Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Siku 4 baada ya uhuru, wanajeshi wazua ghasia-3

85273 Lumumbapic MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Siku 4 baada ya uhuru, wanajeshi wazua ghasia-3

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Januari 1960 Wabelgiji walilazimika kuita mkutano katika jiji la Brussels, Ubelgiji, katika mkutano huo maalum ndipo ilipokubaliwa Congo watapewa uhuru wao Juni 30 ya mwaka huo.

Baada ya ghasia zilizozuka Oktoba 23, 1959 na kudumu hadi Oktoba 28, 1959 na baada ya Patrice Lumumba kukamatwa na kuhukumiwa kifungo gerezani baada ya chama chake kusababisha ghasia hizo, Serikali ya Ubelgiji ilichapisha ripoti kuhusu ghasia hizo.

Jumapili ya Novemba 1, 1959 Lumumba alikamatwa na Serikali ya kikoloni na kumhukumu kifungo cha miezi sita gerezani. Tofauti na ilivyodhaniwa awali, kifungo hicho kiliongeza umaarufu wa Lumumba. Katika ghasia hizo iliripotiwa watu 30 waliuawa.

Theodore Trefon katika kitabu ‘Reinventing Order in the Congo: How People Respond to State Failure in Kinshasa’ anasema ghasia zilizokuwa mbaya zaidi katika historia ya Congo ni zile za kati ya Januari 4 na 6, 1959. “Karibu raia wote Waafrika waliingia mitaani kufanya vurugu”. Ghasia hizo zilianza polisi wa Ubelgiji walipovamia mkutano wa chama cha Abako na kuwatawanya wafuasi wake. Kwa mujibu wa andiko linaloitwa ‘The Congo Operation, 1960—63’ la Birendra Chakravorty, zaidi ya watu 100 waliuawa.

Hata kabla ripoti hiyo haijachapishwa, mkutano uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji na kumalizika Jumanne ya Januari 13, 1959 uliamua kwamba wakati wa Congo kupewa uhuru wake umefika.

Mpango wa kuwakabidhi Wakongo Serikali ya kujitawala wenyewe uliandaliwa tangu Desemba 1955 na kutangazwa Februari 1956. Aliyeifanya kazi hiyo ni Profesa wa Ubelgiji kutoka Chuo Kikuu cha Antwerp aliyeitwa Anton Arnold Jozef “Jef” Van Bilsen.

Mpango huo ulipewa jina la “Thirty Year Plan for the Politial Emancipation of Belgian Africa”.

Alipendekeza kuwepo mpango wa miaka 30. Pendekezo hilo la Desemba 1955 aliliita “Mpango wa Miaka 30”. Kwa maneno mengine, ikiwa ushauri wa Profesa Bilsen ungefuatwa, Congo ingejipatia uhuru wake mwaka 1985.

Karibu kipindi chote cha mwaka 1959 Congo iligubikwa na ghasia. Kuona hivyo, Januari 1960 Serikali ya Ubelgiji iliitisha mkutano mjini Brussels ambao vyama vyote vikubwa vya siasa na viongozi wa makabila makubwa ya Congo walihudhuria.

Mkutano huo ulitawaliwa na madai ya “uhuru sasa”. Baada ya shinikizo kuwa kubwa, Ubelgiji waliamua kwa shingo upande kuwapatia Wakongo uhuru wao ifikapo Juni 30 ya mwaka huo.

Wakati wa kampeni za uchaguzi za Aprili 1960 vyama vingi viligombea viti vya ubunge. Vyama vikubwa vilivyoshiriki uchaguzi huo ni MNC cha Patrice Lumumba kilichokuwa na sera ya kuiunganisha Congo yote iwe moja, na kingine ni kile cha Joseph Kasavubu cha Alliance des Bakongo (Abako).

Katika uchaguzi uliofanyika kuanzia Mei 11 hadi 25, 1960, Lumumba na waungaji mkono wake walipata ushindi mkubwa wa viti bungeni akifuatiwa na Kasavubu, wakalazimika kugawana madaraka. Kasavubu alikubali kuwa Rais wa nchi na Lumumba akiwa mtendaji mkuu wa serikali, yaani Waziri Mkuu.

Juni 23, 1960 Lumumba aliapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Congo na, Juni 30, 1960, ikawa ndiyo siku ya uhuru wa Congo. Siku hiyo na siku tatu baadaye zikatangazwa kuwa siku za mapumziko ili raia washerehekee uhuru wao.

Katika sherehe hizo kila kitu kilionekana kufanyika katika hali ya amani. Ofisi ya Lumumba ilikuwa na shughuli nyingi huku kukiwa na msururu wa watu kuingia na kutoka huku Lumumba akijishughulisha na ratiba ndefu ya mapokezi ya wageni.

