Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Majasusi waanza kumshughulikia Lumumba-4

85381 Pic+lumumba MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Majasusi waanza kumshughulikia Lumumba-4

Sat, 23 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ijumaa, Julai 15, majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliwasili Congo. Julai 16, baada ya kukutana na Lumumba, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) Congo, Ralph Bunche, aliripoti, “Lumumba alikuwa kama kichaa na alitenda mambo kwa tabia za kitoto.” Lumumba na Bunche hawakuelewana vizuri.

Baada ya hali kuzidi kuwa mbaya, Jumapili ya Julai 17 Lumumba alitishia kuwa atayaita majeshi ya Urusi ili yasaidie kuyaondoa majeshi ya Umoja wa Mataifa kama watashindwa kuyaondoa majeshi ya Ubelgiji ndani ya saa 72.

Hali ya utulivu na amani ilipozidi kudorora Congo katika zile siku chache baada ya uhuru, Lumumba aliwatishia Umoja wa Mataifa kuwa atayaita majeshi ya Urusi ili yamsaidie kulinda amani Congo na kujikuta akirushiana maneno na Bunche.

Jumamosi Julai 9, 1960, ikiwa ni siku tisa tangu ijipatie uhuru, Serikali ya Congo ilibadili jina la jeshi kutoka ‘Force Publique’ na kuwa ‘Armee Nationale Congolaise’ (ANC). Baraza la Mawaziri lilimteua Victor Lundula, mwafrika aliyepigana katika Vita Kuu II ya Dunia, kuwa jenerali wa kwanza mkuu wa majeshi ya Congo na kuchukua nafasi ya Jenerali Emile Robert Alphonse Janssens ambaye alikuwa Mbelgiji.

Lumumba alimteua pia Joseph-Desire Mobutu kuwa mmoja wa mawaziri wadogo katika ofisi ya Waziri Mkuu, kama kanali na mnadhimu mkuu wa ANC.

Kitabu ‘The Congo: From Leopold to Kabila: A People’s History’ cha Georges Nzongola-Ntalaja katika ukurasa wa 98 kinasema uteuzi wa watu hao wawili Lundula na Mobutu ulitolewa vibaya.

“Lundula hakuwa na sifa zinazohitajiwa kuendesha jeshi la nchi, hususan jeshi jipya. Na kwa Mobutu, Lumumba alifanya kosa kubwa kwa kuamini tu kwamba ana uwezo wa kusimamia jeshi kwa vile aliweza kuwasimamia watu wachache waliomzunguka.”

Kitabu hicho kinasema “(Lumumba) hakusikiliza uvumi uliosambaa uliodai Mobutu alikuwa wakala wa majasusi wa Ubelgiji na Marekani. Kwa kumteua Mobutu kushika wadhifa huo, tayari (Lumumba) alikuwa amemchagua Yuda wake mwenyewe.”

Mwandishi wa historia, Didier Ndongala Mumbata, alilifafanua zaidi katika kitabu ‘Patrice Lumumba, Ahead of His Time’. Mumbata anaandika kuwa matukio ya kati ya Julai na Septemba 1960 yalibadili sana uhusiano wa Lumumba na baadhi ya mawaziri wake na wanasiasa wenzake. Alionekana kupigana vita mwenyewe.

Mambo yalipokuwa mazuri alizungukwa na marafiki na ‘wapongezaji’ wengine wa kweli na wa uongo. Mambo yalipokwenda mrama alijikuta yuko mwenyewe.

Mobutu, ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu na ambaye awali alimteua kuwa msaidizi wake katika chama chake cha MNC, kisha akamwingiza serikalini baada ya kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Congo, na baadaye akamfanya kuwa mnadhimu mkuu wa jeshi la Congo, alimsaliti na kujiunga na kambi ya Joseph Kasavubu. Wote wawili, Kasavubu na Mobutu walishiriki kwa kiasi kikubwa kumwangusha na kumuua Lumumba.

