Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961:Patrice Lumumba auawa kwa kupigwa risasi-12

86524 Lumumbapic MAUAJI YA LUMUMBA 1961:Patrice Lumumba auawa kwa kupigwa risasi-12

Sat, 30 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakiwa wanashikiliwa katika nyumba ya mkulima Lucien Brouwez ambako walipelekwa na Kamishna wa Polisi Frans Verscheure, Rais wa Katanga, Moise Tshombe, alikuwa akisubiri kupashwa habari kuhusu mahabusu hao.

Kufikia wakati huu, wasaidizi wa Tshombe walikuwa wameshamfikishia taarifa kuwa Patrice Lumumba na wenzake wawili wameshaletwa Katanga na sasa wanashikiliwa katika nyumba maalumu.

Tshombe, ambaye alikuwa katika jumba lake la kifahari akitazama sinema iliyoitwa ‘Liberte’, aliahirisha kuendelea kuangalia sinema hiyo.

Muda mfupi baadaye aliita kikao cha dharura cha baadhi tu ya mawaziri wake. Kikao hicho kilihudhuriwa na mawaziri watano tu na kilifanyika saa 12 jioni. Mmoja wa waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Katanga, Godefroid.

Baada tu ya kupewa taarifa kuwa anahitajika kwa Tshombe, Munongo aliwaacha akina Lumumba wakiendelea kuteswa na watesi wao na yeye akaenda kuhudhuria hicho kikao cha dharura. Rais Tshombe alikuwa akiishi umbali wa kiasi cha maili sita kutoka eneo walimokuwa wameshikiliwa Lumumba na wenzake wawili.

Kikao hicho hakikuzidi dakika 90, kilikaa kuanzia saa 12:30 jioni na kumalizika saa 2:00 usiku. Munongo na Tshombe tayari walishaamua la kufanya juu ya mateka wao.

Azimio lao la mwisho lilikuwa ni lazima Lumumba, Mpolo na Okito wafe. Lazima wauawe. Kwa kuwa wawili hao walikuwa wamefikia uamuzi wa kuwaangamiza Lumumba na wenzake wawili, ndipo walipoita kikao cha baraza la mawaziri wake na kuwashirikisha nia yao hiyo.

Saa 11:45 kikao cha ‘baraza la mawaziri’ kiliitwa na kikaanza saa 12:30. Muda huo miogoni mwa watawala wakubwa wa Katanga-Muongo, Kibwe na Kitenge walikuwa njiani kwenda kwenye nyumba ya Brouwez na Kazadi, Mukamba na Zuzu walikuwa nyumbani kwa Tshombe.

Huu haukuwa mkutano wa kawaida wa baraza la mawaziri. Baadhi ya mawaziri waandamizi hawakuwapo, lakini baadhi yao ambao hawakuaminika huko Elizabethville walikuwapo.

Pombe ilikuwa inanyweka kwa wingi. Watu walikuwa wanakuja, wanakula na kuondoka ... muda mfupi kabla ya saa 12:30 jioni, Tshombe mwenyewe, akiongozana na Munongo na Kibwe, wakaondoka kwenda kuwaona mabahusu kabla ya kurudi na kuendelea na kikao.

Baadaye jioni hiyo hiyo, ujumbe kutoka Leopoldvile ulikwenda kupata chakula cha jioni na Cleophas Mukeba, ambaye alikuwa ni mmoja wa mawaziri wa Katanga. Inaelekea sherehe za kifo cha Lumumba zilianza mapema.

Kabla ya saa 2 usiku Kamishna wa Polisi, Frans Verscheure alipokea simu akiwa ofisini kwake. Simu hiyo ilipigwa kutoka nyumbani kwa Tshombe. Kwa kuwa umbali kutoka kituo cha polisi hadi kwa Tshombe haukuwa mrefu, Kamishna Verscheure alitembea kwa mguu kuelekea nyumbani kwa Tshombe.

Akiwa huko aliambiwa waingie kwenye gari na maofisa kadhaa wa Kiafrika kwenda kwenye nyumba ya Brouwez walimokuwa wanashikiliwa Lumumba na wenzake.

Muda mfupi baadaye kikundi cha mawaziri kiliondoka nyumbani kwa Tshombe, akiwamo Tshombe mwenyewe, na kwenda kwenye nyumba hiyo. Baadhi ya mawaziri hao ilikuwa ni mara yao ya pili kufika kwenye nyumba hiyo kuwaona Lumumba na wenzake.

Kwa mara nyingine tena walishiriki kuwatesa na kuwadhalilisha. Jean- Baptiste Kibwe, ambaye alikuwa waziri wa fedha wa jimbo la Katanga, alikuwa akitishwa sana na msimamo wa Lumumba, na kwa sababu hiyo alimchukia sana. Kisha akamtamkia Lumumba kuwa yeye ni msaliti na kwamba kifo chake kitasherehekewa sana na watu wa Katanga kesho yake.

Ripoti ya Kamishna Verscheure iliyopatikana miaka 40 baadaye imetaja kauli za Kibwe kwa Lumumba. Ripoti hiyo ilisema majira ya saa moja jioni, hata kabla ya kile kikao cha dharura kilichoitwa na Tshombe, Jean- Baptiste Kibwe alisikika akimtamkia Lumumba kwamba “punde tu utakufa wewe.”

