Wakati mijadala na maandamano yakiendelea, wengi walihoji kuhusu kijana aliyeitwa John Okello. Lakini kwa kifupi, Okello, ambaye ametajwa katika kitabu cha “Mwalimu: The Influence of Nyerere” kama ‘masiha mjinga’, alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Lango kaskazini mwa Uganda.
Alisoma Shule ya Msingi ya Misheni ya Aloi, umbali wa kilometa 72 kaskazini mashariki mwa mji wa Lira. Kwa kuwa wazazi wake walifariki dunia alipokuwa angali mtoto, hakupata watu waliomsukuma kuendelea na shule. Kwa hiyo hakuweza kumaliza masomo ya awali.
Badala yake alianza kufanya kazi za aina tofauti. Kwanza alianza kufanya kazi nchini Uganda, na alipoona hali ya maisha imekuwa ngumu tofauti na alivyotarajia, alivuka mpaka na kuingia Kenya.
Kazi yake ya kwanza ilikuwa mtumishi wa nyumbani kwa mtu mmoja mwenye asili ya India, tajiri aliyeishi Soroti, umbali wa kilometa 112 kaskazini magharibi mwa mji wa Mbale. Baadaye alifanya kazi katika shamba la pamba ambako wakati mmoja aliitisha mgomo wa wakulima, akidai hali bora za wafanyakazi zizingatiwe na kuthaminiwa na ujira kwa vibarua uongezwe.
Hali hiyo ya kuwa na ushawishi kwa wafanyakazi wenzake ulisababisha tajiri wake amfukuze.
Aliondolewa kwa nguvu kutoka shamba hilo. Alikuwa kihisi kuwa machungu ya maisha yake yalitokana na kunyanyaswa na Waarabu na Wahindi na hivyo kuwa na chuki nao.
Baada ya vuguvugu kuzidi, Januari 11, 1964 saa 1:00 asubuhi, Okello, ambaye pia aliwahi kuitwa “Gideon” na jarida la Spectator, alianza kutoa moja ya matangazo yanayojulikana Zanzibar kuwa ni mabaya zaidi.
Alitamka kwa mara ya kwanza kuwa yeye ni “Field Marshal wa Wapigania Uhuru”. Awali hakutaja jina lake, lakini saa chache baadaye alitamka jina lake likitanguliwa na cheo alichojipachika; Field Marshal John Okello, gazeti la Tanganyika Standard la Januari 13, 1964 liliandika.
Mchana wa siku hiyo, Okello alitangaza redioni akisema: “Amkeni ninyi mnaojiita wafalme. Hakuna tena serikali ya kifalme katika kisiwa hiki. Sasa hii ni serikali ya wapigania uhuru. Amkeni nyie watu weusi, na kila mmoja wenu abebe bunduki na zana za vita na kuanza kupigana.”
Baada ya kuridhika na mipango yake, mchana wa Januari 12, 1964, Okello alitangaza jamhuri; Jamhuri ya Zanzibar huku mwenyewe akajitangaza kuwa na cheo cha “Waziri wa Ulinzi na Utangazaji na Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi”.
Pia alimtangaza Sheikh Abeid Karume kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Kassim Hanga akatangazwa kuwa Makamu wa Rais, na Abdulrahman Babu pamoja na viongozi wengine wa ASP wakawa mawaziri katika serikali mpya.
Aboud Jumbe alipewa nafasi ya Waziri wa Afya na Huduma za Jamii, Othman Sharif (Elimu), Hasnu Makame (Kilimo), Idris Abdul Wakil (Biashara) na Abdulrahman Babu (Mambo ya Nje).
Katika matangazo mengine ya redio, Okello alimteua tena Hasnu Makame kuwa Waziri wa Fedha na Saleh Sadalla (Kilimo).
Siku iliyofuatia, Januari 13, Okello, akiwa aliwateua mawaziri wake, kwa mujibu wa gazeti la Tanganyika Standard la Januari 14, 1964 alikuwa na kukurukakara nyingi.