Familia ya Lumumba ilimjua sana Mobutu. Lumumba alikutana na Mobutu wakati yeye (Mobutu) akisomea uandishi wa habari mjini Brussels, Ubelgiji.

Mobutu na Lumumba walikuwa na matamanio yaliyokaribia kufanana. Walitamani kuona Congo iliyo na umoja, walichukia kutawaliwa na wageni. Kwa ushawishi wa Lumumba, Mobutu aliingia katika siasa za Congo kupitia MNC. Mobutu alifanya kazi kama katibu muhtasi wa Lumumba. Yeye ndiye aliyeamua nani aonane na Lumumba na kwa muda gani.

Mwandishi Mumbata anasema kwa ujumla Mobutu ndiye aliyekuwa anapanga ratiba yote ya shughuli za kisiasa za Lumumba.

Nyumbani kwa Lumumba kulikuwa kama nyumbani kwa Mobutu kwa sababu aliweza kwenda huko wakati wowote kadri alivyotaka na alikuwa akijihudumia vyakula na vinywaji kadri alivyoweza.

Sehemu kubwa ya maisha yake ya kikazi siku za mwanzo za harakati za siasa za Congo kuelekea siku ya uhuru, Mobutu alikaa nyumbani kwa Lumumba. Hii ilimfanya awe karibu zaidi na Lumumba kuliko mwanasiasa yeyote duniani.

Katika ukurasa wa 2562 wa kamusi ‘The 20th Century Go-N: Dictionary of World Biography, Volume 8’ iliyohaririwa na Frank Magill, inasimuliwa kuwa Lumumba alimwamini sana Mobutu.

Mwandishi Didier Mumbata anasimulia: “Lumumba aliwaamini watu kirahisi, na haraka. Alikuwa mwema, alikuwa akimwambia mkewe kuwa Mobutu alikuwa rafiki yake sana na nyumbani kwake (Lumumba) ni nyumbani kwa Mobutu.

Lumumba alijua fika kuwa Mobutu alihitaji sana fedha kuikimu familia yake, lakini alikuwa akimwambia asijaribu kuisaliti Congo na watu wake kwa sababu ya fedha. Lakini Mobutu, kama alivyokuwa Yuda kwa Yesu (Kristo), alikuja kumsaliti rafiki yake huyo kwa Wabelgiji na Wamarekani.”

Hata hivyo, lilipokuja suala la kupata msaada wa kijeshi kutoka Urusi ili isaidie kuyaondoa majeshi ya Ubelgiji nchini Congo, ndipo Rais Kasavubu na Mobutu walipoungana kumpinga Lumumba.

Lumumba alipoona hapati msaada wa haraka kutoka majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, Julai 17, 1960 alitishia kuyaita majeshi ya Urusi ili yasaidie kuyaondoa ya Umoja wa Mataifa kama watashindwa kuyaondoa majeshi ya Ubelgiji ndani ya saa 72.

Baadaye siku hiyo, Lumumba alitoa tishio jingine. Akasema ikiwa majeshi ya Umoja wa Mataifa hayatayaondoa majeshi ya Ubelgiji kabla ya Julai 20, watalazimika kuyaita majeshi ya Urusi kuwaondoa wao.

Julai 22, malori 100 ya kijeshi kutoka Urusi yaliwasili Congo, lakini hayakukabidhiwa jeshi la Umoja wa Mataifa. Katika Mkutano wa Usalama wa Taifa (NSC) nchini Marekani, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), Allen Dulles, aliwaambia wenzake mkutanoni kuwa alihisi “Lumumba amenunuliwa na Wakomunisti”. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Rais Dwight Eisenhower.

Julai 27, akiwa Umoja wa Mataifa, kwa mara nyingine Lumumba aliomba msaada Umoja wa Mataifa, Marekani na Urusi.

