Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MASTORY YA OSCAR OSCAR: Umejiandaa kuwa Diamond Platinumz?

Umejiandaapic Data Diamond Platnumz

Tue, 22 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Siku moja isiyo na jina, Diamond Platnumz alikuwa na shoo mkoani Iringa. Baada ya hapo alikuwa na shoo Nairobi, Kenya. Kisha alikuwa anatakiwa kurudi Dar es Salaam kwenye shoo.

Arusha na Mwanza zilikuwa zinamsubiri pia. Ni shoo tano ndani ya siku tano kwenye miji tofauti. Hii ni ratiba ya kazi ya msanii tajiri kuliko wote nchini. Hii ni ratiba ya kazi ya msanii mwenye ushawishi mkubwa kuliko wasanii wote Afrika Mashariki kwenye mitandao ya kijamii.

Hii ndiyo ratiba ya kazi ya msanii kipenzi cha watu kwenye kizazi hiki. Ukitazama ratiba ya kazi ya Diamond Platinumz na yako ni vitu viwili tofauti. Huna umaarufu wowote. Huna utajiri wowote bado unafanya kazi kwa maringo. Bado unalala hadi saa nne asubuhi. Kuna mengi sana ya kujifunza kutoka kwa Diamond Platinumz. Ni kijana wa Kitanzania ambaye makuzi yake na historia vinafanana na vijana wengi wa Kitanzania, lakini ameamua kuweka utofauti kwa kufanya kazi na bidii.

Vijana wengi bado hatuamini kwenye kufanya kazi. Vijana wengi bado hatuamini kwenye kujituma. Watu wengi bado tunaishi maisha ya kufikirika zaidi. Ukijipa muda kidogo wa kuchunguza maisha ya watu waliofanikiwa utagundua kuwa wanafanya kazi saa nyingi kuliko wewe.

Ukijipa muda wa kuchunguza watu waliokuzidi maisha utagundua wewe unalala saa nyingi kwa siku kuliko wao. Vijana wengi baada ya kupata gari dogo na kupanga vyumba viwili pale Magomeni Mapipa huona tayari maisha wameyapatia.

Vijana wengi baada ya kusafiri Arusha, Mwanza na Mbeya kwao maisha huwa yanaishia hapo. Safari ya mafanikio inahitajika hesabu ndefu. Msanii kama Diamond Platinumz watu wanapaswa kumtazama kama ‘rolimodo’ wao. Ni kijana anayeweza kubaki namba moja kwa anachofanya kila siku.

Ni aina ya msanii ambaye maisha yake yanapaswa kuwa shule tosha kwa vijana wengi wa Kitanzania. Kama kila mtu kwenye eneo lake akiamua kuwa Diamond Platinumz, Sky is the limit! Tuache kutengeneza chuki kwa watu waliotuzidi maisha. Hawa ni aina ya watu tunaopaswa kuwasogeza kwenye maisha yetu. Ukitaka kufika mbali jifunze bila kuchoka kwa watu waliofanikiwa. Pale Tandale anapotoka Diamond vijana wengi wa Kitanzania ndiyo makuzi yetu yalivyo. Hakuna tofauti yoyote.

Kinachomtofautisha Diamond Platinumz na tulio wengi ni bidii tu ya kazi. Kinachomtofautisha Platinumz na tulio wengi ni kuchukia watu waliofanikiwa badala ya kujifunza kutoka kwao. Maisha sio chuki. Maisha ni kujifunza.

Kila mtu ana nafasi ya kuwa Platinumz kwenye eneo lake la kazi. Kila mtu anaweza kuwa Platinumz kwenye taaluma yake. Tatizo kubwa ni kuridhika mapema. Tunapoteza muda mwingi kutukana mtu aliyekuzidi kimaisha. Tunapoteza muda mwingi kulinganisha watu. Tunapoteza muda mwingi kusambaza uzushi. Diamond Platinumz hajafanikiwa kwa bahati mbaya.

Anapiga kazi saa nyingi kuliko wewe. Anatafuta pesa kwa bidii kuliko mimi. Kwa zilezile anazopitia Platinumz ukizifanya kwenye biashara yako unatoboa. Kwa mbinu zilezile anazotumia Diamond ukizitumia kwenye kipaji chako chochote unatoboa.

Pamoja na pesa alizonazo pamoja na umaarufu alionao. Diamond Platinumz anatajwa kuwa kijana mwenye nidhamu ya kazi kuliko mtu mwingine yeyote. Vijana wengi baada ya kupata gari ndogo na kupanga chumba pale Kinondoni, watu wengi huridhika. Vijana wengi baada ya kupata umaarufu mkubwa, nidhamu ya kazi hupungua! Hapa ndipo lilipo daraja la Diamond na wewe.

Hapa ndipo Platinumz anatofautiana na watu wengine. Kuridhika mapema ni ugonjwa mkubwa, lakini kumchukia mtu aliyefanikiwa ni ugonjwa hatari zaidi.

Ukitaka kusogea mbele kimaisha ni lazima ujifunze kwa waliofanikiwa. Ukitaka kupiga hatua mbele lazima uwe na ‘rolimodo’ wako. Diamond Platinumz ana sifa zote za kuwa ‘rolimodo’ wa vijana wengi tu wa nchi hii.

Kuna mengi sana ya kujifunza kutoka kwake kikazi. Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwake kwenye namna ya kutumia mitandao ya kijamii. Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwake kwenye kuheshimu watu.

Amezaliwa kwenye mazingira ya chini ambayo wengi wa vijana wa Tanzania wamezaliwa. Amekuwa kwenye jamii ambayo athari zake wote mnazijua. Huyu ni balozi mzuri sana kwenye safari ya mafanikio. Sio lazima na wewe uimbe muziki.

Columnist: www.mwananchi.co.tz