Alionekana akipita hapa na pale kama mtu aliyekuwa akitafuta jambo fulani asilipate. Mipango yake ilikuwa haijamalizika, badala yake ilizidi kuwa mingi. Aliwateua maofisa wengine zaidi wa serikali yake, wengi wao wakiwa ni watu ambao ndio kwanza walihamia kutoka bara.
Huku watu wengi visiwani Zanzibar na duniani wakiwa hawajawa na uhakika wa kitakachoendelea, sauti ya Okello ilisikika redioni ikisema: “Serikali sasa inaendeshwa na sisi, Jeshi. Ni juu ya kila raia, mweusi, maji ya kunde au mweupe, kutii amri. Ukiwa mkaidi au kudharau amri, nitachukua hatua kali mara 88 zaidi ya hatua nilizochukua sasa (kuangusha serikali ya Sultan).”
Vitisho na uwezo wake wa kutekeleza anayoahidi viliwashtua wananchi. Siku iliyofuata ya Januari 14, 1964, alitoa tangazo jingine lililokuwa na maneno makali zaidi.
“Huyu ni Field Marshall (Jemadari Mkuu) wa Zanzibar na Pemba. Ninafikiria kwenda (kijiji cha) Mtendeni kukiangamiza ikiwa watu wa huko hawataki kutii amri. Baada ya dakika 40 nitakuja kuwamaliza nyie wote, hasa Wacomoro.”
Mara mbili, Okello alifanya safari za kwenda Dar es Salaam na Pemba na hivyo kutoonekana Unguja. kutoonekana kwake kuliathiri cheo chake huko Unguja, hasa kutokana na hofu iliyoongezeka Zanzibar iliyotokana na maasi ya kijeshi ya Dar es Salaam.
Maasi ya kijeshi ya Dar es Salaam yalisababisha manowari ya Jeshi la Maji la Uingereza inayoitwa Rhyl, pamoja na wanajeshi wake kuamriwa kwenda Dar es Salaam hivyo polisi wa Tanganyika walitoa ulinzi kidogo tu kwa Karume. Okello aliporejea kutoka Pemba alikutana na mabadiliko mengi.
Baadaye Okello aliitwa na Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam. Alhamisi ya Februari 20, alisindikizwa na Karume mwenyewe hadi uwanja wa ndege. Kabla hajaondoka uwanjani hapo, Hasnu Makame, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Maendeleo ya Zanzibar, alimpa Karume paundi 357.17 za Kiingereza kwa ajili ya kulipia safari za Okello.
Akiwa mjini Dar es Salaam akisubiri ahadi kutoka kwa wanasiasa wa bara itekelezwe, aliletewa gazeti kutoka Zanzibar lililokuwa na habari iliyomhusu. Habari hii ilimshtua kuliko habari nyingine yoyote aliyowahi kupokea katika maisha yake; “Okello marufuku kuonekana Zanzibar”.
Okello alipigwa butwaa. Alipigwa marufuku na serikali ya Karume asifike Zanzibar.
Hakumjua aliyemletea gazeti. Lakini inawezekana alikuwa mmoja wa watu wa usalama wa Taifa wa Tanganyika. Kabla hata hajamaliza kusoma habari yote iliyomhusu, Okello alifumba macho kwa muda. Pengine ni kwa sababu machozi yalikuwa tayari yanaanza kumlengalenga machoni au labda alikuwa akitafakari hali ya mambo ilivyokuwa, au labda alikuwa katika sala ya kumuomba Mungu wake kuwa jambo hilo lisiwe la kweli.
Nyerere, kupitia kwa Oscar Kambona, alimwambia Okello aendelee kubaki Dar es Salaam na “atazamie kutembelewa na Karume hivi karibuni”.
Hii ilikuwa ni mbinu nyingine ya kuipa Serikali ya Mapinduzi muda zaidi wa kujiandaa dhidi ya Okello ikiwa angeamua kurejea Unguja?
Soma zaidi: Kilichomponza Okello baada ya kuongoza Mapinduzi