Alipozuru Washington, Lumumba alikwenda kukutana na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani, Douglas Dillon, ambaye baadaye alidai kuwa Lumumba ni “mwendawazimu” na kwamba “ni mgumu kushughulika naye.”

Agosti 1, akizungumza mbele ya Umoja wa Mataifa, Lumumba alimshutumu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjold, kwa kuyakatalia majeshi ya Umoja wa Mataifa kuishambulia Katanga.

Agosti 7, Lumumba alikwenda kwa siri Ghana alikokutana na Rais Kwame Nkrumah kuzungumza suala la nchi hizo kuungana.

Agosti 8 Jimbo la Kasai Kusini nalo likatangaza kujitenga na Congo. Juma moja baadaye, Lumumba aliomba msaada wa kijeshi kutoka Urusi kudhibiti majimbo ya Katanga na Kasai yaliyojitenga.

Kesho yake, Agosti 16, Urusi wakatangaza kuwa huenda Congo wakahitaji kupatiwa jeshi la nje kuleta hali ya amani. Lumumba akasisitiza kuwa majeshi ya Umoja wa Mataifa yaondoke Congo.

Agosti 18 Urusi wakatuma kwenda Congo ndege 10 za kivita zenye rangi ya jeshi la Congo.

Baada ya kurejea Congo akitokea Marekani, Lumumba aliwaambia Rais Kasavubu na Mkuu wa Majeshi yake, Joseph Mobutu, kwamba ameamua sasa kuyaita majeshi ya Urusi.

Itaendelea kesho...

Kasavubu na Mobutu walimkatalia. Lakini Lumumba alikuwa ameshafanya uamuzi. Aliita majeshi ya Urusi ambayo yangemsaidia kuzuia kujitenga kwa jimbo la Kasai Kusini. Alifanikiwa, lakini mara baada ya mapigano kumalizika yalifuatiwa na mauaji ya watu zaidi ya 1,000 na wengine wapatao 250,000 kuyakimbia makazi yao.

Mara moja wakala wa CIA nchini Congo, Larry (Lawrence) Devlin, akatuma ripoti Washington ikidai kuwa Lumumba anajiandaa kufanya mapinduzi ya Kikomunisti.

Mradi wa kwanza wa CIA wa kumshughulikia Lumumba ulianza mapema Agosti 1960 na ulipewa jina la ‘Operation Wizard’. Sehemu moja ya utekelezaji wa mpango huo ni kuwahonga waandishi wa habari wa ndani na nje ya Congo ili waandike habari mbaya za Lumumba, kufadhili maandamano ya kumpinga, na kuhonga wanasiasa watofautiane naye. Mpango huo ulisimamiwa na mkuu wa CIA nchini Congo, Larry Devlin na watu wake.

Katika kitabu ‘Shadow Warfare: The History of Africa’s Undeclared Wars’ cha Larry Hancock, aliyekuwa akiandika muhtasari wa mkutano huo ni Robert Johnson. Dulles alikaririwa akisema, “Kwa Lumumba, tunakabiliana na mtu wa aina ya Castro au mbaya kuliko Castro.”

Siku chache baadaye, kwa mujibu wa kitabu ‘The Assassination of Lumumba’ cha Ludo de Witte, Agosti 26 “Allen Dulles, mkuu wa CIA, alituma telegramu kwenda ofisi za CIA za Leopoldville chini ya Larry Devlin: Telegramu hiyo ilisomeka “Kuondolewa kwa Lumumba madarakani lazima kuwe jambo la lazima na la haraka ... Lazima lipewe kipaumbele cha kwanza katika shughuli zetu.”

Baadaye siku hiyo hiyo Dulles alituma ujumbe mwingine kwenda Congo uliosomeka: “Sasa ni uhakika kwamba iwapo (Lumumba) ataendelea kushikilia wadhifa wake (Uwaziri Mkuu) Ukomunisti utatawala ... Kung’olewa kwake lazima kupewe kipaumbele.”

Itaendelea…!

Columnist: mwananchi.co.tz