Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba ateswa ndani ya ndege, marubani wajawa hofu-11

86374 Pic+lumumba MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba ateswa ndani ya ndege, marubani wajawa hofu-11

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya kumaliza vikao vya kujadiliana namna ya kumhamisha Patrice Lumumba kutoka Leopoldville na kumpeleka kwenye mahabusu za Jimbo la Katanga lililokuwa chini ya aliyekuwa hasimu mkubwa wa Lumumba, Moise Tshombe, hatimaye jioni ya Jumatatu ya Januari 16, 1960, muda mfupi baada ya majadiliano mengi, mkuu wa idara ya usalama ya Congo, Victor Nendaka, alipanda ndege kuelekea mjini Thysville (sasa Mbanza-Ngungu) alikokuwa anashikiliwa Lumumba. Usiku wa siku hiyo alilala katika hoteli mojawapo ya mji huo.

Saa 11:30 alfajiri ya kesho yake, Januari 17, Nendaka alikwenda kuwachukua Lumumba, Joseph Okito na Maurice Mpolo kutoka katika vyumba tofauti vya mahabusu walimokuwa wamehifadhiwa. Haijajulikana kwa nini aliamua kuwachukua mahabusu watatu tu wakati kulikuwa na mahabusu wengine.

Msafara mdogo wa kikosi cha jeshi la Congo, ANC (Armee Nationale Congolaise) ulianza safari kuelekea Kusini Magharibi, mbali na mjini wa Leopoldville, kuelekea uwanja mdogo wa ndege katika mji wa Lukala, kiasi cha kilomita 180 kutoka Leopoldville, ambako kulikuwa na ndege ndogo iliyokuwa ikiwasubiri.

Msafara huo uliwasili katika mji wa Lukala saa mbili asubuhi. Mahabusu hao Lumumba, Okito na Mpolo pamoja na Victor Nendaka Bika na wanajeshi watatu walianza safari ya kutoka uwanjani hapo wakiwa kwenye ndege iliyokuwa ikiwasubiri.

Walisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 360 kuelekea mji wa Muanda ulioko pwani ya Congo. Wakati Nendaka na wanajeshi wake wakiwasafirisha akina Lumumba kuelekea Muanda wakitokea Thysville, ndege ya Congo, DC-4, iliondoka Leopoldville kuelekea Muanda ikiwa na maofisa wawili wa serikali ya Congo, Ferdinand Kazadi Lupeleka na Jonas Mukamba Kadiata Nzemba.

Wakati huo Kazadi alikuwa Kamishna (cheo cha Waziri) wa Ulinzi nchini Congo baada ya kuteuliwa na Joseph Mobutu Septemba ya mwaka huo.

Wote hawa Kazadi na Mukamba ni wanasiasa kutoka Kasai, na walikuwa na uhusiano wa karibu na Albert Kalonji, ambaye nyakati fulani alikuwa mpinzani mkubwa wa kisiasa wa Lumumba.

Kwa mujibu wa kitabu ‘The Assassination of Lumumba’ (uk. 84) kilichoandikwa na Ludo de Witte, Kalonji aliapa kuwa atatumia fuvu la kichwa cha Lumumba “kama jagi la maji”. Kalonji alikuwa amemtangaza Lumumba kama mtu “mwenye kiu ya damu” na mtu ambaye “ni lazima ashitakiwe na kuuawa.” Wafuasi wa Kalonji walimwona Lumumba kama “mwovu” ambaye hakupaswa kuishi.

Kalonji alikuwa kiongozi wa jimbo la Kasai Kusini lililojitenga na Congo Agosti 12 mwaka huo. Kujitenga huko kulikuja siku chache tu baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru. Kujitenga huko kulitokana na kutofautiana kisiasa na Lumumba.

Wakati ndege iliyowabeba Lumumba na mahabusu wenzake ikielekea Muanda, ndege nyingine iliyowabeba maofisa wa serikali ya Congo nayo ilikuwa njiani kuelekea huko huko Muanda ikitokea Leopoldville. Katika uwanja wa ndege wa Muanda, maofisa hao waliisubiri ndege iliyowabeba Lumumba na wenzake.

Walipowasili mahabusu walihamishiwa kwenye ndege iliyotoka Congo. Wote waliotoka Thysville, isipokuwa Nendaka, waliingia kwenye ndege hiyo kuelekea Elizabethville (sasa Lubumbashi). Nendaka yeye alirudi Leopoldville (sasa Kinshasa).

Walinzi waliokuwa wakiwalinda mahabusu hao walikuwa wakiwafanyia vitendo vya kikatili. Waliwatesa tangu walipotoka Camp Hardy, Thysville hadi Muanda. Lakini hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi katika safari ya kutoka Muanda hadi Elizabethville, kiasi cha maili 1,100. Wakati wote huo walikuwa wakiteswa kwa kupigwa vibaya.

Mateso yaliendelea kiasi kwamba hata marubani wa ndege hiyo walianza kulalamika wakisema wanahofia hata usalama wa ndege yao ikiwa angani. Ili wasisikie mateso hayo yakiendelea. Kwa mujibu wa kitabu ‘Lumumba: Africa’s Lost Leader’ cha Leo Zeilig, wafanyakazi wa ndege hiyo waliamua kufunga mlango wa kuingia chumba cha marubani.

