Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961:Mipango ya kumhamisha Lumumba gereza yaiva-10

86275 Lumumbapic MAUAJI YA LUMUMBA 1961:Mipango ya kumhamisha Lumumba gereza yaiva-10

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Lumumba akiwa bado mikononi mwa watesi wake, Rais Kasavubu wa Congo alikuwa kwenye shinikizo kali kuhusu hatima ya Lumumba.

Kwa kuona hivyo, Januari 2, 1961, Kasavubu aliitisha mkutano ambao ungewajumuisha wanasiasa mbalimbali wa Congo. Pia wanasiasa wa Afrika na Asia waliokuwa wafuasi na watetezi wa Lumumba, walikuwa wanakutana Casablanca wakitaka aachiwe mara moja.

Kuongezea uzito wa hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dag Hammarskjold alipanga kurudi tena Congo Januari 10. Viongozi wa kisiasa wa Congo waliogopa kwamba kama wangemwachia huru Lumumba, huenda UN wangeshinikiza arudi madarakani.

Mapema asubuhi ya Januari 13, nidhamu katika kambi ya Camp Hardy ilianza kutoweka. Wanajeshi wa kambi hiyo walikataa kupokea amri yoyote kutoka kwa wakubwa zao hadi walipwe stahiki zao, baadhi yao wakitaka Lumumba aachiwe huru.

Baadaye siku hiyo hali ilivyozidi kuwa mbaya Kasavubu, Mobutu, Bomboko na Nendaka waliitana na haraka kuelekea kambini kujadiliana na wanajeshi hao.

Baadaye ukazuka uvumi kwamba Januari 14, Lumumba angekuwa huru na hivyo wanajeshi wanaomtii waliokuwa Katanga wangekuwa njiani kuelekea Kinshasa.

Wanajeshi waliokuwa Katanga tayari walishateka eneo lote la kaskazini hata kabla machafuko ya Thysville. Viongozi walishahamishia familia zao Brussels, Ubelgiji.

Januari 13, mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) nchini Congo, Lawrence Raymond Devlin, alituma ujumbe Marekani akisema serikali ya Congo inaweza kuanguka wakati wowote na kama Marekani hawatachukua hatua za haraka, maslahi yake nchini humo yatakuwa hatarini. Nchini Ubelgiji, mikutano ya haraka ilifanyika kuhusu hali ya kisiasa ya nchi hiyo.

Mwandishi wa habari, Kwame Afadzi Insaidoo katika ukurasa wa sita wa kitabu chake cha “Ghana: A Time to Heal & Renew the Nation” amelikariri jarida la The Economist la Februari 24-Machi 2, 2007, Vol. 382, No. 8517, ukurasa wa 95, kuhusu maendeleo ya hali nchini Congo.

“Bw. (Larry) Devlin alikula njama na mkuu wa jeshi la nchi, Joseph Mobutu, ambaye ni sajini aliyepandishwa cheo hivi karibuni, kumkamata Waziri Mkuu (Lumumba),” ameandika akinukuu jarida hilo.

Wakati Lumumba alipozidi kusababisha matatizo na nchi ikatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, Rais Dwight Eisenhower (wa Marekani) alitoa amri ya kumuua Lumumba, kwa mujibu wa Bw. Devlin.

Kwa mujibu wa kitabu “Betrayal of Trust: The Collapse of Global Public Health” cha Laurie Garrett, uamuzi wa Marekani kumuua Lumumba ulikuja baada ya mawasiliano ya mara kwa mara kati ya mkurugenzi mkuu wa CIA, Allen Dulles na mkuu wake katika kituo cha Congo, Larry Devlin.

Katika taarifa moja ya telegramu iliyotumwa Marekani, Devlin aliripoti kuwa “kuna jitihada za kuifanya Congo kuwa ya kikomunisti”.

Katika mkutano wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, ilitengenezwa mipango ya kuivuruga Congo kwa kutengeneza ghasia za mara kwa mara kiasi cha Lumumba kushindwa kutawala.

Kubwa zaidi lililofanyika ni kupandikiza mgogoro wa uongozi ambao hatimaye ulimfanya Lumumba kupoteza cheo chake.

Ghasia zilikuwa za mara kwa mara katika miji mingi ya Congo. Ghasia za Camp Hardy ziliwasukuma maofisa wa Congo kumhamishia Lumumba sehemu nyingine. Baadhi ya wanasiasa wa Katanga, Kasai na Kinshasa walihakikisha wanazuia njia zozote za kumwachia Lumumba.

Mipango ya kumtoa Lumumba mjini Kinshasa kwenda Katanga ilikamilika. Jimbo la Katanga lilikuwa linaongozwa na mmoja wa mahasimu wake kisiasa, Moise Tshombe.

Walioongoza kikao cha mipango ya kumhamisha ni Kandolo Damien na Andre Lahaye, Mbelgiji aliyekuwa mshauri mkubwa wa mkuu wa Idara ya Usalama Congo, Victor Nendaka.

