Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

MAONI YA MHARIRI: Mwongozo unahitajika kwa wasomi kushiriki Mapinduzi ya Viwanda

11895 MHARIRI+PIC TanzaniaWeb

Sun, 22 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Vijana wa kike wa wa kiume wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu wamejitokeza kwa wingi kwenye Maonesho ya 13 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018 yenye kaulimbiu isemayo “Elimu ya Juu Bora kwa Mapinduzi ya Viwanda”.

Katika maonyesho hayo yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, yanamalizika leo, huku vyuo 68 vikiwa vimeshiriki na mambo mbalimbali kuonyeshwa ukiwamo umahiri wa vyuo, mambo ya utafiti, maisha ya wanafunzi vyuoni na elimu kwa jumla.

Katika mabanda ya maonyesho ya vyuo hivyo washiriki wengi walijipanga vyema kuhakikisha wanafanya usajili wa vijana waliojiandaa kujisajili kwa ajili ya kuanza masomo yao ya elimu ya juu, Oktoba mwaka huu.

Maofisa kadhaa kutoka kwenye vyuo hivyo walionekana kuwa makini katika kunadi umahiri wa kozi zinazotolewa kwenye vyuo vyao, huku vyuo vingine katika kuonyesha umakini vikituma wahadhiri wao ili waweze kuwaelimisha vijana hao.

Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam na Chuo cha Ustawi wa Jamii ni miongoni mwa vyuo vinavyoshiriki maonyesho hayo ambavyo vimetuma wahadhiri wao.

Tume ya Vyuo Vikuu (TCU)ambao ni waandaaji wa maonyesho hayo walionyesha umakini katika usimamizi kwani muda mwingi viongozi husika walitembelea akiwamo mkurugenzi wa udahili na nyaraka.

Umakini ulioonyesha kwenye maonyesho haya ndiyo unaopaswa kuendelea kuonyeshwa kwa kuwafuatilia kwa karibu wanafunzi hao wapya wanapoingia vyuoni kuanza masomo, ikiwamo kuwapa mwongozo wa matumizi mazuri ya mikopo ya elimu wanayopewa.

Nasema wanapaswa kupewa mwongozo wa masuala mbalimbali kwenye suala la mkopo kwani wapo waliowatangulia ambao wameutumia vibaya kwenye masuala ya anasa ikiwamo kushindana kumiliki simu na redio za gharama huku wakisahau kwamba watatakiwa kulipa fedha hizo mara watakapohitimu na kuajiriwa au kujiajiri.

Vyuo vinapaswa kubeba jukumu la kuwapa mwongozo sahihi wanafunzi hao kwa sababu wazazi au walezi wengine hawatambui njia za kuwaelimisha vijana wao hasa kwa maisha ya chuo, kutokana na kwamba hawakufika huko.

Taasisi mahsusi zinazohusika na malezi zikiwamo taasisi za dini zinazotambulika nchini, shule na nyinginezo hazitimizi wajibu wao ipasavyo, hivyo kuliacha suala hili mikononi mwa vyuo husika. Hali hiyo imesababisha uwepo wa matukio ya ukatili na kuvunjika kwa uhusiano na migogoro inayozua chuki miongoni mwa jamii, jambo ambalo linakwamisha maendeleo.

Hapa tuwekane wazi kwamba ni kweli wapo wazazi au walezi ambao wamekuwa wakikwepa majukumu yao ya kuzungumza na vijana katika kuwaelimisha kuhusu masuala muhimu.

Kuwasaidia kujitambua, kudhibiti mihemko, kuzingatia masomo, matumizi ya fedha, upendo na ushiriki wao kwenye masuala ya maendeleo ni mambo muhimu kufundishwa wanafunzi wapya vyuoni.

Wakati Serikali inanadi Tanzania ya viwanda, ukweli ni kwamba kama kwenye jamii kuna vijana ambao hawajielewi, wamekosa mwelekeo kutokana na migogoro ya kifamilia na kijamii hawawezi kuwa na utulivu utakaoibeba dima hii nzuri ya Taifa letu.

Vijana wakiwa na akili iliyotulia, inayoweza kuwaongoza kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za uzalishaji mali iwe kwa kuajiriwa ama kwa kujiajiri ni tunu muhimu.

Columnist: mwananchi.co.tz