Ilipotimu saa 10:30 jioni ya Jumanne ya Januari 17, ndege hiyo ilikuwa imeshafika anga la Kusini Mashariki mwa Congo na sasa ilikuwa inakaribia kutua uwanja wa ndege wa Luano wa Elisabethville.

Wakati ndege inakaribia kutua, waongoza ndege katika uwanja huo walianza kuwasiliana na viongozi wa Congo wakitaka wapatiwe maelekezo ya nini cha kufanya kuhusu ndege hiyo. Sasa ndege ilikuwa anga la Katanga lililokuwa chini ya Moise Tshombe.

Wakati ndege ikizunguka juu ya uwanja huo, ofisa mmoja wa uwanjani hapo alimpigia simu Tshombe lakini hakumpata. Wakati huo Tshombe hakuwa uwanjani hapo kama ilivyopangwa awali. Ndege hiyo iliwahi kufika kabla ya muda uliopangwa.

Kwa mujibu wa kitabu ‘The Assassination of Lumumba’, wakati ndege inatua Tshombe alikuwa kwenye jumba lake akitazama sinema iliyoitwa ‘Liberte’.

Ndege hiyo ilitua saa 11 jioni. Aliyekuwa uwanjani hapo wakati ndege ikitua ni Godefroid Munongo ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Katanga.

Munongo alikuwa na kikosi kikubwa cha wanajeshi kikiwa kimeweka ulinzi mkali uwanjani hapo.

Polisi wapatao 50 walikuwa uwanjani. Wengine waliokuwamo ni vikosi viwili vya wanajeshi wa Katanga. Inakumbukwa kuwa Julai 1960, baada ya Katanga kujitenga na Congo, Munongo alimpiga marufuku Lumumba kukanyaga ardhi ya Katanga, lakini leo, Januari 17, 1961, karibu miezi sita baadaye, aliiruhusu ndege iliyombeba Lumumba kutua eneo la kijeshi la Katanga.

Wengine waliokuwa uwanjani hapo ni baadhi tu ya maofisa wa serikali ya Katanga. Hatimaye Lumumba, Mpolo na Okito walishushwa kutoka kwenye ndege hiyo. Walikuwa na majeraha na maumivu makubwa kutokana na mateso waliyopata wakiwa ndani ya ndege.

Wanajeshi waliowateremsha waliwapakia kwenye gari la jeshi. Wakati umati wa watu uwanjani hapo wakiangalia kilichokuwa kinaendelea, wanajeshi hao waliondoka na mahabusu wao uwanjani hapo.

Aliyekuwa akisimamia operesheni ya kuwashughulikia Lumumba na wenzake katika zile saa chache za mwisho za maisha yao tangu walipofikishwa Elizabethville ni Kamishna wa Polisi, Frans Verscheure.

Januari 22, 1960, wakati serikali ya kikoloni ilipomhukumu Lumumba kifungo huko Stanleyville kwa tuhuma za kusababisha vurugu, Kamishna Verscheure ndiye aliyempeleka Lumumba gereza la Jadotville la Katanga. Sasa ni mwaka mmoja baadaye, Lumumba na Verscheure wanakutana kwa mara nyingine.

Jioni ya siku hiyo, Januari 17, hata kabla ile ndege haijatua, Munongo alimwambia Verscheure kuwa Lumumba yuko njiani akiletwa Katanga na hivyo aandae kabisa sehemu ya kumhifadhi na bila kusita, wazo lililomjia Verscheure ni jina la mkulima aliyeitwa Lucien Brouwez aliyekuwa na nyumba ambayo haikuwa na mtu aliyekuwa akiishi ndani yake.

Nyumba hiyo ilikuwa umbali wa kiasi cha maili mbili kutoka uwanja wa ndege wa Luano, na Verscheure alichukua sehemu ya nyumba hiyo kama mahabusu ya muda.

Maofisa usalama walikata uzio wa chuma wa uwanja huo kuelekea kwenye nyumba hiyo ili mahabusu hao wapitishwe eneo hilo badala ya kupitishwa kwenye lango kubwa.

Serikali ya Katanga ilichonuia kumwondoa Lumumba uwanjani hapo kwa siri na kwa haraka iwezekanavyo.

Muda mfupi baadaye Verscheure alipigiwa simu na kuelekezwa kwenda nyumbani kwa Rais wa Katanga, Moise Tshombe. Umbali wa kutoka kwenye kituo cha polisi, ambako ndiko ilikuwa ofisi ya Verscheure, kwenda nyumbani kwa Tshombe ni wa kutembea kwa mguu. Simu aliyopigiwa ilimsisitiza awepo kwa Tshombe usiku huo.

Kikosi cha Kapteni Julien Gat, aliyekuwa ofisa wa kijeshi wa Ubelgiji aliyekuwa Congo, kiliwafikisha mahabusu hao katika nyumba ya Brouwez, kisha wakaweka ulinzi mkali wasiweze kutoroka na kuzuia majeshi ya UN kuwaokoa.

Simulizi fulani inasema Munongo na maofisa wengine wawili au zaidi nao walichukua nafasi kuwatesa Lumumba na wenzake wawili.

Columnist: mwananchi.co.tz