Hamu ya kuwaangamiza watatu hao Lumumba, Mpolo na Okito ndiyo pekee iliyowaondolea mateso waliyokuwa wanayapata kutoka kwa watesi wao. Baadaye mawaziri hao waliondoka eneo hilo.

Nje ya nyumba hiyo, kiasi cha saa 2:30 usiku, na kama ilivyokuwa imeamriwa, Kamishna Verscheure aliwachukua Lumumba, Mpolo na Okito na kuwarundika kwenye kiti cha nyuma cha gari lake.

Gari liliondolewa eneo hilo na ikaelezwa kuwa wanaelekea gereza la Jadotville, umbali wa kiasi cha maili 80, mahali lilipokuwa gereza la kuwarekebisha wafungwa.

Waliokuwamo katika msafara huo, kwa mujibu wa mwandishi Ludo de Witte, ni Tshombe mwenyewe, baadhi ya mawaziri wa Katanga, maofisa watatu wa kijeshi wa Ubelgiji na kamishna wa polisi wa Kibelgiji.

Lakini badala ya kuelekea gereza la Jadotville kama ilivyosemwa awali, wawili hao Julien Gat na Frans Verscheure wakashika njia nyingine kuelekea eneo ambalo kikosi cha mauaji kingefanya kazi yake.

Walichepuka na kuelekea kwenye kijiji cha Mwadingusha. Kwa kuwa ulikuwa ni usiku wa giza totoro, mwanga pekee ulioonekana kwa wakati huo ni taa za magari waliyotumia.

Kapteni Julien Gat ni kamanda wa Kibelgiji aliyekuwa akiongoza kikosi cha wanajeshi na askari wengine waliokuwa wakiwalinda Lumumba na wenzake.

Walipowasili katika kijiji hicho walikuta tayari makaburi ya Lumumba na wenzake yalikuwa yameshachimbwa na askari wa kikosi cha mauaji waliotangulizwa eneo hilo. Lumumba na wenzake wawili walikuwa wanatembezwa pekupeku wakiwa wamevaa suruali zao na fulana tu.

Askari wa eneo hilo waliokuwa wakipokea amri kutoka kwa shemeji yake Munongo nao waliingia katika operesheni hiyo ya mauaji ya Lumumba. Katika giza hilo, wakimulikiwa na taa za magari ya kijeshi yaliyokuwa kwenye msafara huo, Julien Gat na Frans Verscheure, pamoja na maofisa wawili Wazungu ambao walikuwa na vyeo vya chini kuliko hao Wabelgiji, walisimama kando kutoa amri kwa askari hao wa Kafrika waliokuwa chini ya shemeji yake Munongo.

Tshombe, Munongo, Kibwe na maofisa wengine wa serikali ya Katanga walisubiri kushuhudia mauaji hayo. Kamishna Verscheure alimsukuma kila mateka mmoja na kumsogeza karibu na kaburi lake. Kila mateka Lumumba, Mpolo na Okito alikuwa akipangiwa askari wanne wenye silaha tayari kwa kuwafyatulia risasi.

Wakati Verscheure akimsukuma Lumumba, yeye Lumumba alimuuliza: “Umekuja kutuua? Sivyo?” Kamishna Verscheure akajibu, “Ndiyo.”

Ndipo Julien Gat akatoa amri kwa kila kikundi cha askari wanne kumfyatulia kila mmoja risasi. Lumumba, Mpolo na Okito wakauawa mmoja baada ya mwingine.

Walikuwa wakichukuliwa mmoja mmoja kutoka kwenye gari. Kila mmoja alipelekwa mbele ya kaburi lake, akapigishwa magoti, akaambiwa asali, na kisha akapigwa risasi na kutumbukia shimoni.

Lumumba alikuwa wa mwisho kuuawa, baada ya kumiminiwa risasi na askari wa Kiafrika kwa amri ya ofisa wa Ubelgiji. Kila aliyekuwa akipigwa risasi alikuwa akitumbukia kwenye shimo lililochimbwa kama kaburi lake.

Mwandishi Iam A. Freeman, katika kitabu ‘Seeds of Revolution: A Collection of Axioms, Passages and Proverbs’ (Volume 2, uk. 192) ameandika: “Lumumba alikuwa wa mwisho kuuawa. Lumumba alipiga magoti kusali. Askari wa Kiafrika aliyeamriwa kumuua alikataa kumfyatulia risasi, ndipo ofisa wa jeshi wa Ubalgiji, Kanali Charles Huyghe, alipochomoa bastola yake iliyokuwa kiunoni na kumpiga Lumumba risasi yeye mwenyewe.”

Kwa kutumia bastola yake, Kanali Huyghe ndiye aliyefyatua risasi iliyohitimisha uhai wa Patrice Emery Lumumba.

Baadhi ya askari waliwafukia kwa udongo na mchanga. Kisha waliondoka haraka eneo hilo. Walikuwa na haraka ya kuondoka kiasi kwamba waandishi Emmanuel Gerard na Bruce Kuklick katika kitabu chao, ‘Death in the Congo: Murdering Patrice Lumumba’ wanasema waliacha hata silaha nyingine zikiwa zimekwama kwenye matope.

Itaendelea kesho…

Columnist: mwananchi.co.tz