Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Waziri mlevi atoa siri ya kuuawa kwa Lumumba-13

86623 Pic+lumumba MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Waziri mlevi atoa siri ya kuuawa kwa Lumumba-13

Sun, 1 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza wa Congo, aliuawa kwa kupigwa risasi saa 3:40 usiku wa Jumanne ya Januari 17, 1961.

Kwa kuwa jioni ya siku hiyo karibu wote walioshiriki mauaji hayo walikuwa wamekunywa na kulewa nyumbani kwa Rais Moise Tshombe wa Katanga, walikuwa wakisemezana wao kwa wao na kuwaambia wengine waliowaamini kuhusu tukio walilolifanya.

Waliokuwa wakisema na wenzao ni Kamishna wa Polisi, Frans Verscheure na Kapteni Julien Gat ambaye alikuwa kamanda wa Kibelgiji aliyeongoza kikosi cha wanajeshi na askari wengine waliokuwa wakiwalinda Lumumba na wenzake.

Saa 5:00 usiku wa Januari 17, watu wote walioshiriki mauaji ya Lumumba walikuwa wanarejea mjini. Ni polisi wachache tu waliobaki wakifukia makaburi ya Lumumba na wenzake wawili kina Maurice Mpolo na Joseph Akito.

Mawaziri wa Jimbo la Katanga waliohudhuria tukio la mauaji hayo waliharakisha kuelekea nyumbani kwa Rais Tshombe wakati Luteni Gabriel Michels, Brigedia Francois Son na wanajeshi wa Katanga wakielekea kwenye nyumba ya Brouwez walimokuwa wakiteswa Lumumba na wenzake.

Kwa upande wake, Kapteni Gat, ambaye alikuwa kamanda wa Kibelgiji aliyekuwa akiongoza kikosi cha wanajeshi na askari wengine waliokuwa wakiwalinda Lumumba na wenzake, alikwenda moja kwa moja kwenye Kambi ya Massart.

Usiku huo yeye na Luteni Michels walikutana kwenye bwalo la jeshi kambini hapo. Walijumuika na wanajeshi wengine wa Ubelgiji. Hata hivyo maofisa wengi wa jeshi hawakukawia sana kwa sababu walihitajika katika maeneo yao ya kazi asubuhi ya kesho yake.

Katika mazungumzo yao, Kapteni Gat alisikika akisema “Kusema kuwa siku yangu imekwenda vizuri leo ni kujidanganya.”

Kamishna wa Polisi, Verscheure, alijikuta anaelemewa na mawazo. Alipoondoka eneo la mauaji, alikwenda moja kwa moja hadi kwenye shamba la Le Pondoir, nje kidogo ya mji wa Elizabethville. Huko alikutana na Carlo (Charles) Huyghe na familia ya Brouwez, mmiliki wa nyumba walimoteswa Lumumba na wenzake.

Mwandishi Ludo de Witte ameandika kuwa Kamishna Verscheure aliposhuka kwenye gari alikuwa akiyumba kama mlevi na suruali yake ilikuwa imetapakaa matope.

Kitabu ‘The Assassination of Lumumba’ kinamkariri Kanali Huyghe akisema Kamishna Verscheure alikuwa akitetemeka sana, na akampigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani (wa Katanga). Kisha hakukawia sana, akaondoka kwenda kuonana na Inspekta Mkuu wa Polisi wa Katanga, Raphael Mumba.

Baadaye Inspekta Mumba alikaririwa akisema Kamishna Verscheure alikuwa akitetemeka sana na hakuwa katika hali ya kawaida. “Alitishwa sana na kilichotukia,” alisema Inspekta Mumba na kudai kuwa alimwambia Lumumba alikuwa mtu wa mwisho kuuawa mbele yake.

Verscheure na Mumba waliondoka pamoja kwenda nyumbani kwa Rais wa Katanga, Tshombe, ambako waliwakuta mawaziri wa Katanga waliokuwa kwenye mauaji ya Lumumba.

Mfanyakazi mmoja wa nyumbani kwa Tshombe alikaririwa akisema mawaziri wa Katanga walijipanga msururu kusafisha damu iliyotapakaa kwenye mikono yao, na kisha wakaanza tena kunywa na kulewa.

Wakati raia wengi wa Katanga wakiwa usingizini, maofisa wengi waandamizi wa jimbo hilo walikuwa wakisherehekea mauaji ya Lumumba waliyoyafanya usiku huo.

Kulipopambazuka, Jumatano ya Januari 18, raia wakaanza kuzungumzia hatima ya mahabusu watatu walioonekana uwanja wa ndege jana yake kabla ya kupelekwa kuteswa na hatimaye kuuawa.

Siku hiyo hiyo, mazungumzo yaliyotawala mitaani yalimhusu Lumumba. Ni wengi sana walijua kuwapo kwa Lumumba katika mji wa Elizabethville lakini ni wachache sana waliojua kuwa mtu waliyemwona jana yake uwanja wa ndege wa Luano tayari alikuwa amekwishauawa usiku wa kuamkia Januari 18.