Nendaka alikuwa ofisini kwake mjini Kinshasa wakati Kandolo alipomwendea akiwa na waraka ulioonyesha ratiba ya ndege itakayotumika. Andre Lahaye naye alikwenda ofisini kwa Nendaka alikokutana tena na Kandolo.

Kabla ya hapo, Jumanne ya Desemba 6, 1960, Kanali Joseph Mobutu aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwaambia kuwa Lumumba yuko katika mikono salama.

Aliwaonyesha waandishi hao kile alichosema kuwa ni cheti cha daktari kinachoonyesha kuwa Lumumba yuko katika hali njema sana kiafya.

Aliwaambia Lumumba atashtakiwa kwa kosa la kusababisha ghasia katika jeshi na kuwatesa baadhi ya wabunge. Mobutu hakutaja tarehe ambayo Lumumba angeshtakiwa.

Januari 16, mkuu wa kikosi cha usalama, Victor Nendaka Bika, alikutana na wanasiasa wa Congo katika ofisi za Shirika la Ndege la Ubelgiji, Sabena, na kupanga kuwa watamhamisha Lumumba kutoka Bakwanga na kumpeleka Elizabethville.

Operesheni hiyo ingefanyika jioni. Hiyo ilikuwa ni siku moja kabla ya mauaji ya Lumumba. Wanasiasa wawili Fernand Kazadi na Jonas Mukamba walitakiwa washiriki kumsafirisha Lumumba.

Kushikiliwa kwa Lumumba kulianza kuitisha Ubelgiji tangu siku ile majeshi ya Mobutu yalipozingira makazi yake. Uvumi ulisambaa kwamba jimbo la Katanga lilitaka kubadilishana wafungwa na Kinshasa na kwamba Lumumba angekuwemo.

Uliposambaa sana uvumi huo, Waziri wa Mambo ya Afrika nchini Ubelgiji, Harold d’Aspremont Lynden aliwasiliana na maofisa wa serikali yake waliokuwa Congo akiwataka wazuie mazungumzo hayo.

Jumapili ya Januari 14, msiri na mtu wa karibu na Lynden aliyejulikana kwa jina la Meja Jules Loos, na ambaye ni mmoja wa walioshiriki njama za kumuua Lumumba, kwa mujibu wa kitabu “Patrice Lumumba, Ahead of His Time” cha Didier Ndongala Mumbata, alimpelekea Lynden mbinu nyingine za “kumalizana na Lumumba”.

Hiyo ni baada ya kukerwa na magazeti ya Congo kuhusu maasi ya kijeshi ya Thysville ambako Lumumba alikuwa anashikiliwa.

Loos alimshauri Luteni Kanali Louis Marliere, ofisa wa kijeshi wa Ubelgiji nchini Congo kumpeleka Lumumba Katanga kwa hasimu wake, Moise Tshombe.

Lynden alituma ujumbe wa siri kwa Luteni Kanali Marliere na Meja Loos akiwataka wahakikishe Lumumba anaondolewa na wampeleke sehemu nyingine ya siri, lakini yenye ulinzi mkali zaidi.

Januari 16 alimtumia Tshombe ujumbe akimsihi amchukue Lumumba na amshikilie huko Katanga. Hata hivyo ujumbe huo ulifika jioni wakati Tshombe alishafanya uamuzi wake.

Mipango ya kumpeleka Lumumba Katanga iliandaliwa Kinshasa. Tshombe alikubaliana nayo. Mmoja wa maofisa wa serikali aliyeidhinisha kuhamishwa kwa Lumumba na kupelekwa Katanga ni Albert Delvaux, ambaye awali alikuwa waziri wa Lumumba kabla ya mgogoro wa uongozi na alikuwa pia ni mmoja wa maofisa wa Kasavubu waliosaini kuondolewa kwa Lumumba na Justin Marie Bomboko mwaka 1960.

Baadaye Delvaux alikuwa waziri katika baraza la mawaziri la Joseph Ileo ambaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa Congo.

Katika kipindi chote cha mwanzoni mwa Januari 1961, Delvaux alikuwa na harakati nyingi za kuwaweka pamoja akina Kasavubu, Tshombe na Mobutu kuhusu suala zima la Lumumba.

Asubuhi ya Januari 16, wakati mshauri wa Kasavubu wa masuala ya usalama, Andre Lahaye na mkuu wa shirika la huduma za kijasusi la kikoloni, Victor Nendaka, wakijadiliana namna ya kumsafirisha Lumumba kumpeleka Katanga, aliyekuwa akisimamia mawasiliano baina ya Tshombe na Kasavubu ni Delvaux.

Hatimaye jioni ya Jumatatu ya Januari 16, muda mfupi baada ya tafakuri na majadiliano mengi, Nendaka alipanda ndege kuelekea mjini Thysville (sasa ni Mbanza-Ngungu) alikokuwa anashikiliwa Lumumba. Usiku wa siku hiyo alilala katika hoteli mojawapo ya mji huo.

Itaendelea kesho…!

Columnist: mwananchi.co.tz