Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961:Lumumba aponyoka, CIA washindwa kumuua kwa sumu-6

85549 Lumumbapic MAUAJI YA LUMUMBA 1961:Lumumba aponyoka, CIA washindwa kumuua kwa sumu-6

Sat, 23 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) lilituma ‘ujumbe wa sumu’ kwenda Congo kwa ajili ya kumuua Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, Patrice Emery Lumumba. Ujumbe huo kwenda kwa aliyekuwa mkuu wa CIA, Congo, Lawrence (Larry) Raymond Devlin, ulipelekwa na wakala wa CIA aliyeitwa Sidney Gottlieb

Kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa na Madeleine G. Kalb katika kitabu ‘The Congo Cables: The Cold War in Africa-From Eisenhower to Kennedy’, ulimwambia Devlin hivi: “Atajitangaza kama Joe kutoka Paris... ni muhimu uonane naye haraka mara atakapokupigia simu. Atajitambulisha kwako kikamilifu na kukueleza kazi aliyokuja kuifanya.”

Ndipo jioni ya Jumatatu ya Septemba 26, Gottlieb aliwasili Congo. Devlin, aliyekuwa anafanya kazi ya ujasusi kwa mwamvuli wa ofisa wa ubalozi wa Marekani Congo, aliondoka ofisini kwake kwenda kukutana na mgeni wake.

Walipokuwa kwenye gari la Devlin, Gottlieb alimweleza kuwa “nimekuja Congo kukupa maelekezo kuhusu operesheni moja muhimu.”

Kitabu ‘Poisoner in Chief: Sidney Gottlieb and the CIA Search for Mind Control’ cha Stephen Kinzer kinasema Gottlieb aliwahi kuifanyia majaribio sumu yake kwa wafungwa, watumiaji dawa za kulevya, wagonjwa mahospitalini, washukiwa wa upelelezi, raia wa kawaida na hata wafanyakazi wenzake, na kote huko, alisema, alifanikiwa.

Gottlieb alikuja kujulikana kuwa ni ofisa pekee wa CIA aliyebeba sumu kutoka Amerika kwenda kumuua kiongozi wa nchi nyingine katika bara la Afrika.

Akiwa nyumbani kwa Devlin katika ubalozi wa Marekani mjini Leopoldville, ndipo Gottlieb alipomfahamisha Devlin kuwa alikuwa amebeba vifaa vyenye sumu ya kumuua Waziri Mkuu Lumumba.

“Mungu wangu,” alishangaa Devlin. “Nani aliyeidhinisha hii operesheni?” Alihoji.

“Ni Rais (Dwight) Eisenhower,” alijibu Gottlieb. “Nilikuwapo wakati akiidhinisha, lakini Dick Bisell alisema Eisenhower anataka Lumumba aondolewe madarakani.” Wakati huo Dwight David “Ike” Eisenhower ndiye alikuwa Rais wa Marekani na Bisell alikuwa ofisa wa CIA aliyeshughulikia miradi mikubwa.

Gottlieb na Devlin wote walijikuta wameacha kuongea kwa dakika kadhaa. Devlin akawasha kwanza sigara kabla hajaendelea kuongea. Baadaye kidogo Gottlieb akavunja ukimya uliotawala.

“Ni jukumu lako kufanya operesheni hii, ni yako peke yako,” Gottlieb alimwambia Devlin. “Maelezo ni yako, lakini lazima (operesheni) iwe safi, ifanyike kwa namna ambayo hakuna kitu kinachoweza kuacha nyuma alama yoyote ya kuihusisha serikali ya Marekani.” Kisha akamkabidhi kasha la sumu alilotoka nalo Marekani.

“Chukua hii,” alimwambia. “Kwa kilichomo humu ndani kikitumika hakuna mtu atakayejua kamwe kuwa Lumumba aliuawa.”

Baada ya hapo Gottlieb akaanza kumpa Devlin maelezo na maelekezo ya namna ya kufanya. Ingeweza kuwekwa kwenye kitu chochote ambacho kingeugusa mdomo wa Lumumba—iwe ni mswaki au chakula, na hapo kazi ingekuwa imemalizika.

Sumu hiyo haikutengenezwa kwa namna ya kuua haraka, lakini kifo kingekuja baada ya saa kadhaa. Alimwambia pia kwamba hata kama kungefanyika uchunguzi wa sababu za kifo, kile ambacho kingeonekana ni zile sababu za kawaida tu.

