Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba aondolewa madarakani, atoroka-7

85765 Pic+lumumba MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba aondolewa madarakani, atoroka-7

Mon, 25 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Agosti 21, 1960 Waziri Mkuu wa Congo, Patrice Lumumba aliomba waziwazi msaada wa kijeshi Urusi. Siku tano baadaye, Agosti 26, baada ya kukataliwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa (UN) kuishughulikia Kasai Kusini iliyojitenga, Lumumba alituma majeshi ya Congo yanayomtii kwenda Kasai Kusini.

Wanajeshi hao walikuwa katika ndege 15 za kijeshi za Urusi na malori 100. Nia ya Lumumba ni kulirejesha jimbo lililojitenga. Kufikia hatua hiyo, Allen Dulles alimtumia Devlin ujumbe akimwelekeza amuue Lumumba.

Mwishoni mwa Agosti maofisa wa Urusi waliwasili Congo. Kwa kuona Lumumba alikuwa akiegemea sana ushauri na misaada kutoka Urusi, Rais Joseph Kasavubu alianza kuingiwa na wasiwasi.

Septemba 5, Rais Kasavubu akamfukuza kazi Lumumba kama Waziri Mkuu wa Congo. Wakati huo huo Lumumba naye akamfukuza kazi Rais wake, Kasavubu. Kwa hiyo walifukuzana kazi, Kasavubu alimteua Joseph Ileo kuwa waziri mkuu badala ya Lumumba.

Septemba 9, hata baada ya kudaiwa kufukuzwa kazi, Lumumba aliidhinisha malipo ya dola milioni moja kwa wanajeshi wa Leopoldville (sasa Kinshasa). Mgogoro wa uongozi ukaongezeka kati ya Lumumba na Kasavubu.

Baada ya vuta nikuvute kati ya Lumumba na Kasavubu, mgogoro ukafikia kilele chake Septemba 5, 1960. Mgogoro ulisababishwa na kutoelewana kati ya Lumumba na Kasavubu kuhusu namna ya kushughulikia Jimbo la Katanga lililojitenga na Congo.

Siku hiyo serikali ya Congo ikapasuka vipande viwili. Kasavubu akamfukuza Lumumba kazi ya uwaziri mkuu na kuliomba jeshi la UN lichukue madaraka ya utawala Congo. Baraza la Mawaziri la Lumumba nalo likamfukuza Kasavubu kama Rais wa nchi, likimtuhumu kwa uhaini.

Septemba 14, 1960, kikao cha pamoja cha Baraza la Congo kikapiga kura na kumkabidhi Lumumba madaraka ya kuongoza nchi hadi hapo mgogoro wa uongozi utakapomalizika na tume ya kibunge ndiyo ambayo ingemwongoza.

Hadi hapo kulikuwa na kambi mbili za serikali, moja ya Joseph Ileo (baadaye alibadili jina na kujiita Sombo Amba Ileo) ambaye aliteuliwa na Kasavubu kama Waziri Mkuu badala ya Lumumba. Kambi nyingine ni ya Lumumba ikiwa na baraka za tume ya Bunge.

Katika kuhakikisha viwanja vya ndege na redio havitumiwi vibaya, majeshi ya UN yalivitwaa lakini hata baada ya Baraza la Congo kupiga kura kumpa Lumumba mamlaka ya kuendelea kutawala, siku hiyo hiyo, Jumatano ya Septemba 14, Mobutu alitangaza anatwaa madaraka ya nchi hadi Desemba 31 ili kuwapa muda Lumumba na Kasavubu waafikiane. Kisha akateua serikali ya mpito.

“Kuanzia sasa,” alisema Mobutu, “Kasavubu na Lumumba hawako madarakani... ni mpaka mwishoni mwa Desemba watakapokubaliana namna ya kuongoza pamoja.

Baada ya Mobutu kuwatoa madarakani Kasavubu na Lumumba, Kasavubu alikimbilia Brazaville kujificha wakati Lumumba akibaki Leopoldville kwenye nyumba ya makazi ya waziri mkuu akilindwa na majeshi ya Mobutu asitoroke.

Mkono mrefu wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) ulionekana. Mwandishi James Hunter Meriwether katika ukurasa wa 218 wa kitabu chake, ‘Proudly We Can be Africans: Black Americans and Africa, 1935-1961’ anaandika: “Katika kipindi chote cha misukosuko, maofisa wa Serikali ya Marekani walikuwa katika jitihada kubwa ya kumhamisha Mobutu, msaidizi binafsi wa Lumumba kabla bosi wake hajamteua kumfanya mnadhimu wa jeshi, kumhamishia kwenda kambi ya Kasavubu. Saa chache baada ya Kasavubu kutangaza kuliahirisha Bunge, Mobutu alitwaa madaraka kwa jina la jeshi.

