuwahabarisha kinachoendelea duniani kuhusu lugha hii adhimu ya Kiswahili.

Dhamira kubwa ya safu hii leo ni kukusihi mpenzi msomaji kuhusu hatua tunazopaswa kuchukua Waswahili wenye mapenzi na Kiswahili.

Awali ya yote ifahamike kwamba kuna Kiswahili cha mawasiliano na Kiswahili cha kitaalamu katika viwango mbalimbali vya elimu.

Mataifa ya kigeni yanapotangaza ajira au kuweka mikakati ya kufundisha Kiswahili katika shule za msingi, sekondari au vyuo, ifahamike kwamba wanaohitajika ni wataalamu wa Kiswahili katika viwango hivyo vya elimu. Kujua tu kuwasiliana kwa Kiswahili haitoshi, ujuzi au utaalamu ndio unaohitajika.

Jambo jingine la msingi ni kwamba, ajira za namna hiyo licha ya kumtaka mtu kujua maarifa ya isimu na fasihi ya Kiswahili, mhusika anatakiwa kuwa na utaalamu wa lugha ya/za kigeni mathalani Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kichina na kadhalika.

Kwa hivyo, tunapaswa kuchukua hatua za makusudi kutaalamikia Kiswahili katika viwango mbalimbali vya elimu. Kadhalika, jitihada binafsi zinahitajika katika kujifunza lugha mbalimbali za kigeni.

Tunadhani kwamba ili kuweza kupata ajira za namna hiyo, kujua Kiswahili pekee kunatosha. Ikumbukwe kuwa wanafunzi hao wa kigeni wana lugha zao.

Ili kurahisisha ufundishaji na mawasiliano mengine, mwalimu au mtaalamu wa Kiswahili, hana budi kujua lugha husika ya kigeni itakayorahisisha mawasiliano katika ufundishaji darasani na nje ya darasa hilo.

Msomaji mmoja wa safu hii aliwahi kumnadi mwanaye kwamba ni mhitimu wa kidato cha nne na angependa kwenda kufundisha Kiswahili nje ya nchi.

Ingawa lengo letu katika makala aliyosoma hata kufikia uamuzi wa kupiga simu halikuwa kutangaza ajira, kwa viwango vya ufundishaji wa Kiswahili kimataifa, kijana hana sifa. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, ajira nyingi zinazotangazwa kuhusu kufundisha Kiswahili nje ya nchi wanaohitajika ni watu wa shahada ya pili, madaktari na maprofesa.

Hilo linaashiria kwamba tunapaswa kujiendeleza katika taaluma za Kiswahili kwa kiwango cha juu. Shahada moja au chini ya hapo haitoshi.

Kadhalika, tukumbuke vilevile kwamba wapo wengine wengi katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki waliotaalamikia Kiswahili na kujua vizuri lugha za kigeni ambao wanawania ajira hizo pia.

Mpenzi msomaji, ikiwa tunashangilia ajira za Kiswahili zinapotangazwa katika mataifa ya kigeni tukiwa na mawazo ya kupata ajira hizo, basi kwa nia ya dhati tujipange.

Columnist: mwananchi.co.tz