Alhamisi ya Juni 30, 1960, Congo ilijipatia uhuru kutoka kwa Ubelgiji. Waziri Mkuu Patrice Emery Lumumba akiwa na miaka 35, akawa kiongozi wa jamhuri hii mpya. Lakini hali ya amani na utulivu ikatoweka muda mfupi baadaye. Kikosi cha majeshi ya waasi kikazua vurugu kiasi kwamba Ubelgiji ilipeleka jeshi lake kulinda raia wake.
Siku chache baadaye, Jumatatu ya Julai 11, ya mwaka huo, Jimbo la Katanga, lililokuwa likiongozwa na Moise Kapenda Tshombe likajitenga. Umoja wa Mataifa ukaingilia kati kwa kutuma jeshi la kulinda amani.
Jumanne ya Januari 17, 1961, miezi sita tu baada ya uhuru wa Congo, Patrice Lumumba aliuawa katika Jimbo la Katanga. Februari 13, maofisa wa Jimbo la Katanga wakatangaza kifo cha Lumumba, lakini hakuna aliyewaamini. Hata wao hawakuziamini taarifa walizotoa. Lawama zikaanza kumiminika kutoka pande zote za dunia.
Urusi iliwashutumu mabeberu na kuitaka Marekani iondoe watu wake Congo, pia ikamtaka aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjold, kujiuzulu kwa sababu alionekana kuwa kibaraka wa wakoloni.
Katika jiji la Moscow nchini Urusi watu waliandamana baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa Lumumba. Katika jiji la Beijing, China, kulifanyika maandamano makubwa ya watu waliokadiriwa kuwa zaidi ya 100,000. Katika nchi mbalimbali raia walivamia balozi za Ubelgiji na kufanya uharibifu.
Ndani ya mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Lumumba, Umoja wa Mataifa ulifanya uchunguzi na baadaye ikabainika kuwa hata Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) lilishiriki katika njama za kumuua Lumumba.
Katika ukurasa wa 198 wa kitabu “The African Liberation Struggle: Reflections” cha Godfrey Mwakikagile, jasusi wa Marekani, Stephen Andrew Lucas, ambaye alikuja Tanzania na kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa Congo na kufanya kazi chini ya mkuu wa CIA, Larry Devlin, wakati Lumumba alipokamatwa na kuuawa. Mwingine aliyekuwa Congo na baadaye akaenda Zanzibar ni Frank Carlucci.
Pamoja na Lumumba walikuwako wengine wawili waliokamatwa na kuuawa pamoja naye; Joseph Okito (alikuwa Naibu Spika wa Bunge la Congo) na Maurice Mpolo (alikuwa Waziri wa Vijana na Michezo). Watatu hao walisafirishwa kwa ndege kutoka Kinshasa hadi mji mkuu wa Kalonji wa Bakwanga (sasa unaitwa Mbuji-Mayi).
Wakiwa kwenye ndege aina ya DC-3, wote watatu waliteswa kikatili na walinzi wa Congo. Ndege ilipowasili anga la Bakwanga, rubani hakuweza kutua kwa sababu uwanjani hapo kulikuwa kumetapakaa matanki ya ujazo wa galoni 55.
Rubani aliamua kwenda kutua Uwanja wa Elisabethville (sasa Lubumbashi), na ndege ilipotua, Lumumba alikuwa anakaribia kuzirai kutokana na maumivu.
Ndani ya ndege walikuwa wakiteswa mbele ya Kamishna wa Ulinzi wa Congo, Ferdinand Kazadi na Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Congo, Jonas Mukamba. Walipofikishwa Lubumbashi walipelekwa kwenye nyumba jirani na Uwanja wa Ndege wa Luano na kuendelea kuteswa.
Lumumba, ambaye uso wake uliharibiwa kiasi cha kutotambulika kutokana na vipigo na nguo zake zikiwa zimetapakaa damu, alisimamishwa kwenye kichuguu kikubwa huku akimulikwa na taa za magari.
Kwa amri ya Moise Tshombe, rais wa jimbo la Katanga ambaye naye alikuwa akipokea maelekezo kutoka Brussels, Lumumba aliteswa. Kikosi cha mauaji kilimtoa Lumumba katika nyumba alimokuwa akiteswa na kumsafirisha kwa mwendo wa dakika 45 hadi Katanga.
Hapo aliuawa na kikosi cha mauaji kwa kupigwa risasi kwa amri ya Kapteni wa Ubelgiji, Julien Gat. Aliyemfyatulia risasi ni askari wa Ubelgiji, kanali Carlos Huyghe. Mwingine aliyeshiriki kuwafyatulia risasi na kuwaua Okito na Mpolo ni kapteni Julien Gat.
Baada ya kuuawa kwa risasi, miili ya watatu hao ilizikwa eneo walilouawa. Kwa hofu kwamba kaburi la Lumumba lingegundulika na baadaye lingeweza kugeuzwa kuwa eneo la heshima, Wabelgiji na vibaraka wao waliamua kupoteza ushahidi ambao ungeweza kuelekeza uliko mwili wake.
Jumatano ya Januari 18, ikiwa ni siku moja baada ya mauaji hayo, miili ya kina Lumumba ilifukuliwa na kupelekwa ndani zaidi msituni na kuzikwa upya karibu na mpaka wa Rhodesia (Zimbabwe) na Congo.
Usiku wa Jumapili ya Januari 22 ndugu wawili wa Ubelgiji Kamishna wa Polisi wa Ubelgiji, Gerard Soete na ndugu yake walikwenda tena kufukua miili ya Lumumba, Okito na Mpolo. Safari hii walikuwa na shoka na misumeno.
Waliikatakata miili hiyo vipande vipande kabla ya kuyeyusha mabaki yake kwa tindikali iliyokuwa imejaa kwenye pipa la petroli la lita 200. Baadaye Soete alikiri kwamba alitumia koleo kung’oa meno mawili ya Lumumba kwa ajili ya ukumbusho.
Katika kitabu cha “Encyclopedia of leadership: A-E” (ukurasa 925), George R. Goethals na Georgia Sorenson wanasema mpango wa kumuua Lumumba uliitwa ‘Operesheni Barracuda’ na uliandaliwa na Marekani, hususan CIA, ndipo Lumumba akakamatwa na Kanali Mobutu Oktoba 10, 1960.
Katika kikao kilichofanyika jijini Washington, Marekani iliamriwa Lumumba aondolewe madarakani na awekwe kiongozi ambaye angekubali kulinda maslahi ya Wamarekani nchini Congo.
Maagizo hayo yakatumwa kwa mkuu wa CIA nchini Congo, Lawrence Raymond Devlin. CIA wakaunganisha nguvu zao na Ubelgiji.
Agosti 1960, msaada wa kijeshi kutoka Urusi uliingia Congo, jambo ambalo halikuwapendeza Wamarekani na Wabelgiji. Ilikuwa lazima Lumumba aondoke kwa gharama zozote.
Ndipo wakamshawishi Rais wa Congo, Joseph Kasavubu, lakini waligonga mwamba. Devlin akaripoti taarifa hizo makao makuu ya CIA jijini Langley, Marekani, Agosti 24, 1960.
Dk Sidney Gottlieb, mtaalamu wa dawa, akapewa maagizo ya kutafuta sumu ya kumuua Lumumba na isijulikane kuwa Marekani imehusika, na iwe ni dawa ambayo chanzo chake ni Afrika.