“Aliahidi ‘kubatilisha’ nyadhifa za Kasavubu, Lumumba, Ileo na wanasiasa wengine hadi mwisho wa mwaka (1960). Aliwaita wanafunzi wa Chuo Kikuu Congo na wahitimu wengine wa vyuo kuendesha serikali. Aliwafukuza mabalozi wa Urusi na Czechoslovakia. Siku chache baadaye wakati CIA ilipomtahadharisha Mobutu juu ya njama za kumuua, Mobutu alibadilika, akaanza kuegemea upande wa Kasavubu aliyefuata matakwa ya nchi za Magharibi.

“Aliwaambia maofisa ubalozi wa Marekani kuwa angemkamata Lumumba na kuweka madaraka mikononi mwa serikali ya Ileo-Kasavubu mwishoni mwa Oktoba. Hata hivyo Mobutu hangeweza kumkamata Lumumba kwa sababu Lumumba alikuwa nyumbani kwake akilindwa na UN. Kwa hiyo, majeshi ya Mobutu walimzuia Lumumba asiondoke kwenye nyumba hiyo.”

Septemba 19 ‘Tume ya Wanavyuo’, ikiwa na wahitimu zaidi ya 30, ikaundwa ili kuendesha serikali ya mpito. Kuanzia hapo kamatakamata ilianza. Kasavubu aliondoka kwenda New York, Marekani kuhudhuria mkutano wa Baraza la Usalama la UN. Huko alitoa hotuba yake Novemba 8 na alitambuliwa kama Rais wa Congo licha ya kwamba Mobutu alijitangaza yuko madarakani na serikali ya mpito.

Novemba 27, 1960, siku ambayo Kasavubu alirejea kutoka New York, alikopeleka malalamiko yake UN na kisha akapokewa kwa shangwe na wanasiasa kadhaa wa Congo, ndiyo siku ambayo Lumumba aliondoka Leopoldville kwenda Stanleyville (Kisangani) kuanzisha upya mapambano ya kisiasa.

Hadi Novemba 27 alikuwa chini ya ulinzi wa UN nyumbani kwake Leopoldville lakini aliruhusiwa kutoka na kurudi nyumbani.

Akiwa nyumbani kwake, Lumumba aliona shamrashamra za mapokezi ya Kasavubu zikiendelea. Waliokuwa wamezingira eneo zilipokuwa zikifanyika shangwe hizo ni askari wa Mobutu.

Lumumba aliona atumie fursa hiyo kutoroka na kwenda Stanleyville ambako Antoine Gizenga, aliyekuwa naibu wake, alikuwa akiwaandaa wapambanaji ili kujipanga upya. Alitoroka kwake bila askari wa Mobutu kugundua.

Baada ya kuona kuwa hangeweza tena kurudi madarakani kwa njia za kawaida, hasa baada ya kurejea kwa Kasavubu kutoka UN, Lumumba aliona njia pekee ya kutwaa madaraka ni kuitwaa Leopoldville akitokea Stanleyville.

Wanasiasa wengine saba waliokuwa tayari kujiunga na Lumumba na waliokuwa kwenye baraza lake la mawaziri ni Christophe Gbenye, Joseph Mbuyi, Maurice Mpolo, Anicet Kashamura, Pierre Mulele na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Barthelemy Mujanay. Msafara wao ulikuwa wa magari matatu, mojawapo liliibeba familia yake.

Baada ya Kasavubu na Mobutu na Wamarekani na Wabelgiji kugundua Lumumba ametoroka na familia yake, walianza kumsaka.

Viongozi wa Leopoldville walinuia kumkamata kwa gharama zozote. Shirika la huduma za kijasusi la kikoloni nchini Congo la Surete, chini ya Victor Nendaka Bika, liliingia kazini kumsaka Lumumba. Mkuu wa CIA Congo, Larry Devlin, na mshauri wa Kasavubu wa masuala ya usalama, Andre Lahaye, walishirikiana kikamilifu na taasisi ya Nendaka.

Ubelgiji walitoa ndege ndogo za kuruka karibu na usawa wa ardhi. Mbelgiji mshauri wa Mobutu, kanali Louis Marliere, alisambaza askari wa kuweka vizuizi barabarani na kwenye mito iliyofikiriwa Lumumba angeweza kupitia.

Mvua iliyokuwa inanyesha na vizuizi vya barabarani vilipunguza kasi ya Lumumba kutoroka. Kilichomchelewesha zaidi ni kusimama karibu kila kijiji alipowaona watu na kuanza kuwahutubia.

Huku akiendelea kusalimiana na watu kila alikopita, inaelekea Novemba 30 waliokuwa wanamtafuta wakiwa angani waliuona msafara wake. Kesho asubuhi, Alhamisi, alipita njia-panda ya mji wa Port Francqui karibu na mpaka wa Leopoldville na Kasai.

Itaendelea kesho…!

Columnist: mwananchi.co.tz