Hata hivyo ilishindikana, hawakuweza kumwekea sumu kwa kile ambacho John Jacob Nutter alikisema katika kitabu chake, ‘The CIA’s Black Ops: Covert Action, Foreign Policy, and Democracy’, kwamba “Hata kuweka sumu kwenye chakula chake ilikuwa shida sana kwa sababu CIA haikuwa na mawakala ambao wangeweza kuingia jikoni kwa Lumumba.” Kwa hiyo CIA haikufanikiwa kumuua Lumumba kwa sumu.

Kwa zaidi ya miongo miwili akiwa CIA, Gottlieb alikuwa ameelekeza nguvu na akili zake zote katika utafiti wa namna ya kuanzisha mfumo wa kudhibiti akili za mwanadamu lakini alijulikana zaidi kama “mtengenezaji mkuu wa sumu katika CIA.”

Tafiti zake zilikuwa zikifanyika kwa siri kubwa kiasi kwamba alipokuja kuacha kazi mwaka 1972 aliteketeza asilimia 80 ya nyaraka zilizokuwa na ripoti mbaya. Alilazimika kuyateketeza kabla ya kuondoka kazini. Asilimia kubwa ya nyaraka hizo inahususu kazi za Gottlieb.

Anne Collins, katika ukurasa wa 30 wa kitabu chake, ‘In the Sleep Room: The Story of the CIA Brainwashing Experiments in Canada’, anaandika kuwa nyaraka hizo zilikuwa na taarifa mbaya kiasi kwamba maelfu ya kurasa za nyaraka “ziliharibiwa kwa amri ya watu wawili: Mkurugenzi wa CIA Richard Helms, aliyestaafu mwaka 1973 na Dk Sidney Gottlieb, ambaye alihusika zaidi na nyaraka hizo.”

Ilidaiwa kuwa nyaraka hizo zingewekwa wazi zingezua kashfa kubwa zaidi duniani na huenda ingeufungulia ulimwengu sababu za kuifungulia mashtaka CIA kwa ukatili dhidi ya wanadamu.

Kitabu ‘Top Secret Government Archives: Missing Files and Conspiracy Paper Trails’ cha mwandishi wa habari za utafiti, Nick Redfern, kinaandika: “Kama tulivyoona, wakati hofu ilipotanda ndani ya CIA kwamba itajulikana kwa watu wa nje [ya CIA] mradi wa CIA [dhidi ya utu], mkurugenzi wa shirika hilo, Richard Helms na Sidney Gottlieb waliandaa mpango wa kuziteketeza moja kwa moja nyaraka hizo.

Nyaraka hizo zilijulikana pia kama ‘Mpango wa CIA wa kudhibiti akili za wanadamu’.

Sehemu ya mradi huo ulikuwa ni kufanya majaribio juu ya ubongo wa mwanadamu kwa kuendeleza dawa ambazo zingeweza kutumiwa kudhoofisha uwezo wa mtu wa kudhibiti akili yake ili atamke yale asiyokusudia kuyatamka.

Mradi huo na mingine mingi iliandaliwa chini ya Ofisi ya Ushauri wa Kisayansi ya CIA kwa kuratibiwa na Maabara ya Vita ya Kibaiolojia ya Jeshi la Marekani.

Nick Redfern anaendelea: “Kumbuka kuteketezwa nyaraka hizo kulivyofanikiwa; ni kwa kuzimwaga kwenye tanuri, mwaka 1973, katika kituo cha kumbukumbu cha CIA, kilichokuwa Warrenton, Virginia. Kwanini hili jambo lilikuwa la muhimu? Kwa sababu kugundulika siri zilizokuwa kwenye nyaraka hizo kungeonyesha ukatili dhidi ya mwanadamu uliofanywa na shirika...”

Hata hivyo, wakati watu wengi waliokuja kujulishwa kuwa ndugu zao walilishwa sumu iliyotengenezwa na Sidney Gottlieb, walianza kufungua mashtaka mmoja baada ya mwingine alianza kuitwa katika mahakama mbalimbali za nchini Marekani.

Wakati baadhi ya kesi hizo ziliendelea na nyingine zikiwa kwenye upelelezi, Gottlieb alifariki dunia Jumatano ya Machi 10, 1999 Jijini Washington.

Itaendelea…

Columnist: mwananchi.co.tz