Siku ya uhuru Lumumba alitangaza kuwa Jumapili ya Julai 3 ingekuwa siku ya msamaha wa jumla kwa wafungwa wote. Lakini tangazo hilo halikutekelezwa na Julai 4, Lumumba aliita kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili machafuko ya wanajeshi wa Congo.

Wanajeshi wengi waliokuwa na matumaini makubwa kwamba mara baada ya uhuru kupatikana wangepandishwa vyeo na kuongezewa maslahi, walianza kufanya fujo baada ya kuona matarajio yao hayatimii. Ingawa ilikuwa ndani ya wiki moja tu tangu uhuru kupatikana, baadhi yao waliona kuwa Lumumba hatimizi matarajio yao haraka kama walivyotarajia awali.

Bunge lililokutana katika kikao cha kwanza tangu uhuru na kuanza kazi ya kutunga sheria, kilipiga kura ya nyongeza yao ya mishahara. Lumumba alishtushwa na kitendo hicho cha Bunge lake. Kwa kujua hatari ambayo ingesababishwa na kitendo hicho, Lumumba alikiita “upumbavu wa uharibifu.”

Julai 5,, Kamanda wa Jeshi la Congo, Jenerali Emile Janssens, ambaye alikuwa Mbelgiji, aliwaita maofisa wa jeshi na kuwataka wadhibiti hali ya amani. Alisisitiza kuwa hali ilivyokuwa kabla ya uhuru ndivyo itakavyokuwa baada ya uhuru. Lakini tangazo hilo halikutuliza hasira ya baadhi ya wanajeshi.

Siku iliyofuata yaani Julai 6 ambayo ilikuwa siku ya sita tu baada ya uhuru Lumumba aliwapandisha vyeo askari wa Congo kwa ngazi moja lakini hali ya ghasia ilipozidi kuwa mbaya, Lumumba alimfukuza kazi Jenerali Janssens.

Siku mbili baadaye, Ijumaa ya Julai 8, Lumumba aliwaondoa maofisa wote wa kijeshi wa Ubelgiji na kuweka wa Congo ingawa Wazungu kadhaa waliendelea kubaki jeshini kama washauri.

Julai 9 Balozi wa Marekani Congo, Clare Hayes Timberlake, alituma taarifa kwenda Marekani, akidai Ubelgiji wakiingilia mgogoro wa Congo kutakuwa na maafa.

Julai 10 Ubelgiji walituma wanajeshi kwenda Congo kuwalinda raia wao na biashara zao. Kasavubu na Lumumba waliigeukia Marekani kuomba msaada wa kulipanga upya jeshi la Congo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani ikasema Marekani iko tayari kusaidia lakini chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na uongozi wa Ubelgiji.

Julai 11 Moise Tshombe akatangaza kuwa Jimbo la Katanga limejitenga na Congo na kisha akalitangaza kuwa liko huru huku akiiomba Ubelgiji walitambue na wapewe misaada.

Jumanne, Julai 12 Kasavubu na Lumumba waliiomba Marekani msaada kudhibiti uchokozi wa Wabelgiji na siku hiyo hiyo baraza la mawaziri lilikutana bila Lumumba na Kasavubu kuwapo kwenye kikao, na wakaomba wapewe wanajeshi 3,000 wa Marekani.

Rais wa Marekani, Dwight David Eisenhower, aliamuru vikosi vya nchi yake, vikiwa na zana za kivita, kwenda Congo ikiwa Waziri Mkuu wa Urusi, Nikita Krushchev, angetuma majeshi yake kwenda huko.

Jumatano, Julai 13, Urusi iliutaka Umoja wa Mataifa kuzuia uchokozi wa Ubelgiji nchini Congo. Alhamisi ya Julai 14 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kupeleka jeshi Congo. Siku hiyo hiyo Lumumba na Kasavubu wakawasiliana na Urusi na kuwaomba wafuatilie hali ya Congo. Urusi ilikubali.

Itaendelea kesho...

Ijumaa, Julai 15, majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliwasili Congo. Julai 16, baada ya kukutana na Lumumba, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Congo, Ralph Bunche, aliripoti “Lumumba alikuwa kama kichaa na alitenda mambo kwa tabia za kitoto.” Lumumba na huyo Bunche hawakuelewana vizuri.

Baada ya hali kuzidi kuwa mbaya, Jumapili ya Julai 17 Lumumba alitishia kuwa atayaita majeshi ya Urusi ili yasaidie kuyaondoa majeshi ya Umoja wa Mataifa kama watashindwa kuyaondoa majeshi ya Ubelgiji ndani ya saa 72.

Columnist: mwananchi.co.tz