Kidogo kidogo habari za mauaji ya Lumumba zikaanza kuvuja. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likapata fununu hizo na kuanza kuzichunguza.

Uvumi ulikuwa umeanza kusambaa mitaani kuwa watu hao Lumumba, Akito na Mpolo waliuawa usiku. Uvumi huo ulipoenea sana, maofisa wa Katanga waliitana na kupanga kuitangazia Katanga kuwa mahabusu wako salama.

Baadaye Redio Katanga ikatangaza kuwa mahabusu “waliwasili jioni ya jana na wamepelekwa eneo salama nje ya mji.” Taarifa kwa vyombo vya habari ikatolewa, ikisomeka “Mhaini Lumumba” amehamishiwa sehemu salama zaidi kwa pendekezo la Rais Kasavubu.

Rais Tshombe naye akatoa taarifa yake, ambayo ilitangazwa na redio hiyo. Tangazo la redio lilisema: “Kufuatia uvumi unaosambazwa na vyombo vya habari vya nje, Rais wa Katanga amesema kuwa, baada ya kuwasili Elizabethville, Lumumba hakuteswa na askari wa Katanga wala Wazungu.”

Februari ya mwaka huo, 1961, kwa kuzingatia hali ilivyokuwa Congo, hususan baada ya mauaji ya Lumumba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio Februari 21, kuchukua hatua na kuchunguza mazingira ya kifo cha Lumumba.

Karibu miaka 20 baada ya mauaji hayo Gat, Verscheure na washirika wao walioshiriki katika mauaji ya Lumumba na wenzake wawili walihojiwa na kutoa ushuhuda wa kile walichotenda. Pia Wakongo walioshiriki katika mauaji hayo walihojiwa katika miaka ya 1990.

Gat na Verscheure walieleza kile walichokumbuka na wenzao walitoa simulizi za walichosimuliwa na Gat na Verscheure. Lakini ushahidi mwingi ulikuwa umeshatoweka.

Kilichoonekana kuwa ni ushahidi ni shajara ya Verscheure aliyokuwa akiandika kumbukumbu zake ambako pia alirekodi kifo cha Lumumba kwa kuandika “9.43 L. dead” akimaanisha Lumumba aliuawa saa 3:43 usiku.

Lucas Samalenge, ambaye alikuwa Waziri wa Habari wa Jimbo la Katanga, hakuwa miongoni mwa wale mawaziri watano waliokwenda kwa Tshombe kufanya kikao cha kumuua Lumumba kwa sababu yeye si mmoja wa mawaziri wanaohusika na vita.

Lakini jioni ya siku ile ambayo Lumumba alipelekwa kuuawa, Samalenge alikwenda kwenye baa moja moja maarufu mjini ya Relais, na wakati akilewa alipayuka akisema tayari Lumumba ameshakufa na kwamba amegusa maiti yake. Aliendelea kurudia kauli hiyo hadi polisi walipofika na kuondoka naye.

Kesho yake, Januari 18, mnadhimu wa jeshi la Ubelgiji alimwendea Samalenge akimwomba ampe picha ya Lumumba aliyekamatwa akiwa hai ili waitumie kwa ajili ya vyombo vya habari. Lakini Samalenge aliendelea kuongea kuhusu habari za kuuawa kwa Lumumba.

Akitabasamu, Samalenge alisema, “Huwezi kumpiga picha sasa kwa sababu tayari ameshakufa.” Rais Tshombe aliposikia ‘kupayuka’ kwa waziri wake, Samalenge, alijawa na hasira. Alimpiga marufuku kuhudhuria dhifa yoyote ya kitaifa kwa muda fulani.

Siku moja baada ya kumuua Lumumba, mapema asubuhi ya Januari 18, 1960 Kamishna Verscheure alianza kukumbuka matukio ya usiku uliopita. Alikumbuka alivyowabeba Lumumba na wenzake na kuwarundika kwenye gari kama magunia.

Alikumbuka alivyowapeleka eneo la mauaji hadi alipotoa amri ya kuwaua na jinsi walivyowatupa kwenye mashimo waliyowachimbia kama makaburi yao.

Alikaa ofisini kwake na kumsimulia polisi mwenzake, Gerard Soete, hatua kwa hatua juu ya mambo ya jana yake. Jana yake Soete hakuwa kazini na kwa sababu hiyo hakujua kilichotukia. Alijikuta akimwambia kuwa alilazimishwa kufanya uovu huo.

Kwa upande mwingine, wananchi wa eneo ambalo Lumumba na wenzake waliuawa, walianza kusimuliana namna wavyosikia milio ya risasi usiku wa jana yake.

Wengine walikwenda eneo la tukio kuona makaburi ya watu hao. Katika kaburi moja waliona mkono ukiwa umejitokeza nje ya kaburi la mmoja wa waliouawa.

Itaendelea kesho…

Columnist: mwananchi.co.tz